Saturday, February 18, 2017

MAMLAKA YA UENDELEZAJI KANDA MAALUM ZA KIUCHUMI (EPZA) NA KIWANDA CHA TOOKU VYATOZWA FAINI YA MILIONI 30 KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA


MAMLAKA ya Uendelezaji Kanda Maalum za Kiuchumi (EPZA)na Kiwanda kilichopo ndani ya Mamlaka hiyo ya Tooku kinachojishughulisha na utengenezaji wa nguo zimetozwa faini ya kiasi cha sh.mill 30 kwa kosa la kutililisha maji machafu katika makazi ya watu. 

Ambapo EPZA inapaswa kulipa faini ya Mill20 huku Kampuni ya TOOKU kulipa faini ya mill 10 na kuhakikisha zinarekebisha mifumo yake ya kupitisha maji taka ipasavyo na kuunganisha katika Mfumo maalum wa Dawasco . 

Akizungumza Jijini Dar es Salaam ,Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Muungano,Luhaga Mpina wakati wa ziara yake ya kukagua baadhi ya viwanda nchini,kuangalia hali ya mazingira ambapo aliambatana na Maofisa mbalimbali kutoka 

Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC),alisema faini hizo zinapaswa kulipwa ndani ya siku 14.Mpina alisema anahasira zaidi na taasisi za serikali zisizofata sheria ya mazingira na kutililisha maji machafu katika makazi ya watu. 

"Nina hasira na taasisi hizi za serikali kwani serikali yenyewe haiwezi kugeuka kupeleka sumu kwa wananchi wake, ambao muda wote inawazuia na kuwakinga wananchi hao hao wasipatwe na 
madhara,"alisema 

Alisema wanapokuta na taasisi ya serikali zinazokiuka miiko iliyoweka katika utunzwaji wa mazingira ni lazma wawapige faini kubwa zaidi kuliko taasisi binafsi ili kuweza kuwa mfano mkubwa kwa jamii.Mpina alisema Mamlaka hiyo ya Uendelezaji Kanda Maalum za Kiuchumi EAPZ ilisema kuwa mfumo wao wa kuyabeba maji taka na kuyapeleka katika mfumo rasmi wa maji taka wa Dawasco umeharibika lakini hawakuweza kuwaandikia NEMC barua ya taarifa juu ya matatizo hayo. 

"Nawataka EPZA ndani ya siku saba mfumo wa kupitishia maji taka wa EPZA uwe umetengenezwa na kukamilika hivyo kuzuia maji taka yanayotoka kutotoka tena kwa sababu yatakuwa yanaingia rasmi katika mfumo wa Dawasco,"alisema.Aidha alisema kwa upande wa Kampuni ya TOOKU yenye inatakiwa kufanya marekebisho makubwa katika mitambo yake ya kutibu maji taka kwani inaonekana kuwa na kasoro. 

"Sheria ya mazingira inakataza utililishaji huu wa maji taka katika mazingira kwani maji yanayotililishwa yanakuwa na kemikali mbalimbali ambazo zinadhuru wanyama,mimea na maisha ya binadamu,kwahiyo viwanda vyetu nchini hatuviruhusu kutililisha maji taka nje kwenda kwenye mazingira na endapo yatatililishwa yanapaswa kupimwa,kuhakikiwa na kudhibitishwa kuwa hayana madhara,"alisema . 

Aidha alisema katika ukaguzi walioufanya mamlaka hiyo na kiwanda hicho hakikuweza kuonyeshwa ubora wa maji yanayotililika kuja katika mazingira ya watu kwani maji yanayotililika kutoka katika Mamlaka hiyo na Kiwanda hicho cha yanatoka na rangi. 

Kwa Upande wake Mratibu wa Kanda ya Mashariki NEMC , Jafari Chimgege alisema katika kiwanda cha Tooku kimekuwa mbaya wa kutibu maji taka na kusababisha kumwaga maji machafu katika mazingira bila kuyatibu ambapo ni kinyume cha sheria. 

"Viwanda vinafahamu kuwa vinapomwaga maji machafu katika mazingira bila kuyatibu au kuyapeleka katika mifumo rasmi ni kosa,kiwanda hiki cha TOOKU na Mamlaka hii ya EAPZ vimefanya kosa,"amesema.Chimgege amesema maji yanayotilishwa na viwanda mbalimbali 
katika mito ni makosa kwani maji hayo yanakuwa na madhara kwa wananchi. 

Nae Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Muongozo,James Ngoitanile alisema wananchi wake wamekuwa wakipata shida na maji hayo wakati mwingine yanawaletea madhara.Amesema wapo watu wanaolima michicha ambao wanatumia maji ya mto huo kumwagilia hivyo yanavyochanganyika na maji hayo yanasababisha watu kula mbogamboga zenye kemikali.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina akiwa katika ziara ya ukaguzi wa Mazingira katika kituo cha uwekezaji cha EPZA, kilichopo Ubungo Jijini Dar es salaam. 
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina akiangalia shughuli za uzalishaji wa nguo katika kituo cha uwekezaji cha EPZA mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mazingira katika kituo hicho kilichopo Ubungo Jijini Dar es salaam. 
. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina akiangalia suruali aina ya Jinsi zinazozalishwa katika kituo cha uwekezaji cha EPZA wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa mazingira mapema hii leo Jijini Dar es salaam. 
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina akiangalia mfereji wa maji machafu yanayotiririshwa na kituo hicho ambayo yamekuwa ni kero kwa wananchi.

No comments: