Monday, February 20, 2017

FAO YATOA KIASI CHA SHILINGI MILIONI 280 KATIKA MCHAKATO WA KUPITIA UPYA SERA YA TAIFA YA MISITU YA MWAKA 1998


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ( kushoto) akiwa na Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) , Fred Kafeero (kulia) wakisaini hati ya makubaliano ya kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa. ( Picha na Lusungu Helela- Maliasili) 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ( kushoto) akiwa na Mwakilishi Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Fred Kafeero (kulia) wakibadilishana hati ya makubaliano ya  kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa. ( Picha na Lusungu Helela- Maliasili)
Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa akionesha kitabu cha Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka ya 1998 ambayo imepitwa na wakati kutokana na mabadailiko mengi kutokea nchini. Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ( kushoto) akiwa na Mwakilishi Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Fred Kafeero (kulia).( Picha na Lusungu Helela- Maliasili)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ( kushoto) akizungumza kabla kutia saini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ya kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa. ( Picha na Lusungu Helela- Maliasili)



Serikali ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) wameisaini makubaliano ya kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi amesema mpango huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 280 ambazo zimetolewa na FAO kwa ajili ya kufanya utafiti wa kuongezea takwimu ambazo zitaboresha Sera ya Misitu ya Taifa ili iweze kufikia hadhi ya kimataifa.

Amesema hatua hiyo imekuja Kutokana na Sera ya Misitu ya Taifa ya mwaka 1998 inayotumika hadi hivi sasa kupitwa na wakati yakiwemo mabadiliko ya Kiuchumi, Kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja na Mabadiliko ya tabia ya nchi.

Maj. Gen. Gaudence ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la ufyekaji misitu na hivyo kumechangia kupunguza uoto wa asili kutoka hekta milioni 55.9 kwa mwaka 1990 hadi kufikia hekta milioni 46 kwa sasa lakini Sera ya Misitu ni ile ile.

‘’ Sera ya Taifa ya Misitu ilishafanyiwa mapitio kuanzia mwaka 2009, Lakini kutokana na Sera hii kukaa kwa muda wa takribani Miaka 9 hadi hivi sasa tumegundua kuwa baadhi ya wadau wengi hawakupata nafasi ya kutoa mawazo yao. Hata wale waliotoa mawazo yao mengi yameshapitwa na wakati.’’ Alisema Maj. Gen. Milanzi

Naye Mwakilishi Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) , Fred Kafeero amesema kuwa Mradi huo utasaidia wananchi wengi kushiriki na kutoa mawazo mengi kuhusiana na Sera ya Misitu ikiwa pamoja na kuwajengea uwezo watumishi kuweza kukusanya taarifa nyingi ili ziwezeshe kuboresha sera kupitia tafiti. 


Aidha,Kafeero amesema kutokana na mabadiliko hayo FAO itasaidia katika kuhuisha sera mpya ambayo itatoa majibu kwa changamoto zinazoikabili nchi hivi sasa na kukidhi mikataba ya kimaifa kama vile mabadiliko ya tabia ya nchi .

No comments: