Timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango ikiongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Bibi Florence Mwanri imefanya ziara katika Kiwanda cha Tanga Cement kilichopo Mkoani hapa kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho.
Katika ziara hiyo, Bibi Mwanri alipata fursa ya kukagua maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na eneo linalotumika kuchimba malighafi za kutengenezea saruji, teknolojia ya kisasa inayotumika kuendesha mashine kiwandani hapo pamoja na kuangalia hatua mbalimbali zinazotumika katika uzalishaji wa saruji.
Akiwa katika eneo linalochimbwa mawe ya kutengenezea saruji, Mwanri alieleza kuwa kiwanda hicho kina wajibu wa kuhakikisha sheria na taratibu za utunzaji wa mazingira zinazingatiwa muda wote ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama licha ya shughuli za uchimbaji kuendelea kufanyika.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akiuliza namna mifumo ya komputa ya kiwanda hicho inavyoendesha shughuli za uzalishaji wa saruji katika kiwanda cha Tanga Cement.
Mwanri alipongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake katika kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuwa nchi ya Viwanda na kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo inayosisitiza kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Naye Meneja wa Kiwanda hicho, Mhandisi Ben Lema alisema kuwa kiwanda hicho kimeendelea kutoa ajira kwa watanzania katika kada mbalimbali ambapo kwa sasa kua ajira zaidi ya 600 ambapo ajira 300 ni za moja kwa moja huku ajiara 300 zingine ambazo sio za moja kwa moja zinajumuisha wauzaji, wasambazaji, wasafirishaji na wengine walioko katika mnyororo huo.
Meneja wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Ben Lema akionesha aina za malighafi na aina mbalimbali za saruji zinazozalishwa na kiwanda hicho.
Aliongeza kuwa bidhaa za kiwanda hicho bado zinafanya vizuri sokoni licha ya ushindani uliopo kufuatia kuanzishwa kwa viwanda vingi vinavyozalisha saruji kwa kuwa mahitaji ya saruji bado ni mwakubwa sokoni.
Lema alieleza kuwa viwanda vya saruji vinapata faraja kubwa kwa kuwa miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali na hata inayotekelezwa na sekta binafsi inatumia saruji inayotengenezwa na viwanda vya ndani.
Meneja wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Ben Lema (mwenye Miwani) akimwonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (mwenye koti jenkundu) eneo (halipo pichani) linalochimbwa na kiwanda hicho kwa zaidi ya miaka 30 kwa ajili ya kupata malighafi zinazotumika katika kutengeneza saruji kiwandani hapo. Wengine ni Maofisa wa Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo walioambatana na Kaimu Katibu Mtendaji katika ziara hiyo.
Eneo linalochimbwa kwa zaidi ya miaka 30 kwa ajili ya kupata mawe yanayotumika kutengenezea saruji. Baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji, Kiwanda cha Tanga Cement kitafanya eneo hilo kuwa sehem ya utalii kwa kutengeneza bwawa na kufuga wanyama mbalimbali.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akikagua mifumo ya kisasa inayotumika kuendesha shughuli mbalimbali katika kiwanda cha Tanga Cement.
Baadhi ya mitambo inayoendelea kufanya kazi katika kiwanda cha Tanga Cement.
PICHA ZOTE NA ADILI MHINA, TUME YA MIPANGO
No comments:
Post a Comment