Tuesday, January 24, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKUTANA NA WAJUMBE WA BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es salaam Januari 24, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng'i Issa akitoa taarifa ya Baraza hilo katika kikao kati ya Baraza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kilichofanyika kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es salaam Januari 24, 2017 
 Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, John Jingu  akitoa maelezo kuhusu Baraza hilo katika kikao kati ya Baraza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kilichofanyika kwenye Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es salaam Januari 24, 2017.

  Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na watumishi wa Baraza hilo wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza nao kwenye makazi yake , Oysterbay jijini Dar es salaam Januari 24, 2017
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi baada ya kuzungumza nao kwenye makazi yake, Oysterbay  jijini Dar es salaam Januari 24, 2017. 

WAZIRI MKUU amewataka Wajumbe wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) wakutane na wamiliki wa taasisi za kifedha ili kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo yenye gharama nafuu.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Januari 24, 2017) wakati alipokutana na wajumbe wa baraza hilo katika Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema ni vema wajumbe hao wakakutana na wamiliki wa taasisi hizo za kifedha ili kuwasaidia wananchi kupata mikopo yenye masharti nafuu itakayowawezesha kukuza uchumi wao.

“Baraza likutane na wamiliki hao na kuzungumza namna sahihi ya kuwezesha kutoa mikopo ya masharti nafuu. Pia tuangalie taasisi hizo  zinatuasadiaje sisi kama Serikali kuwawezesha Watanzania kupata mikopo ya masharti nafuu,” amesema.

Amesema wananchi wanahitaji kuona ni namna gani Serikali imejipanga kuwawezesha wao kiuchumi, hivyo baraza litoe muelekeo wa namna ya wananchi watakavyoweza kufuga na kulima kitaalam ili waweze kupata tija.

Waziri Mkuu amesema asilimia 80 ya wananchi wanajishughulisha na kilimo kama njia sahihi ya kuboresha uchumi. Pia ufugaji unaweza kusaidia jamii ya wafugaji kupata tija, hivyo baraza liwasaidie kwa kuwapa mbinu sahihi za kuboresha ufugaji wao.

Awali Mwenyekiti wa baraza hilo, Dk. John Jingu  alisema baraza  lilizinduliwa Januari 8, 2017 na walikubaliana kuanza kazi katika maeneo ya kipaumbele yatakayokuwa na tija kwa wananchi ambayo ni kilimo, sanaa, ufugaji na uvuvi.

Alisema wanaamini kuwa uwezeshaji katika maeneo hayo utaleta matokeo ya haraka kwa wananchi wengi kwa kuwa shughuli zao nyingi zimejikita katika maeneo hayo.

Dkt. Jingu alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kutafuta mbinu zitakazoweza kutatua changamoto kubwa zinazowakabili ambazo ni pamoja na ukosefu wa mitaji na  masoko ya uhakika kwa mazao yao.

Alisema moja ya mbinu wanazotarajia kutumia ili kuleta mabadiliko ya haraka na yenye tija ni kuimarisha uhusiano katika sekta bukwa na za kati na vikundi vya wazalishaji wadogo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM

JUMANNE, JANUARI 24, 2017.

No comments: