Tuesday, March 7, 2017

Jokate aanzisha mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa kike

Mrembo mwenye vipaji lukuki nchini, Jokate Mwegelo ameanzisha mpango maalum wa kufundisha somo la ujasiriamali kwa wanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari ya Majani ya Chai iliyopo Vingunguti katika Manispaa ya Ilala.

Jokate ataanza mafunzo hayo maalum kwa wanafunzi wa kike kuanzia wiki ijayo na lengo la mafunzo hayo ni kuwapa ufahamu wanafunzi hao na kuanzisha biashara zao mara baada ya kumaliza elimu yao ya sekondari.

Alisema kuwa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi ni muhimu kwani yanawawezesha kujiandaa vizuri kukabiliana na maisha mara baada ya kuhitimu masomo yao ya sekondari na kushindwa kuendelea na masomo ya ngazi ya juu.Kwa mujibu wa Jokate, unaweza kusoma mpaka Chuo Kikuu ndani na nje ya nchi, lakini bado utakabiliana na ugumu wa kupata ajira ambazo kwa sasa ni haba.

“Kuna wengine wamesomea taaluma fulani  kwa ngazi ya Chuo Kikuu lakini mpaka sasa hawana ajira na kukata tama katika maisha, pia unaweza kufanya kazi tofauti na taaluma uliyosomea, lakini kwa ujasiriamali ni tofauti, utajifunzi jinsi ya kupata mtaji, kukopa na kurejesha, kufanya biashara gani na mbinu zake,”

“Mfano halisi mimi mwenyewe, nimesomea mambo tofauti na kazi ninazozifanya ni tofauti, ni mbunifu wa mitindo, mavazi, muigizaji wa filamu, mwanamuziki na pia ni mfanyabiashara, haya yote sikusomea, ila najivunia kwani ndiyo yanaendesha maisha yangu, wanafunzi wana vipawa tofauti, naamini katika programu hii nitapata wengi na kupata mafanikio,” alisema Jokate.

Alisema kuwa atakuwa anafundisha mafunzo hayo mara moja kwa wiki kuanzia wiki ijayo. “Nimeamua kuanza rasmi siku ya wanawake duniani, maandalizi yamekamilika na nawaomba wanafunzi wajiandae kwani mafunzo ni mazuri na yatawajengea moyo wa kujiamini kwani si kila anayesoma anatakiwa kuajiliwa,” alisema.
Jokate Mwegelo akicheza muziki na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Majani ya Chai ya Ilala wakati wa mahafari ya mwaka jana.
Jokate Mwegelo akikabidhi zawadi kwa mmoja wa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Majani ya Chai wakati wa maafali ya mwaka jana ya kidato cha nne.

No comments: