Monday, February 27, 2017

Serikali kutoa matrekta ili kuinua kilimo biashara kwa wanawake.



SERIKALI imeahidi kutoa pembejeo za kilimo cha kisasa yakiwemo matrekta kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kupitia taasisi inayojihusisha na kuendeleza wanawake katika kilimo Tanzania (CAWAT) ili waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo cha kisasa hususani cha kibiashara.

Ahadi hiyo ya Serikali ya serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha kwa Niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza kwenye harambee kukusanya fedha kwa ajili ya kuwezesha mradi wa kuwajengea uwezo wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara iliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Land O’ Lakes kwa kushirikiana na CAWAT na kufanyika jijini Dar es salaam mwshoni mwa wiki.

“Serikali ipo tayari kutoa pembejeo hizo za kilimo cha kisasa yakiwemo matrekta bora kabisa ambayo yataolewa kwa vikundi vya kina mama wanachama wa CAWAT ambao wataonyesha nia na uwezo wa kutekeleza kilimo cha kisasa hususani cha kibiashara. Zaidi wanufaika hao watahakikishiwa soko la uhakika kwa kile watakachozalisha,’’ alisema Ole Nasha ambae pia yeye binafsi alitoa mchango wa mil. 2 kwenye harambee hiyo.

Alisema serikali ipo tayari kushirikiana na taasisi yeyote nchini yenye nia ya dhati katika kuleta mabadiliko yenye tija yatakayoliwezesha taifa kuongeza kasi yake katika kuelekea uchumi wa viwanda na mapinduzi ya kilimo.

Hatua hiyo ya serikali inakwenda sambamba na ahadi ya Benki ya Maendeleo ya kilimo nchini (TADB)kwa CAWAT ambapo kupitia Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wake Bw Francis Assenga, ilitangaza kwenye warsha hiyo kwamba ipo tayari kushirikiana na CAWAT ili kutoa ushauri utakaoambatana na fursa ya kutenga sh milioni 600 kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake katika kuendesha kilimo hicho cha kibiashara kupitia taasisi hiyo.

"Kupitia ushirikiano wetu huo na CAWAT ni wazi kwamba TADB tunakwenda kufanya mabadiliko makubwa kwenye sekta ya kilimo hasa cha kisasa kupitia wanawake nchini. Baada ya kupitia malengo ya CAWAT tumelizika moja kwa moja kuwa tuna kila sababu ya kushirikiana nao ili kuifikisha hii nchi kwenye uchumi wa viwanda kupitia kilimo,’’ alisema.

Katika harambee hiyo kiasi cha pesa zaidi ya milioni 27 kilipatikana ikiwa ni ahadi na taslimu, huku pia ikielezwa kuwa Balozi za Japan na Switzerland hapa nchini zimeonyesha nia ya kusaidia miradi mbalimbali itakayoendeshwa na taasis hiyo ya CAWAT.

Awali wakizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya CAWAT Dk Victoria Kisyombe pamoja na Mkurugenzi Mradi kutoka taasisi ya Land O’ Lake Dr Rose Kingamkono walisema kwa sasa taasisi ya CAWAT ipo kwenye mchakato wa awali wa kuanza kujitegemea yenyewe kiuendashaji bila kutegemea msaada iliyokuwa ikiupata kutoka shirika la msaada la Marekani USAID. 


 Mkurugenzi Mradi kutoka taasisi ya Land O’ Lake Dr Rose Kingamkono akizungumza kwenye harambee ya kukusanya fedha  kwa ajili ya kuwezesha mradi wa kuwajengea uwezo wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
 Baadhi ya washiriki wa harambee hiyo.
 Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha  akizungumza kwenye harambee hiyo.  Ole Nasha alimuwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye harambee hiyo iliyofanyika kwa mafanikio makubwa!
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini  (TADB) Bw Francis Assenga akizungumza kwenye harambee hiyo.Benki hiyo ilitangaza nia yake ya kutenga sh milioni 600 kuwezesha miradi ya taasisi  ya CAWAT.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi inayojihusisha na kuendeleza wanawake katika kilimo Tanzania (CAWAT)  Dk Victoria Kisyombe (Kushoto) akipeana mkono wa pongezi na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Bw Francis Assenga kwenye harambee hiyo ikiwa ni ishara kuanza kwa ushirikiano baina ya taasisi hizo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mradi kutoka taasisi ya Land O’ Lake Dr Rose Kingamkono.
 Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa taasisi za CAWAT, Land O’ Lake, SAGCOT pamoja na maofisa wa juu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) kwenye harambee hiyo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha akipeana mkono wa pongezi na Meneja Uhusiano wa Mfuko wa pesheni wa PPF, Lulu Mengele ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa mfuko huo kwenye harambee hiyo.

No comments: