Thursday, February 9, 2017

MHANDISI WA UJENZI MKOA ASIMAMISHWA KAZIMkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa huo wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya awali ya uchunguzi gharama za ujenzi wa Hospitali ya Mkoa
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa huo wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya awali ya uchunguzi wa gharama za ujenzi wa Hospitali ya Mkoa.
Baadhi ya Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu wakimsikiliza Katibu Tawala Mkoa huo, Ndg.Jumanne Sagini wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya awali ya uchunguzi wa gharama za ujenzi wa Hospitali ya Mkoa.


Na Stella Kalinga

Mhandisi wa Ujenzi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Deusdedit Mshuga amesimamishwa kazi kwa kukabiliwa na mashtaka matatu.

Akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini amesema Mhandisi huyo anashtakiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu aliyopewa kwa kiwango cha kuridhisha.

Amesema akiwa mtumishi wa umma kinyume na kipengele cha 8 cha sehemu"A" ya jedwali la kwanza la kanuni za Utumishi wa Umma, Tangazo la Serikali Na.168/2003; mtumishi huyo alishindwa kuandaa makadirio ya gharama za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa yenye uhalisia.

Aidha , Aliandaa makadirio ya Tsh46,106,456,000 yaliyosomwa mbele ya Mhe. Rais tarehe 11 Januari,2017 ambayo ni ya juu kuliko uhalisia. 

Shtaka la pili linalomkabili ni kufanya uzembe mkubwa wakati wa utekelezaji wa majukumu ya kazi iliyopewa kinyume na kipengele cha 13 cha sehemu "A" ya jedwali la kwanza la Kanuni za Utumishi wa Umma,Tangazo la Serikali na 168/2003;

Alitaja (1) kuandaa makadirio ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa Tshs.46,106,456,000 hali iliyosababisha Mhe Rais kusomewa taarifa ya gharama zisizo na uhalisia na(2) Kuandaa michoro ya taswira (3 D)isiyoendana na michoro halisi ya Hospitali ya Mkoa iliyooneshwa mbele ya Mhe.Rais

Shtaka la tatu ni kufanya kazi kwa kukiuka maadili ya taaluma yake wakati wa utekelezaji ya kazi aliyopewa kinyume na kipengele cha 14 cha Sehemu "A" ya Jedwali la kwanza la Kanuni za Utumishi wa Umma, Tangazo la Serikali Na.168/2003:- kwa (1) Kuandaa makadirio ya shilingi 46,106,456,000 ya gharama za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa bila kuzingatia mita za mraba za eneo, michoro na kusababisha gharama kubwa zisizo na uhalisia

(2) Kuandaa makadirio ya shilingi 3,009,640,000 yasiyo na uhalisia ili kugharamia ujenzi wa majengo ya msingi kuwezesha Hospitali kuwa "functional" kwa kupiga simu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Katibu Tawala wa Mkoa, Ndg..Jumanne Sagini ametoa wito kwa watumishi wa Umma mkoani humo kutekeleza majukumu waliyopewa kwa bidii, weledi na uadilifu ili kuepuka makosa ambayo husababisha watumishi kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

“Nikiwa kama mwajiri nimesikitishwa na kufadhaishwa na wataalam walioajiriwa ngazi ya mkoa kuishauri Sekretarieti ya Mkoa na kuzisimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuzishauri kitaalam, kutenda matendo yanayodhihirisha upungufu wa weledi, kushindwa kutekeleza majukumu na uzembe mkubwa” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa huo,Mhe. Anthony Mtaka amesema gharama zilizowasilishwa awali na wataalam hazikuwa na mchanganuo toshelevu na makisio hayakuwa na uhalisia, hivyo amemwomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli, kwa taarifa za upotoshaji zilizotolewa na wataalam wakati wa ziara yake Mkoani humo. 

“....kuna vitu vingine vilivyopachikwa kwenye ramani, wenye taaluma yao walipokutana ili kujustify hiyo bilioni 46.1 walishindwa kujustify kwenye ramani, kwa hiyo hatukuwa na uhalisia; baada ya mapitio ya kazi zote ilionekana Hospitali ya Mkoa wa Simiyu inaweza kujengwa kwa gharama ya bilioni 11.4 mule mule alimosema Rais” alisema Mtaka.

Makadirio ya awali ya Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa yalikuwa ni shilingi bilioni 46.1 na gharama hii haikukubaliwa na Mhe.Rais na badala yake akaagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kutembelea TBA Makao Makuu, ili kujifunza na kuona jinsi walivyoweza kujenga majengo ya hosteli ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa gharama ndogo ya shilingi bilioni 10 na akaahidi kutoa bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

No comments: