Thursday, February 23, 2017

DC MTATURU ATOA MWEZI MMOJA WAFANYABIASHARA WA ASALI KANDO YA BARABARA SINGIDA-DODOMA KUHAMIA JENGO JIPYA.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akionyesha moja ya kifungashio bora cha asali katika uzinduzi wa vifungashio hivyo.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akizungumza na wadau wa asali wakiwemo wazalishaji na wafanyabiashara katika uzinduzi wa vifungashio vya asali wilayani humo.
Mkurugenzi wa wilaya ya Ikungi Rustika Turuka akitoa salam kwenye uzinduzi wa vifungashio vya asali uliofanyika katika kijiji cha Issuna wilayani humo.

…………………………………………………………………………..

MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu ametoa mwezi mmoja kuanzia leo kwa wafanyabiashara wote wanaouza asali pembezoni mwa barabara kuu ya Singida-Dodoma kuhamia katika jengo lililojengwa na serikali ili kuongeza thamani na kurahisha upatikanaji wake.


Akizungumza katika uzinduzi wa vifungashio vya asali uliofadhiliwa na wakala wa misitu Tanzania(TFS)leo katika kijiji cha Issuna A wilayani humo Mtaturu amesema serikali iliwekeza kwa makusudi katika jengo hilo ili kuwainua wazalishaji wa asali lakini ni zaidi ya miaka mitatu sasa toka likamilike na halijaanza kutumika.

“Kauli mbiu yetu ni asali bora, maisha bora na hii inaenda sambamba na mikakati ya serikali katika kuboresha maisha ya wananchi na dira ya maendeleo ya Taifa 2025 lakini pia inaunga mkono Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 iliyoahidi kuendeleza program ya ufugaji nyuki ili kuwajengea uwezo wadau,”alisema Mtaturu.

Aliwapongeza TFS kwa juhudi zao katika uhifadhi wa misitu na kutoa mafunzo kwa kamati za mazingira karibu vijiji vyote wilayani humo lakini pia kwa hatua yao ya kuleta vifungashio na kwa wadau kuendelea na ushirikiano waliouonyesha.

Alisema vifungashio hivyo vitatumika kufungashia asali bora ya Ikungi na hivyo kuondokana na vifungashio ambavyo vimezoeleka ambavyo kiafya sio salama huku akiwaasa wazalishaji na wafanyabiashara kuwa pamoja ili kupata fursa mbalimbali na kuboresha uzalishaji wenye tija zaidi kiuchumi.

“Sekta hii ikipewa kipaumbele ikiwemo kutatua changamoto zake inayo nafasi kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uhifadhi wa mazingira ,itapunguza umaskini na kuongeza pato la mwananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuwa soko la bidhaa hii na nta lipo ndani nan je ya nchi,”aliongeza Mtaturu.

Alieleza mpango wa wilaya kuwa ni kusaidia uanzishwaji wa vikundi vya ufugaji nyuki vya wanawake na vijana na kuvijengea uwezo ili hatimaye viongeze uzalishaji na kupelekea kuwa na kiwanda cha kuchakata asali wilayani humo hatua ambayo itasaidia kuongeza thamani ya zao hilo na kumuagiza mkurugenzi wa halamshauri hiyo kuongeza bidii ya uundaji wa vikundi ili kuvijengea uwezo na kufikia malengo mapema.

Mtaturu aliwanunulia vikundi viwili vifungashio 200 vya kuanzia na kuahidi kuwapelekea mizinga 20 kama chachu ya kutumia mizinga ya kisasa ambayo uvunaji mmoja unapata lita 18 kwa mzinga tofauti na ile ya kienyeji inayovunwa kiwango kidogo kisichofikia lita 5 kwa mzinga.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na kaimu meneja wa TFS wilaya Samson Lyimo zinaonyesha kuwa kila mwaka uzalishji wa asali unaongezeka ambapo mwaka 2014/2015 ilikuwa tani 3.6 na 2015/2016 tani 4.617 na kusisitiza kufuatwa kwa kanuni za kuwa na mizinga bora,uvunaji bora na kutumia vifungashio vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ambapo ameeleza changamoto waliyokuwa wanaipata ya kushindwa kuwafikia wafanyabiashara kutokana na kutokuwa na eneo maalum.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo meneja wa TFS kanda ya kati Mathew kiondo aliahidi kuendelea kutoa vifungashio vya kutosha ili asali Ikungi iongezeke ubora kwa kifungashio cha lita moja wachangie shilingi mia 500 na cha nusu lita wachangie shilingi 300 na kueleza lengo lao ni kuwaweka pamoja ili kuwapatia fursa ya mikopo kupitia program ya kopa mzinga lipa asali.

Katika uzinduzi huo alichangia madawati 50 katika kusaidia mkakati wa wilaya uliotangazwa na mkurugenzi wa halamshauri Rustika Turuka wa kumaliza tatizo la madawati uliopewa jina la “changia dawati umnusuru dogo wa Ikungi asikae chini”.

No comments: