Na Othman Khamis Ame, OMPR
Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa miundombinu ya Ujenzi ya Garware
yenye Makao Makuu yake Mjini Mumbai Nchini India imeonyesha nia yake
ya kutaka kujenga Ukumbi Mpya wa Kisasa wa Kimataifa wa Mikutano
Zanzibar endapo itapata fursa ya kufanya kazi hiyo.
Uwamuzi huo umekuja kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na
mpango wa Kutaka kujenga Ukumbi wenye hadhi hiyo katika azma yake ya
kuimarisha Sekta ya Utalii inayoonekana kuimarika na kuleta ufanisi
mkubwa.
Mkurugenzi Miradi wa Kamuni Garware Bwana Deepak Menghnani
alithibitisha hilo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mwishoni mwa ziara ya Wiki Moja ya
Ujumbe wa Zanzibar hapo katika Hoteli ya Kimataifa ya Eros Mjini New
Delhi India.
Bwana Deepak Menghnani alimthibitishia Balozi Seif kwamba Wahandisi
wa Kampuni ya Garware iliyoanzishwa karibu miaka sita iliyopita wana
uwezo wa Kujenga Jengo la Mikutano katika kipindi kisichozidi miaka
Mitatu kwa mujibu wa uwezo wa mahitaji ya muhusika.
Alisema teknolojia rahisi inayotumika katika Kampuni hiyo imewawezesha
Wataalamu na Wahandisi wake kuendesha ujenzi wa Mjengo tofauti ikiwemo
Hospitali, Skuli, Ofisi za Serikali na hata Taasisi Binafsi pamoja na
nyumba za Makaazi kwa bei inayomuwezesha mtu wa kawaida kumudu
kununua.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa miundombinu ya
Ujenzi ya Garware alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba
Taasisi hiyo ya ujenzi imekuwa ikishirikiana na Wahandisi waliobobea
kutoka Nchini Misri ili kuiwezesha kuwa na uhimili wa Kimataifa.
Bwana Deepak Menghnani alisema Garware tayari imeshatoa huduma za
ujenzi katika Mataifa ya Bukinafaso,Sri Lanka na Dubai ndani ya
kipindi cha miaka Minane tokea kuanzishwa kwake.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuuandalikia barua ya
mualiko Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni hiyo katika muda mfupi ujao ili
kujionea mazingira ya Zanzibar na kuona hatua gani zinastahiki
kuchukuliwa katika mwanzao wa kuelekea kwenye mpango huo wa ujenzi wa
Ukumbi wa Kimataifa.
Balozi Seif alisema Zanzibar imeshafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika
uimarishaji wa Sekta ya Utalii lakini kinachokosekana kwa wakati huu
ni uwepo wa Ukumbi wa Kimataifa unaotoa fursa kwa Wageni na hata
Nchi
rafiki kuelekeza nguvu zao za kufanya makongamano, Mikutano na hata
Vikao vya Kimataifa.
“ Zipo kumbi za Mikutano zinazotumika katika baadhi ya Mahoteli Mjini
na sehemu za Vijijini Zanzibar lakini hazikidhi mahitaji halisi
kutokana na udogo wake ”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema ipo mikutano na baadhi ya semina za Kimataifa
zinazopangwa kufanyika Visiwani Zanzibar lakini wajumbe wa Mikutano
hiyo hulazimika kuishi mbali na maeneo yao ya mikutano jambo ambalo
huleta usumbufu wa kujipangia mambo yao mengine binafsi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amemaliza
ziara yake Nchini India na sasa amewasili Dubai kwa Mapumziko mafupi
ya siku mbili na baadae atarejea Nchini Tanzania kuendelea na majukumu
yake.
No comments:
Post a Comment