Wednesday, March 29, 2017

MAHAKAMA KUU KANDA YA MWANZA YAJIPANGA KUONDOSHA MLUNDIKANO WA MASHAURI


Na Mary Gwera, Mahakama.

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Mwanza imejipanga kuondoa Mashauri yote yenye umri zaidi ya miaka miwili yaliopo katika Kanda hiyo ili kuendana na azma ya Mahakama ya Tanzania ya kutokuwa na mlundikano wa kesi katika Mahakama za ngazi zote nchini.

Hayo yalisemwa na Jaji Mfawidhi, Kanda ya Mwanza, Mhe. Robert Vincent Makaramba katika Mahojiano maalum aliyofanya na Mwandishi wa habari hii hivi karibuni ofisini kwake, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza.

“Mbali na agizo la Mahakama la kutaka kila Mahakama ishughulikie mashauri ya muda mrefu Mahakamani, Mahakama, Kanda ya Mwanza tayari tulishajipanga katika kuondosha Mashauri haya, na kila Jaji amejipangia namna ya kusikiliza na kutolea maamuzi mashauri hayo,” alisisitiza Jaji Makaramba.

Aliongeza kuwa ili suala hili liweze kufanikiwa ni vyema kuwa kitu kimoja na Wadau wa Mahakama kuwezesha zoezi hili kufanikiwa na vilevile kuwa na rasilimali wezeshi kama fedha.

Aidha; ili kuweza kufanyika kwa zoezi hili la kuondoa mlundikano wa Mashauri Mahakamani, Majaji wote saba (7) wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na Naibu Msajili na Mtendaji wa Mahakama walikutana na Wadau wa Mashauri ya Jinai na Madai ili kujadili namna bora ya kuondosha mashauri yenye umri wa miaka miwili Mahakamani.

Kwa upande wake, Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Eugenia Rujwahuka alisema kuwa zoezi la kuondosha mashauri haya linatakiwa liwe limekamilika kufikia mwezi wa tano mwaka huu.

“Kikao hicho kilichojumuisha Wadau mbalimbali kama Mawakili, Waendesha Mashitaka, Magereza n.k, kililenga katika kujipanga ili kufanikisha usikilizaji wa Mashauri ya Mauaji katika vikao maalum vitakavyoanza Aprili, 24, mwaka huu hadi hadi Mei, 24 mwaka huu,” alisema Naibu Msajili.

Mhe. Rujwahuka aliongeza kuwa jumla ya Mashauri 107 yamepangwa kusikilizwa katika vikao hivyo ambavyo vitafanyika Tarime, Sengerema, Magu, Geita, Mwanza na Musoma.

Hata hivyo; katika kikao hicho kati ya Mahakama na Wadau wake walikubaliana kushirikiana ili kufanikisha zoezi zima la uondoshaji wa mrundikano wa mashauri.

Katika muendelezo wa uboreshaji wa huduma ya Utoaji haki nchini Mahakama ya Tanzania imedhamiria kuondoa mlundikano wa kesi katika Mahakama zake.


Baadhi ya Watumishi wa Mahakama na Wadau wakiwa katika kikao hicho.
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza wakiwa katika kikao pamoja na Wadau wa Mahakama wa Kanda hiyo (hawapo pichani) kilichofanyika hivi karibuni, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Eugenia Rujwahuka.


Pichani ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Robert Vincent Makaramba.
Afisa Habari, Mahakama, Bi. Mary Gwera akiwa katika Mahojiano maalum na Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Robert Makaramba ofisini kwake, Mahakama Kuu-Mwanza. 
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza akiongea jambo katika kikao hicho, pamoja nae wanaoonekana katika picha ni baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza ambayo ina jumla ya Majaji saba (7). 

No comments: