Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kamishna mstaafu Zelote Stephen
amelipongeza jeshi la polisi Mkoani Rukwa kwa kufanikiwa kukamata kilo mbili za
madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni heroin na lori la scania lililosheheni
pombe za viroba lililokuwa likitokea Mbeya na kuingia Rukwa kwa njia za panya.
Jeshi la polisi Mkoani Rukwa limemtia nguvuni Mtuhumiwa
wa madawa ya kulevya Linus Tenda Kamwezi (50) mfanyabiashara mkazi wa kizwite
katika manispaa ya sumbawanga aliyebainika kuyaficha madawa hayo katika maua
yaliyokuwa yamezunguka nyumba yake.
“Pamoja na kwamba mna-resource ndogo lakini kazi
mnayoifanya ni kubwa sana, nawapongeza kwa kitendo hiki na mwendelee kushika
kamba hiyo hiyo dhidi ya vita hii ya madawa ya kulevya ambayo si ya jeshi la
polisi peke yao bali ni la wananchi wote wa nchi ya Tanzania,” Zelote Stephen
alieleza.
Sambamba na hilo Kamanda wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando
alifafanua kuwa watu watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kukutwa na
lori aina ya Scania lililosheheni pombe zenye vifungashio vya nailon maarufu pombe
za viroba wakitokea Mkoani Mbeya kuelekea Rukwa.
Lori hilo lilikuwa na pombe aina tatu za
konyagi,valuer na zanzi cream vikiwa ni jumla ya katoon 364 ndani ya gari no.
T. 402 AFC Scania likiwa ni mali ya Kanji Lanji.
Watuhumiwa hao ni
Tuntufya Nicodema, (69), Dereva, mkazi wa Mbeya, Julio Fungameza Myovera, (57)
mfanyabiashara, mkazi wa chanji na Furaha Erasto (29), mkazi wa mbeya, tandiboi.
Taarifa za Kukamatwa kwa
lori hilo zilitolewa na wasamaria wema waliloliona lori hilo likiacha njia kuu
na kuingia katika njia za panya katika Kijiji cha Nambogo Kata ya Lwiche,
Wilayani Sumbawanga na kuamua kuripoti polisi.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alitoa onyo kali kwa vijana
wanaotumia pombe za viroba na kuwatahadharisha wakae navyo mbali ili kuongeza
nguvu kazi ya taifa na kutoa mchango wao katika serikali ya awamu ya tano
iliyolenga kukuza viwanda.
Zelote alisema,”kuna vijana wao wakilala wanafikiria
viroba, wakiamka wanafikiria viroba, sasa ole wao wale watakaokamatwa na
viroba.”
Nae Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa alitoa
onyo kwa wafanyabiashara wote kuacha kuagiza wala kuuza pombe hizo kwani
zimezuiliwa na kuwakikishia wananchi kuwa hataruhusu pombe hizo aina ya viroba
kuingia ndani ya mkoa wake bila kukamatwa.
“ Mfanyabiashra yoyote asijisumbue kwa namna yeyote
ile haitapenya tumetega kila mahala, na wananchi msipende kutumia pombe hii,
tukikukuta hata kama una kiroba mfukoni ni sawa na kukutwa na gongo au bangi,
kwahiyo jihadharini, msinunue pombe hizi ili wauzaji washinndwe kuzalisha na
kuwadodea,” Kamanda George Kyando alisisitiza.
No comments:
Post a Comment