TAARIFA
KWA UMMA
MAADHIMISHO YA SIKU
YA ARDHIOEVU DUNIANI TAREHE 2 FEBRUARI 2017
Kesho tarehe 2
Februari, 2017 ni maadhimisho ya siku ya Ardhioevu Duniani. Siku hii
inaadhimishwa duniani kote kwa kutoa elimu na kuwakumbusha
watu wote kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za ardhioevu.
Ardhioevu ni maeneo
ya ardhi yaliyopo kandokando na ndani ya Chemchem, Mito, Maziwa na mwambao wa
bahari wenye kina cha maji yasiyozidi mita sita wakati wa kupwa. Ardhioevu pia
hujumuisha Madimbwi, Mabwawa, Tingatinga na sehemu zote yanapokusanyika maji
kipindi kirefu cha mwaka.
Tanzania hujumuika
na nchi nyingine wanachama wa Mkataba wa “Ramsar” kuadhimisha siku ya ardhioevu
duniani Februari 2 kila mwaka. Ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya Ardioevu ni: "Ardhioevu
Hupunguza Athari za Majanga” (Wetlands for Disaster Risk
Reduction)".
Tafsiri ya kauli mbiu hii ni kwamba, Ardhioevu huzuia majanga
ya mafuriko yanayoweza kutokea katika pwani za bahari, hupunguza athari za
kiafya zinazoweza kujitokeza kutokana na madini hatarishi kama Zebaki,
hupunguza uwezekano wa kutokea kwa baa la njaa kwa kuwa maeneo okozi wakati wa
kiangazi kama vyanzo vya maji na chakula kwa binadamu na wanyama.
Ardhioevu pia
ni maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa chakula kama vile mpunga na mbogamboga na
chanzo cha maji yanayotumika kwenye kilimo cha umwagiliaji nchini. Arhioevu pia
ni sekta endeshi ya uchumi wa nchi kwa kuwa ni chanzo cha maji yanayotumika
kwenye kilimo, viwandani pamoja na uzalishaji wa umeme wa maji kwa gharama
ndogo.
Inakadiriwa kuwa
asilimia 10 ya ardhi ya Tanzania ni ardhioevu ambayo ni muhimu kwa bioanwai,
uchumi, shughuli za kijamii na kiikolojia. Maeneo haya ni makazi muhimu ya aina
mbalimbali za viumbe hai wakiwemo samaki, viboko, mamba, ndege na viumbe
wengine wasio na uti wa mgongo. Katika ikolojia ya ardhioevu tunapata bioanwai
kubwa kuliko eneo lingine lolote duniani. Maeneo haya ni vyanzo vya maji kwa kipindi
chote cha mwaka, huhifadhi maji na kupunguza mafuriko kwa maeneo ambayo ni
hatarishi.
Maeneo haya ni
muhimu kwa kuchuja kemikali zilizopo kwenye maji yaliyochafuka hususani kutoka
kwenye kilimo, viwanda na matumizi ya nyumbani. Madini yanayochujwa kwa
wingi na ardhioevu ni pamoja na madini
ya Nitrojen, Phosphorus na madini ya Aluminium na Chuma. Madini ya Nitrojen na
Phosphorus husababisha kupungua kwa hewa muhimu ya oxygen kwa viumbe wa majini.
Hii hutokana na kumea kwa wingi kwa mimea aina ya mwani (Algae) ambayo ikiota
kwa wingi kwenye uso wa maji husababisha ukijani unaozuia mwanga wa jua kufika
kwenye kina cha maji na kuzuia “photosynthesis” kutokea. Hewa ya “oxygen”
itapungua majini na viumbe maji kama samaki
hufa kwa wingi.
Ardhioevu pia huzuia
mmomonyoko wa udongo kwenye fukwe/kingo za mito na mifereji unaoweza
kusababishwa na mawimbi ya bahari. Ardhioevu pia ni vyanzo vya umeme, na
huchangia huduma ya usafirishaji na ni maeneo mazuri kwa ajili ya kubarizi.
Maeneo ya ardhioevu
yanasimamiwa na mkataba wa “Ramsar” ambayo Tanzania imeweka saini, Sheria ya
Usimamizi wa Wanyamapori na Mazingira yake, na ndio msingi wa usimamizi na
matumizi endelevu ya ardhioevu duniani. Mkataba huu ulisainiwa na nchi
wanachama kwa mara ya kwanza katika mji wa Ramsar nchini Iran mwaka 1972.
Lengo
la kuanzishwa kwa mkataba huu ni
kuhifadhi Ndege maji kwa mfano Korongo Taji, Korongo Nyangumi Bungunusu, Herroe
Mkubwa, Heroe Mdogo. Ndege hawa ni muhimu kwa utalii na uhifadhi wa mazingira
na mwingiliano wa bianuwai. Pia ni dalili ya afya ya mazingira. Tanzania
iliweka saini makubaliano haya mwaka 2000.
Tanzania kuna maeneo
ya Ardhioevu manne ambayo ni; Ziwa
Natron yenye umuhimu wa kuhifadhi ndege aina ya Heroe Wadogo-(Lesser flamingo),
Malagarasi Muyovosi ina umuhimu wa
kuhifadhi ndegemaji aina ya Korongo
Domkiatu (Shoebill Stork), Bonde la Mto Kilombero yenye umuhimu wa uhifadhi wa
Puku na Rufiji mafia Kilwa uhifadhi wa Mikoko na Mazao ya Baharini.
Serikali imeendelea
kuimarisha usimamizi wa ardhioevu nchini. Hata hivyo, ardhioevu nyingi nchini
zinaharibika na zingine kutoweka kutokana na ongezeko la shughuli za
kimaendeleo zisizo endelevu kama vile ujenzi kwenye vyanzo vya maji, ufugaji
holela, kilimo kisichozingatia kanuni za kilimo cha kisasa na kukata miti ovyo.
Athari zingine zinazotokana na matumizi mabaya ya ardhioevu ni pamoja na vifo
vya mimea maji na wanyama wanaotegemea maji kuishi na kunywa kutokana na
matumizi yasiyoendelevu, ukosefu wa mapato kwa jamii kutokana na kuathiriwa kwa
sekta za uvuvi, utalii, kilimo cha umwagiliaji na ufugaji. Binadamu, mimea na
wanyama wakiwemo samaki pia huathirika kwa kukosa maji.
Mamlaka ya Usimamizi
Wanyamapori Tanzania inawakumbusha wananchi kuwa maeneo ya ardhioevu ndio
vyanzo vya maji ambayo binadamu wanatumia kila siku. Mimea na Wanyama pia
hutegemea maji kutoka kwenye ardhioevu. Mamlaka inatoa wito kwa wananchi
wanaoishi karibu na maeneo ya Ardhioevu, kushirikiana na Serikali na Taasisi
zake pamoja na Taasisi zisizo za Kiserikali katika kuyatunza maeneo haya.
Mamlaka
inatoa wito kwa wananchi kutekeleza
sheria mbalimbali za uhifadhi ikiwemo Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya
mwaka 2009, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Sheria nyingine za kisekta
kama ya Maji na Uvuvi na kuwahimiza wale wote wanaoishi kwenye maeneo ya
ardhioevu na hifadhi kuhama bila shuruti.
Martin T.
Loibooki
KAIMU
MKURUGENZI MKUU-TAWA
1 Februari 2017
No comments:
Post a Comment