Stori na Biseko Ibrahim.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka watumishi wa Wizara hiyo Sekta ya
Uchukuzi kutumia vizuri fursa ya kuhamia Dodoma kwa kuwatumikia watanzania kwa
uadilifu na weledi.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati
akiwaaga watumishi wa Sekta ya uchukuzi wa awamu ya kwanza ambao wameondoka leo
kuelekea mjini Dodoma.
“Nawapongeza kwa kupata fursa ya kuwa
katika awamu ya kwanza katika Wizara hii kuhamia Dodoma fahamuni hii ni fursa
na si changamoto kwani hatua hii inasogeza huduma karibu na wananchi hivyo
watumikieni kwa moyo”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema kuwa nia ya Serikali
ni kuhakikisha watumishi wake wanahamia Dodoma na kuendelea na utekelezaji wa majukumu
yake kwa wananchi.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Sekta ya
Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema awamu ya kwanza ya watumishi zaidi ya
45 inahamia Dodoma mwezi huu na Awamu ya pili itaanza mwezi wa Machi na
watumishi wote wa sekta ya uchukuzi watakuwa Dodoma ifikapo
Agosti mwaka huu.
“Watumishi wa Sekta ya Uchukuzi wanaohamia
Dodoma katika awamu ya kwanza ni pamoja na Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi, Wakurugenzi
na Wakurugenzi wasaidizi, wakuu wa vitengo na maafisa waandamizi”, amesisitiza Dkt.
Chamuriho.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Uchukuzi), Dkt. Leornard Chamuriho kabla ya kuwaaga watumishi wa Wizara hiyo wanaohamia Dodoma leo, jijini Dar es salaam. Picha na Biseko Ibrahim.
No comments:
Post a Comment