Wednesday, March 8, 2017

Makamu wa Rais Mama Samia alaani na kukemea vikali vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea katika jamii

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amelaani na kukemea vikali vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea katika jamii na amewataka wananchi kote nchini kushirikiana katika kukabiliana na vitendo hivyo nchini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo tarehe 8-March-2017 wakati akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji wa Tanzania (TBC) mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema vitendo hivyo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinamchukiza sana hivyo ametoa wito maalum kwa wananchi na wadau wote bila kujadili dini, kabila wala rangi kupambana ipasavyo na vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma jitihada za kumkwamua mwanamke kiuchumi.

Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema anafurahishwa na hatua na jitihada zinazochukuliwa na wanawake kote nchini katika kujikwamua kiuchumi kwa kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali katika kuelekea katika uchumi wa viwanda.

Amesema jukumu kubwa la serikali ya awamu ya Tano ni kuhakikisha wanawake wanaboreshewa ipasavyo mazingira ya kufanyia kazi hasa shughuli za ujasiriamali ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.

“Inapofika katika shida zetu wanawake ni lazima tuwe na kitu Kimoja na sauti Moja katika kulinda na kutetea haki zetu bila kujali itikadi za kisiasa”Amesisitiza Makamu wa Rais.

Katika uundaji wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi nchini, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na kutaka mikoa na wilaya ambazo bado haijaunda majukwaa hayo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo.

Ameeleza kuwa lengo la uundaji wa majukwaa hayo katika ngazi ya wilaya na mikoa nchini ni kuwakutanisha wanawake pamoja katika kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili ikiwemo tatizo la masoko za bidhaa wanazozizalisha.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa majukwaa hayo ambayo yameanza kuundwa katika mikoa mbalimbali nchini yatakuwa sio ya kisiasa.

Katika Mahojiano hayo na mtangazaji Shaban Kissu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mjini DODOMA, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu ametumia sehemu ya mahojiano hayo kwa kuwatakia heri na mafanikio wanawake wote nchini katika kuadhimisha Siku ya wanawake Duniani.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake Duniani ni “Tanzania ya Viwanda,Wanawake ni msingi wa mabadiliko ya Kiuchumi”.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dodoma. 8-Mar-2017

No comments: