Wednesday, March 22, 2017

MAKACHERO SARPCCO WAJADILI UHALIFU UNAOVUKA MIPAKA.


Na. Frank Geofray-Jeshi la Polisi.

Wakuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai kusini mwa Afrika wametakiwa kuongeza ushirikiano katika kubadilishana taarifa za wahalifu na uhalifu unaovuka mipaka ili kuufanya ukanda wa kusini mwa Afrika kuwa salama.

Wito huo umetolewa na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki mjini Bagamoyo alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Upelelezi wa Polisi kutoka Shirikisho la Wakuu wa Polisi kwa nchi za kusini mwa Afrika (SARPCCO) unaofanyika sambamba na kamati za ufundi za SARPCCO kwa lengo la kupanga mikakati ya kupambana na uhalifu na wahalifu.

Kaniki alisema ili kuwabaini wahalifu kwa urahisi ni vyema ushirikiano wa kubadilishana taarifa ukafanyika kwa haraka hasa kwa kuimarisha teknolojia ya habari na mawasiliano na mafunzo kwa maafisa wa Polisi ili kuwajengea uwezo wa kubaini mapema viashiria vya uhalifu katika maeneo yao.
Aidha aliziomba Serikali za nchi wanachama kuendelea kutenga bajeti zinazokidhi mahitaji ya majeshi ya Polisi ili kuyawezesha kufanya kazi kwa ufanisi ambapo pia aliyataka majeshi hayo kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha zinazotengwa kwa lengo la kuimarisha mifumo ya kuzuia na kupambana na uhalifu.

Kwa upande wake Mkurungezi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini DCI Robert Boaz alisema umoja huo utaendelea kuandaa oparesheni za pamoja katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka unaohusisha wizi wa magari, dawa za kulevya, biashara haramu ya usafirsishaji wa binadamu, uharamia, pamoja na ujangili.

Boaz alibainisha kuwa mkutano huo utajadili kwa kina utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano wa Wakuu wa Polisi uliofanyika mwezi Septemba mkoani Arusha pamoja na kuweka mikakati endelevu ya kukabiliana na uhalifu.

Naye Mkuu wa Shirikisho la Polisi wa Kimataifa (INTERPOL) Kanda ya Kusini Bw. Mubita Nawa alisema umoja huo umepata mafanikio makubwa kutokana na oparesheni mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika mara kwa mara katika kukabiliana na uhalifu ambapo amesema biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu bado ni changamoto kwa nchi wanachama.

Shirikisho la Wakuu wa Polisi kusini mwa Afrika (SARPCCO) lipo chini ya Uenyekiti wa Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania ambapo hivi sasa umoja huo unaundwa na nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesotho, Mauritius, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Shelisheli.
Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahmani Kaniki akisaluti kwa wimbo wa taifa kabla ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kamati ndogo za kiufundi za shirikisho la wakuu wa Polisi wan chi za kusini mwa afrika SAPRCCO. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika Bagamoyo mkoani Pwani kujadili mikakati ya kukabili uhalifu unaovuka mipaka. Kushoto ni Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya Jinai DCI, Robert Boaz. Picha Na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.
Naibu Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Abdulrahmani Kaniki akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kamati ndogo za kiufundi za shirikisho la wakuu wa Polisi wan chi za kusini mwa afrika SAPRCCO. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika Bagamoyo mkoani Pwani kujadili mikakati ya kukabiliana uhalifu unaovuka mipaka. Picha Na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.
Naibu Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Abdulrahmani Kaniki akionyesha zawadi kutoka kwa Mkuu wa Interpol kanda ya kusini (kulia) baada ya kutoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kamati ndogo za kiufundi za shirikisho la wakuu wa Polisi wan chi za kusini mwa afrika SAPRCCO. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika Bagamoyo mkoani Pwani kujadili mikakati ya kukabiliana uhalifu unaovuka mipaka. Picha Na Hassan Mndeme-Jeshi la Polisi.

No comments: