Na Stella Kalinga, SIMIYU
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein ametimiza ahadi ya kutoa sadaka ya
vifaa vya ujenzi wa Msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi, ambao ni
Msikiti mkuu Simiyu.
Rais Shein alitoa ahadi hiyo mwezi
Oktoba 2016 wakati alipokuwa Mkoani Simiyu kuwaongoza Watanzania katika
Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wiki ya Vijana na Kumbukumbu
ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl.Nyerere.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya
vifaa hivyo,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka amemshukuru Mhe.Rais Shein
na kubainisha kuwa ujio wake mwaka jana umeleta mafanikio makubwa kwa mkoa na
kujenga uhusiano mazuri kati ya Mkoa wa Simiyu na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Mtaka amesema ujio wa Dkt Shein mkoani
Simiyu umefungua milango ya ushirikiano wa kibiashara kati na Zanzibar, ambapo
alimtuma Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe.Riziki Pembe Juma mwezi Desemba
mwaka jana kuja kuona Chaki za Maswa na sasa Mkoa huo unauza chaki Zanzibar.
Aidha, ameongeza kwa kupitia ujio
wake alimtuma Waziri wa Biashara,Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali kuona
fursa za biashara na sasa wananchi wa Simiyu wamehakikishiwa soko la Mchele na
mazao ya mikunde Zanzibar kupitia makubaliano yatakayowekwa kati ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Mkoa wa Simiyu.
"Dkt.Shein Akiwa Simiyu amefanya ya
kimwili na ya kiroho sisi kama Mkoa tutakuwa mashahidi wa kazi na utumishi wake;kupitia
yeye tumefanya biashara Zanzibar, kupitia yeye Msikiti wetu unajengwa kwa
sadaka yake na kupitia yeye tumefungua milango mipana ya ushirikiano"
alisema.
Amesema Serikali ya Mkoa iko
tayari kushirikiana na BAKWATA katika kuhakikisha mapungufu yatakayojitokeza
yanatatuliwa ili Msikiti wa Kisasa na Ofisi za kisasa za BAKWATA zinajengwa
ambazo zitaendana na hadhi ya makao makuu ya Mkoa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi na
waumin wa Kiislamu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mahamoud Kalokola amesema
anamshukuru Rais Shein kwa sadaka yake hiyo ambayo ina thawabu kubwa kwa
Mwenyezi Mungu.
"Tunamshukuru sana Mhe.Rais Shein
kwa sadaka yake na tunamwomba Mwenyezi Mungu amuongezee pale alipotoa, maana
Quran inasema ajengaye msikiti anajijengea nyumba peponi" alisema.
Vile vile Sheikh Kalokola ametoa wito
kwa watu wote wenye mapenzi mema kusaidia mahali popote misikiti inapojengwa
ili kuwawezesha waumin kupata mahali pa kuswali jambo ambalo litawapa thawabu
kwa Mwenyezi Mungu.
Vifaa vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Ali Mohammed Shein kama sadaka yake
ni saruji,nondo, rangi,mbao n.k ikiwa ni pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya
malipo ya mafundi na vimewasilishwa kwa niaba yake na Ally Habshy Abdallah, ili
kukamilisha msikiti wa MASJID RAUDHAL.
No comments:
Post a Comment