Imethibitishwa kuwa wanawake wakijengewa uwezo wa kujiamini, wanauwezo wa kushinda katika chaguzi mbalimbali bila kuhitajika hitaji la kutengewa viti maalum, kwa sababu wanawake wana uwezo sawa na wanaume na hata kuwapita.
Uthibitisho huo, umethibitishwa katika uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mt. Kibo iliyopo Mbezi Juu jijini Dar es Salaam, ambayo ni shule mchanyiko wa wavulana na wasichana, lakini katika uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi wa shule hiyo, nafasi zote za uongozi wa juu, zimeshikwa na wanafunzi wa kike ambao wamewapita wanafunzi wa kiume.
Ushindi huo umewezekana baada ya uongozi wa shule hiyo, kuamua kufundisha somo la demokrasia kwa vitendo, katika azma ya shule hiyo kutekeleza hoja ya “samaki mkunje angali mbichi” kwa kuwafundisha demokrasia kwa vitendo, wanafunzi wa shule hiyo tangu wangali wadogo.
Mwalimu wa shule hiyo, Sebastian Ngimba, amesema, lengo la mafunzo hayo ya demokrasia kwa vitendo, ni kuwafunza wanafunzi hao jinsi demokrasia inavyofanya kazi, tangu wakiwa wadogo, ili watakapo kuwa watu wazima na kuingia kwenye siasa, wawe wamepata msingi imara wa demokrasia tangu wangali wadogo.
Mafunzo hayo yamefanywa kupitia uchaguzi wa viongozi wa wanafunzi, ambapo iliundwa kamati ya uchaguzi chini ya mwenyekiti wa uchaguzi, wagombea wote wakajaza fomu za kuomba kuchaguliwa, wakapitishwa, wakapiga kampeni za wazi, kisha uchaguzi ukafanyika kwa kaatasi za kura zilizochapishwa na kupigwa kwa kura za siri kupitia masanduku ya kura yanaoonyesha (trasmpaent), kura zikahesabiwa, na matokeo yakatangazwa na washindi kuapishwa kushika uongozi.
Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi wa shule hiyo Aristides Peter Mugisha amesema wameendesha uchaguzi wao wa viongozi wa shule kwa kufuata taratibu kama za NEC katika kuendesha uchaguzi.Makamo Mwenyekiti wa kamati hiyo Arieth Albert amesema wameendesha uchaguzi kidemokasia na walioshinda wameshinda kihalali.
Katika uchaguzi huo, nafasi zote tatu za juu za viongozi wa serikali ya wanafunzi wa shule hiyo, zimeshikwa na wasichana ambao wamewashinda wavulana, katika hali inayoonyesha, watoto wa kike, wakijengewa uwezo wa kujiamini tangu wakiwa shuleni, wanauwezo wa kushindana na wanaume na kushinda, katika hali itakoyopelekea kutohitajika tena kwa nafasi za viti maalum vya wanawake kwa sababu, imethibitishwa wanawake wanauwezo sawa na wanaume na hata kuwashinda.
Viongozi hao wapya ambao ni Dada Mkuu Nancy Mary Mtinga, na Dada Mkuu Msaidizi Angel Jacob, wamesema wamefunzwa kujiamini kuwa wanawake wanaweza, na wamegombea na wanafunzi wa kiume, wamepiga kampeni na wamewashinda vibaya wagombea wa kiume.
Mwalimu Prosper Shimili amesema wanafunzi wa kike sio tuu wanauwezo wa kushinda chaguzi, hata darasani, kuna wanafunzi wengi wa kike wanafanya vizuri kuliko wanafunzi wa kiume.
Mwalimu Doreen Msangi, amesema ili juhudi hizi za kuwajengea wanawake kujiamini, lazima wazazi, familia na jamii, ziwape fursa sawa watoto wa kike na wa kiume, sio kuwaambia kazi Fulani ni za kike na nyingine ni za kiume.
Sensa ya watu na makazi imethibitisha idadi ya wanawake ni wengi kuliko wanaume, hivyo kama wapigakura wanawake tuu wangewachagua wagombea wanawake, hakuna wagombea wanaume wangeshinda chaguzi.
No comments:
Post a Comment