Friday, January 6, 2017

Wakuu wa wilaya za Arusha wabebeshwa mzigo mzito.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(kwanza kulia) akizungumza katika kikao cha maandalizi ya Bajeti 2017/2017 na mapitio ya Bajeti 2015/2016.
Na Nteghenjwa Hossea, Arusha
Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Arusha wameagizwa kusimamia Halmashauri zao kujibu hoja zote zilizowasilishwa na  Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa  Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 kabla ya kufika mwisho wa juma lijalo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo  wakati wa Kikao  cha maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2017/2018 na mapitio ya bajeti ya nusu mwaka wa Fedha 2016/2017 kilichohusisha Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha  na wataalam toka Ofisi ya Mkaguzi wa hesabu za Serikali.
Akitoa Agizo hilo Mhe. Gambo alisema “Nataka kila Halmashauri ikamilishe ujibuji wa Hoja kwa wakati na kwa majibu sahihi sio kufanya majibu ambayo yanaibua hoja zaidi au hayajitoshelezi na kwa Halmashauri ambayo ilipata Hati Chafu au Hati ya Mashaka kwa mwaka uliopita ianishe wataalamu waliopelekea Halmashauri kupata Hati hizo ili waweze kuchukuliwa hatua Stahiki”.
Wakuu wa Wilaya mshiriki Kikamilifu kuhakikisha hoja zinajibiwa ipasavyo na wale waliosababisha hoja hizo kwa kipindi cha nyuma wanachukuliwa hatua ili kuleta nidhamu ili kuongeza umakini katika zoezi zima la ujibuji wa Hoja alisema Gambo.
Aliongeza kuwa “Sitamueleza Mkuu wa Wilaya ambaye Halmashauri yake itapata Hati Chafu au ya Mashaka kwa hesabu za mwaka ulioisha, Mkasimamie Halmashauri zenu kwa nguvu zenu zote na katika hili sitamuonea mtu haya”.
Katika mapitio ya Bajeti ya inayoendelea alizitaka Halmashauri ambazo hazijatoa asilimia kumi ya mapato yao kama mikopo kwa vikundi vya wananwake na vijana zikatoe Fedha hizo kabla ya mwisho wa Januari ili kuweza kuinua uchumi wa makundi haya yaliyoainishwa kwa mujibu wa Sera na Maelekezo.
“Katika hili napenda kuwapongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kukamilisha utoaji wa mikopo  zaidi ya Mil 600 kwa robo ya kwanza naya Pili kwa mwaka wa Fedha 2016/2017 lakini halmashauri zingine zote hazijakamilisha utoaji wa Mikopo inayotakiwa kwa kipindi cha nusu mwaka.”
Awali katika Kikao hicho akiwasilisha mapitio ya Bajeti 2015/2016 na Mpango wa Bajeti 2016/2017 Katibu Tawala Msaidizi huduma za Mipango Bi. Grace Mbaruku alisema Halmashauri zote zinatakiwa kuandaa Bajeti Mpya kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa katika muongozo wa Bajeti.
 Halmashauri haitazingatia vigezo vilivyowekwa inaweza kupelekea bajeti yao kukwama katika ngazi za juu hivyo zingatieni vigezo kama kutenga Fedha za Lishe kwa ajili ya kutokomeza udumavu kwa Watoto alisema Bi. Mbaruku.
Akiwasilisha Taarifa ya Changamoto zinaowakabili katika Usimamizi wa Halmashauri Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Serikali za Mitaa Bi. Susane Mnafe aliainisha ucheleweshaji wa uwasilishaji wa Taarifa toka Halmashauri mara zinapohitajika, kutofuata mfumo elekezi wa uwasilishaji wa Taarifa.
Aliongeza kuwa kutokua na kanzidata ya vyanzo vya mapato na uandaaji wa Bajeti ya Halmashauri kabla ya Sheria ndogo mpya kupitishwa huchangia kukwamisha ukusanyaji wa mapato kwa kutumia viwango vipya.



No comments: