Saturday, January 21, 2017

Taarifa ya ujio wa ziara ya Rais wa Uturuki nchini

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI


 

 Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Uturuki nchini.

Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Mheshimiwa Recep Tayyip Erdogan anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 22 na 23 Januari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Mhe. Rais Erdogan ambaye ataambatana na Mkewe, na kuongoza ujumbe wa watu 150 wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Maafisa kutoka Serikalini na Wafanyabiashara anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 22 Januari, 2017 jioni  na atapokelewa na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uturuki na Tanzania pamoja ‎na kupanua fursa za uwekezaji hususan katika maeneo ya biashara  na uwekezaji.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Erdogan  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili na baadaye Marais hao watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali. 

Siku hiyo ya tarehe 23 Januari, 2017, kutakuwa na Kongamano la Biashara kati ya Uturuki na Tanzania litakalowakutanisha Wafanyabiashara kutoka nchi hizi mbili. Kongamano hilolitahutubiwa na viongozi wa Tanzania na Uturuki.
Mhe. Rais Erdogan na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Mahusiano ya Uturuki na Tanzania
Mahusiano ya Tanzania na Uturuki ni mazuri. Ikumbukwe kuwa, kufunguliwa kwa mara nyingine kwa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini mnamo Mei 2009 kuliongeza kasi ya mahusiano baina ya nchi hizi mbili.  Tangu kipindi hicho kumekuwa na ziara za viongozi wa kitaifa wa nchi hizi mbili ili kukuza na kudumisha mahusiano. Katika hatua nyingine Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi wake nchini Uturuki na hivi leo Mhe. Rais atamwapisha Balozi Mteule, Prof. Elizabeth Kiondo atakayetuwakilisha Uturuki.
Pia kumekuwa na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais mstaafu wa Uturuki, Mhe. Abdullah Gul  nchini mwaka 2009 ; ziara ya Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Uturuki mwaka 2010 na ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein mwaka 2011.
Tume ya Pamoja ya Biashara
Tanzania na Uturuki zinashirikiana pia kupitia Tume ya Pamoja ya Biashara ambayo ilianzishwa baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Ushirikiano kwenye masuala ya Biashara mwaka 2010. Kikao cha kwanza cha Tume hiyo kilifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2012. Katika kikao hicho pande zote zilikubaliana kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali hususan biashara na uwekezaji, elimu, Kilimo, Nishati na Madini, Maendeleo ya viwanda na mawasiliano ya simu.

Kikao cha Pili cha Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Uturuki kilifanyika tarehe 11 – 12 Januari 2017, Uturuki kwa lengo la kujadili utekelezaji wa Makubaliano ya Kikao cha Kwanza na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya pande hizi mbili. Aidha, Mkutano huu pia ulikuwa na umuhimu wa kipekee kwa kuwa ulifanyika ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Kiserikali ya Mheshimiwa Recep Tayyip Erdoğan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Januari, 2017.

Pande zote mbili zimekubaliana kuongeza nguvu katika kuhamasisha uwekezaji kwenye nchi zetu. Katika kutekeleza hili, Uturuki imepanga kuandaa Mkutano wa Uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki ndani ya robo ya pili ya mwaka huu jijini Istanbul. Vile vile, nchi zote mbili zimekubaliana kubadilishana taarifa za fursa za uwekezaji kupitia Balozi zetu na Baraza la Biashara la Tanzania na Uturuki. Aidha, Taasisi zetu za Uwekezaji zimeelekezwa kuanza majadiliano ya kuingia Mkataba wa Ushirikiano ili kuhamasisha uwekezaji nchini. Hali kadhalika, Uturuki imemchagua Mwambata wa Biashara katika Ubalozi wao wa Dar es Salaam na Tanzania imeahidi kuteua Afisa Maalum ndani ya mwezi mmoja kushughulikia uhamasishaji wa uwekezaji na biashara kati ya nchi hizi mbili.

Mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki
Tangu kuanzishwa kwa Tume ya pamoja ya ushirikiano ya kiuchumi mafanikio ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yameonekana ikiwemo:- Kuimarishwa kwa ushirikiano katika masuala ya Usafiri wa Anga ambapo Shirika la Ndege la Uturuki lilianzisha safari tatu  za moja kwa moja kutoka Istanbul hadi Dar es Salaam, Kilimanjaro na hivi karibuni Zanzibar. Kuanzishwa kwa safari hizi kumekuza biashara kati ya Uturuki na Tanzania  ambapo mwaka 2009  ukubwa wa biashara ulikuwa Dola za Marekani milioni 66 sawa na shilingi bilioni 145.2 lakini hadi kufikia Februari 2016 biashara kati  ya nchi hizi mbili iliongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 160 sawa na shilingi bilioni 352. 

Aidha, kuzinduliwa kwa Baraza la Biashara kati ya Tanzania na Uturuki mwaka 2013 ambalo kumewezesha kuimarisha ushirikiano wa sekta binafsi za nchi hizi mbili na  Kuongezeka kwa Makampuni ya Uturuki yaliyowekeza nchini ambapo hadi sasa ni Kampuni 30 zimefanya uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 305.08 na zinatarajiwa kutengeneza ajira 2,959.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
20 Januari, 2017
No comments: