Serikali imesema
imeunda Tume ya uchunguzi ya watu 12 ili kuweza kuchunguza na kubaini chanzo
cha ajali ya moto iliyotokea jana saa Tano usiku katika chumba kidogo cha
kuhifadhia mizigo kilichopo kwenye jengo la Pili la abiria (Terminal II) katika
uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Tume hiyo iliyoundwa inaongozwa na Joseph Nyahende ambae anatoka katika ofisi
za Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege nchini.
“Ninategemea kupata ripoti
ya kitaalamu kutoka kwa Tume hii, ili kutusaidia kubaini kiundani juu ya chanzo
haswa kilichopelekea moto huu”, amesema Waziri Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa
amefafanua kuwa huduma katika jengo hilo
zinaendelea kama kawaida ambapo awali zilisitishwa na kuhamishiwa katika
Jengo la Kwanza la abiria (Terminal I).
“Mara baada ya moto
kutokea, kitu cha kwanza kilichofanyika ni kuudhibiti moto huu ili usiweze
kusambaa katika maeneo ambayo hayajaathirika, kisha tukatafuta njia za
kurudisha huduma kwa abairia”, amesisitiza Profesa Mbarawa.
Katika hatua nyingine,
Profesa Mbarawa ameipa miezi miwili
kampuni ya mizigo ya Swissport kurekebisha huduma zinazolalamikiwa na
wateja wake na endapo itashindwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa JNIA, Paul Rwegasha ameeleza kuwa tathmini na
gharama za mizigo iliyokuwa imehifadhiwa katika chumba hicho bado haijajukana,
ambapo ripoti itaeleza gharama hizo pindi itakapokamilisha uchunguzi wake.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment