Na Salum Vuai, MAELEZO
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdallah, leo amefungua mkutano wa pili wa kamati za kusimamia chanjo na matumizi ya dawa barani Afrika na kutahadharisha changamoto zinazotokana na kuibuka kwa dawa zilizo chini ya kiwango.
Katika mkutano huo wa siku tano unaofanyika kwenye hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani mjini Unguja, Katibu Mkuu huyo alisema nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto kadhaa katika kusimamia na kusajili dawa. Alisema baadhi ya changamoto hizo zinahitaji kuelezwa na kuchukuliwa kama suala la dharura.
Asha alieleza kuwa, dawa bandia na chanjo, uendeshaji wa kliniki zilizo chini ya kiwango na usimamizi mdogo wa sheria na miongozo juu ya matumizi ya dawa, yanahitaji kuwekewa mikakati maalumu ili kuweza kutoa huduma bora za chanjo katika nchi za Afrika.
“Ikiwa mamlaka ya usimamizi, AVAREF ina kazi kubwa kuhakikisha usalama wa chanjo, kuepuka urasimu na ucheleweshaji ambao unaweza kuwakosesha huduma wananchi wengi,” alisisitiza.
Alisema katika kuhakikisha ubora na usalama wa chanjo na dawa mbalimbali katika soko, Zanzibar iliamua kuanzisha Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDB) mwaka 2007.
Alizitaja kazi za bodi hiyo kuwa ni kuratibu, kusajili na kufuatilia usalama wa dawa, bidhaa za chakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria namba 2 ya mwaka 2006 inayohusu bidhaa hizo.
Aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na kamati hizo ikitambua umuhimu wa kuwapatia wananchi huduma bora za afya kwa kusimamia utoaji wa chanjo na dawa zilizo sahihi.
Mapema, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) anayefanya kazi hapa Zanzibar Dk. AndeMichael Ghirmay, alisema katika miaka hii, nchi za Afrika zimekuwa zikiathirika kwa maradhi yanayoambukiza na yale yasiyoambukiza, mengi kati yao yakiwa hayana dawa wala chanjo.
“Zikisukumwa na mahitaji ya dawa na chanjo zilizo bora, ya haraka na rahisi, nchi za Afrika zinazidi kuwa shabaha ya wamiliki wa viwanda vya dawa katika mkakati wao wa kuendeleza dawa na chanji mpya,” alisema.
Hata hivyo, alisema mfumo wa utengenezaji na utumiaji wa dawa na chanjo hizo, bado ni changamoto kwa kamati za maadili na usimamizi, katika kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa.
Kutokana na sababu hizo, Dk. Ghirmay alisema mnamo mwaka 2006, WHO iliunda chombo cha kuratibu na kusimamia mfumo wa utoaji dawa na chanjo (AVAREF) ili kuchochea maendeleo na ufanisi katika suala hilo.
Mkutano huo unashirikisha zaidi ya wajumbe 40 kutoka nchi mbalimbali za Afrika, pamoja na wawakilishi wa Mamlaka za Mashirikisho ya Dawa (FDA) kutoka Marekani na Canada, sambamba na wataalamu na wadau wa masuala ya chanjo na dawa kutoka taasisi tofauti barani Afrika.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdalla akifungua mkutano wa siku tano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Zanzibar Dkt. Andemichael Ghirmay akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo na kuelezea juu ya majukumu ya kamati hizo.
Mwakilishi wa (WHO-AFRO) Dicky Akanmoni akiwasilisha mada juu ya usimamizi wa matumizi sahihi ya dawa katika mkutano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika ulioanza leo Februari 20, 2017 mjini Zanzibar.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika siku ya kwanza ya mkutano huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdalla (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika unaofanyika Zanzibar.
Mkurungezi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa chanjo na matumizi ya dawa kando ya mkutano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika ulioanza leo Februari 20, 2017 katika hoteli ya Zanzibar Ocean View.Picha na Makame Mshenga-Maelezo.
No comments:
Post a Comment