Sunday, February 19, 2017

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akagua ujenzi wa barabara ya kinduni na Kichungwani

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akikagua jengo jipya la Skuli ya Msingi ya Kiombamvua lililojengwa na Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff kutekeleza ahadi za kusaidia huduma na Miradi ya Kijamii.Wa kwanza kulia ni Mshauri muelekezi wa Hoteli hiyo ya Sea Cliff ambae pia ni msimamizi wa Ujenzi wa jengo hilo la Skuli Nd. Yassir De Costa.
Balozi Seif mbae pia ni Mwakilisihi wa Jimbo la Mahonda akikagua Bara bara ya Kinduni iliyopitia Kichungwani na kuelekea Kitope iliyojengwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar katika kiwango cha kifusi.
Balozi Seif akizungumza na baadhi ya Wananchi wa Vijiji vya Kinduni na Kichungwani mara baada ya kuikagua bara bara iliyomo ndani ya Kijiji chao.Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahme Salum na Mbunge wa Viti Maalum Mh.Angelina Adam Malembeka.
Mzee Juma Abdulrahman wa Kijiji cha Kichungwani anayesumbuliwa na maradhi ya macho na Miguu akitoa shukrani kwa niaba ya wanakijiji wenzake mbele ya Balozi Seif kwa hatuanjema iliyochukuliwa na Serikali kuijenga bara bara yao.Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Ujenzi wa Bara bara ya Kinduni, Kichungwani na hatimae kuelekea Kitope unaofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utasaidia kuharakisha maendeleo ya Wananchi hasa wakulima wa Vijiji hivyo.

Alisema Ujenzi wa Bara bara hiyo ambao umo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM unatekelezwa kufuatia ahadi iliyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mstaafu wa Awamu ya Sita Dr. Amani Karume.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na baadhi ya Wananchi wa Vijiji vya Kinduni na Kichungwani baada ya kuikagua Bara bara hiyo iliyojengwa na Wahandisi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar katika kiwango cha kifusi kuanzia Kinduni hadi Kichungwani.

Alisema Bara bara hiyo itakapokamilika rasmi itarahisisha mawasiliano ya usafiri kwa Wananchi wa maeneo hayo ambao wengi wao wanajishughulisha na kazi za Kilimo mchanganyiko katika kujipatia riziki zao za kila siku.

Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi hao kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika hatua ya baadae ya Bara bara hiyo ni kuikamilisha katika kiwango cha lami ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu.

Mapema Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum alisema Bara bara ya Kinduni iliyopitia Kichungwani hadi Kitope ni miongoni mwa Bara bara za ndani lakini kwa agizo la Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein itajengwa katika kiwango cha Lami.

Mh. Mohamed alisema Ahadi zote za Chama cha Mapinduzi zilizotolewa kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 zitaendelea kutekelezwa na Wizara yake kwa upande wa Sekta ya Mawasiliano.

Alisema ahadi zozote zinazotolewa na Viongozi Wakuu popope pale ni agizo maalum linalostahiki Taasisi au watendaji wahusika kuzitekeleza kulingana na mazingira yaliyowazunguuka.

Naye Mzee Juma Abdulrahman akikaguliwa na Mh. Balozi Seif kutokana na hali yake ya afya Kijijini hapo kwa niaba ya wananchi wenzake aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua iliyofikia ya ujenzi wa Bra bara hiyo.

Mzee Juma alisema Bara bara hiyo iliyokuwa kilio cha miaka mingi kilicholeta changamoto na matatizo kwa Wananchi hao itakuwa mkombozi mkubwa hasa kwa wakulima pamoja na kizazi kijacho.

Alisema kero la Bara bara hiyo ilipelekea wananchi Vijiji hivyo wakati wa Awamu zilizopita walilazimika kukata miti ilimradi kupunguza usumbufu waliokuwa wakiupata hasa kwa akina Mama waja wazito wanapokwenda kujifungua.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alitembelea Jengo jipya la Skuli ya Msingi ya Kiombamvua lililomaliza ujenzi wake.

Jengo hilo limejengwa na Uongozi wa Hoteli ya Kimataifa ya Sea Cliff ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zake ilizotowa wakati wa Vikao vyake mbele ya Kamati ya Bandari ya Kiombamvua kwamba itasaidia huduma na miradi ya maendeleo ya Vijiji vinavyoizunguuka Hoteli hiyo.


Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments: