Thursday, February 23, 2017

MAKALA YA MAANDALIZI YA SIKU YA WANYAMAPORI DUNIANI 3/3/2017

Bw. Malima Mbijima akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chisingisa

TAWA wakishirikiana na Mradi wa kuhimarisha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), kwa kutumia wataalamu wake, inafanya ziara ya kutembelea vijiji vinavyozunguka Pori la Akiba Rungwa katika Wilaya ya Manyoni kwa kutoa elimu ya wanyamapori kwa njia za mikutano kufuatia maandalizi ya Siku ya Wanyamapori Duniani ambayo yanategemewa kuadhimishwa jijini Dar es Salaam tarehe 3/3/2017. Kauili mbiu ya Siku ya Wanyamapori Duniani ni ‘Vijana tushiriki katika Uhifadhi’

Elimu hii katika Wilaya ya Manyoni imeanza rasmi tarehe 18/2/2017 na itachukua muda wa siku kumi na kuhitimishwa tarehe 25/2/2017 inawashirikisha wataalamu wa Maliasili kutoka wilaya ya Manyoni  wakiwemo Afisa Misitu  na Afisa wanyamapori wa Wilaya ya Manyoni. Vijiji  vilivyoelimishwa ni kijiji cha Imalampaka, Sasilo na Ipululu. Vijiji vingine ambavyo vimelengwa kuelimishwa ni Simbanguru, Mpapa, Iseke,Nkonko,Damwelu,Doroto na Lulanga.
Msafara huo unaongozwa na Bw. Twaha Twaibu ambaye ni Afisa habari na Mahusiano wa TAWA ambaye ameongozana na Bw. Herman Nyanda naye kutoka TAWA anayeshughulikia Ushirikishwaji jamii katika  uhifadhi, Bw. Ramadhani Mdaile kutoka Pori la Akiba Rungwa nayeshughuka na Masuala ya Uenezi, Bw. Malima Mbijima kutoka mradi wa SPANEST na wataalamu wa maliasili kutoka Wilaya ya Manyoni.
  Bw. Twaha Twaibu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Imalampaka
Kwenye mikutano hiyo, Bw. Twaha aliwaelezea wananchi wa vijiji hivyo faida mbalimbali zitokanazo na uhifadhi wa wanyamapori, Sheria ya kuhifadhi wanyamapori Na.5 ya Mwaka 2009, suala la wanyamapori wakali na waharibifu, utaratibu wa kufuata na jinsi Serikali inavyowalipa wananchi wake kifuta jasho na machozi baada ya mashamba yao kuharibiwa na wanyamapori na wengine kujeruhiwa au kuuwawa na wanyamapori. 
Aliwaeleza kuwa Serikali yao kupitia Wizara ya Malaisili na Utalii inawajali sana na kuwaomba wasijihusishe na vitendo vya ujangili wa wanyamapori,
  
Aidha mtaalam kutoka mradi wa SPANEST Bw. Malima Mbijima alieleza kwamba mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ukiwa na lengo la kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori katika ukanda wa kusini mwa Tanzania unao jumuisha Pori la Akiba la Rungwa, Pori la Akiba Mpanga Kipengele, Hifadhi ya Taifa Ruaha na Kitulo,  ili wanyamapori hao waweze kuchangia zaidi maendeleo ya jamii katika kizazi cha sasa na vijavyo kupitia utalii na fursa nyingine. Shughuli za Utalii hapa Tanzania zinachangia asilimia 25 ya fedha za Kigeni.

Wananchi wa kijiji cha Imalampaka wakiwa kwenye picha ya pamoja

Bw. Ramadhani Mdaile akisisitiza suala la kutojihusisha na  ujangili wa wanyamapori na ukataji wa mbao katika Pori la Akiba, aliwaeleza wananchi kuheshimu mipaka ya Hifadhi ya Mapori ya Akiba kwa kuacha mita 500 kutoka hifadhi  wanapolima au kufanya shuguli zao.
Mita hizi ziko kisheria kwa kuzingatia Sheria ya Kuhifadhi wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009.
Bw. Herman Nyanda kutoka Makao Makuu ya TAWA aliwaeleza wananchi kuhusu faida na umuhimu wa kuanzisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori (WMAs) katika maeneo yao ya vijiji. Uanzishaji na utunzaji wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori ni njia mojawapo ambayo itawawezesha wananchi kunufaika na uhifadhi wa wanyamapori kupitia shughuli za uwindaji wa kitalii na utalii wa picha. 
Aliongeza kuwa, mbali na umuhimu wa WMAs katika utalii, maeneo haya ya uhifadhi yatawasaidia katika ufugaji wa nyuki, kupata kuni ambayo ndiyo nishati inayotumiwa na kutegemewa na wanakijiji pamoja kuhifadhi vyanzo vya maji katika vijiji. Ili kufanikisha katika ulinzi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori katika Jamii basi vijiji havinabudi kujiwekea mpango wa matumizi ya ardhi, kwani maeneo ya WMAs yanatengwa kwenye ardhi ya vijiji kwa kufuata na kuzingatia mpango wa matumizi bora ya Ardhi. 

Wataalamu kutoa halmashauri za wilaya ya Manyoni na Itigi walizungumzia ukataji ovyo wa misitu na upasuaji wa mbao ambao haufuati Sheria na kanuni za misitu. Vitendo hivi vimepelekea uharibi mkubwa wa mazingira katika wilaya yao ya Manyoni. 
Mtaalamu wa misitu alisisitiza kufuata Sheria na taratibu za uvunaji wa misitu. Aidha, Afisa wanyamapori wa Wilaya alizungumzia suala ya wanyama wakali na waharibifu wa mazao, pamoja na  taratibu za kufuata endapo wanapatwa na matatizo hayo. 
Alieleza na kufafanua viwango vya malipo kwa wananchi wanaopatwa na madhara ya wanyamapaori na kuwataka wasifanye shughuli za kijamii karibu na mipaka ya Pori la Akiba.




No comments: