Thursday, January 12, 2017

Walimu Karatu kurejeshewe Fedha za Vitambulisho vya Kazi – RC Gambo

 Na Nteghenjwa Hoseah, Karatu 
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo kuhakikisha fedha za walimu wa shule za sekondari na msingi zilizokatwa na halmashauri ya wilaya hiyo kwaajili ya vitambulisho vya kazi zinarudishwa. 
 Mhe. Gambo alitoa agizo hilo jana wilayani Karatu wakati alipokuwa akizungumza na walimu hao kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Karatu Boys ili kujua changamoto wanazokutana nazo na jinsi ya kuzitatua ikiwemo madeni ya likizo, upandaji wa madaraja. 
 Alihoji ni kwanini walimu hao wakatwe Sh. 6000 kwa ajili ya kutengenezewa vitambulisho vya kazi wakati ni haki yao kama watumishi na waajiriwa wa halmashauri hiyo na ni haki yao kupata vitambulisho vya kazi bure; Mwajiri anao wajibu wa kumtengenezea kila mtumishi Kitambulisho cha kazi. 
 Alimwagiza DC Mahongo kuhakikisha anafuatilia na kumchukulia hatua watumishi wa halmashauri hiyo waliowakata walimu hao wa msingi na sekondari kiasi hicho cha fedha kwa ajili kuwachukulia hatua. 
 "Eti vitambulisho vyenu mmetozwa hela kwa sababu gani wakati ni bure... Sasa nasema aliyehusika na kuwatoza Sh, 6000 kwa ajili ya vitambulisho vyenu vya kazi atachukuliwa hatua kwa nini muwafanye walimu kama shamba la bibi? Hamuwaonei huruma jamani? Wanadai malipo yao na hata vitambulisho vya kazi pia muwakate hela zao hii siikubali"
Pia Mhe. Gambo aliwaondoa hofu walimu hao kuwa serikali ya mkoa wa Arusha itahakikisha kuwa madeni yote yanayodaiwa na walimu hao yatashughulikiwa ili waweze kufundisha vyema wanafunzi wao.
 Awali walimu hao baadhi walisema wengine wanatembea umbali mrefu kwa ajili ya kutoa elimu huku wanafunzi nao kwenye baadhi ya shule wakishindwa kuhudhuria masomo yao kwa wakati sababu njiani wanakutana na wanyamapori.
Pia Mwalimu Joachim Petro akisema awali alisimamishwa kazi kwa mizengwe na baadaye kurudishwa kazini na kuamriwa kupewa Shilingi milioni 3. 5 kama madai ya usumbufu na mshahara yake lakini tangu mwaka juzi hajapewa fedha zake 
 Pia fedha za walimu za SACCOS zaidi ya Sh. milioni 11.3 za walimu ambazo ni makato yao hawazioni na hata wakitaka kuzikopa wanaelezwa hazipo sasa zimekwenda wapi. 
 Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Mahongo alisema anafuatilia suala hilo ili kujua ni mtumishi gani wa halmashauri alichukua fedha hizo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Bw. Waziri Morice ili kuchukua hatua kali za kinidhamu.

No comments: