Monday, January 9, 2017

WANAWAKE MKO WAPI UCHAGUZI MDOGO?


 Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.


Hivi karibuni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kufanya uchaguzi mdogo wa Ubunge pamoja na Udiwani kwa sehemu mbalimbali nchini ambazo viongozi wake wamefariki au wamepoteza sifa za kuendelea kuongoza wananchi katika sehemu husika.

Uchaguzi huo unategemewa kufanyika Januari 22 mwaka 2017 katika Jimbo la Dimani lililopo Zanzibar pamoja na Kata 20 ambazo zipo kwenye Halmashauri 19 za Tanzania Bara.

Mnamo Desemba 2016, NEC ilifanya uteuzi wa wagombea watakaogombea katika uchaguzi huo ambapo walioteuliwa kugombea Ubunge katika Jimbo la Dimani ni 11 ambao wote ni wanaume na kwa upande wa wagombea udiwani katika Kata mbalimbali za Tanzania Bara ni 71 ambapo wanaume ni 67 na wanawake ni watano.

Kwa kuangalia takwimu hizi chache tu zinatosha kutupatia majibu kuwa katika uchaguzi huu wanawake hawajajitokeza kabisa kugombea nafasi hizo wakati asilimia kubwa ya wanawake nchini wana sifa za kugombea nafasi hizo. Kwa uchaguzi huu wanawake wamewaangusha Watanzania wengi ambao wana amini kuwa wanawake wakipewa nafasi wanaweza kuzitendea haki.

Kumekuwa na wadau wengi duniani wanaotetea haki za wanawake kila kukicha kuhakikisha wanawake wanakuwa na haki sawa na wanaume kwenye nyanja mbalimbali zikiwemo za uongozi, kazi pamoja na elimu.

Pamoja na utetezi huo kushika kasi hadi kufanya jamii nzima kuamini kuwa wanawake wanaweza lakini bado wanawake wengi wanajirudisha nyuma kwa kutojiamini kama wanaweza kushika nyazfa mbalimbali za uongozi nchini.

Haina ubishi kuwa wanawake waliopata bahati za kuchaguliwa kuwaongoza wananchi katika sehemu mbalimbali wanafanya kazi nzuri katika kuhakikisha wananchi wao wanapata haki zao na kuishi maisha bora.

Kwa sababu uongozi ni kitu endelevu, nawashauri wanawake kutumia fursa ya sasa kujipanga vyema ili kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao hivyo kuweza kuwaongoza wananchi na kufanya mageuzi makubwa yatakayoleta tija kwa nchi na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye maendeleo.

Pia wanawake kutofikiria kushiriki nafasi za kuteuliwa peke yake badala yake wanatakiwa wawe mstari wa mbele kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwasemea wanawake wenzao katika nyanja mbalimbali kama vile Bungeni na katika Mikutano ya Kimataifa.

Wanawake wanamatatizo mengi ambayo yanahitaji kusemwa ili yaweze kutatuliwa. Matatizo hayo yametokana na mila na desturi ambazo zimekuwepo tangu enzi za mababu, ambazo ni ukeketaji kwa watoto wa kike, ndoa za utotoni, ukatili kwa wanawake, ubaguzi wa elimu kwa watoto wa kike na matatizo mengine mengi.

Matatizo hayo yote hayawezi kutatuliwa bila ushiriki wa wanawake katika nyazfa mbalimbali ambao watatumika kama daraja katika kuwakilisha matatizo yao hivyo kuwakomboa wanawake wenzao ambao bado wana mila na desturi za kizamani ambazo ni kandamizi kwa maendeleo yao. 

No comments: