Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akikagua
moja ya shamba la mahindi lililoharibiwa na tembo katika kijiji cha
Kunzugu, wilaya ya Bunda Mkoani Mara jana wakati wa ziara yake ya
kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa
Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili.
Naibu
Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza
na wananchi wa kijiji cha Kunzugu, wilaya ya Bunda, mkoani Mara jana
alipotembelea moja ya shamba la mahindi lilioharibiwa na tembo wakati wa
ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia ni
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili.
NA HAMZA TEMBA - WMU
.......................................................
Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema italipa madeni yote ya
miaka ya nyuma ya vifuta jasho na vifuta machozi ambayo inadaiwa na
wananchi waliokubwa na vitendo vya uharibifu wa wanyamapori nchini kabla
ya bunge lijalo la bajeti, madeni hayo ni yale ambayo
yameshaifikia wizara hiyo na kuhakikiwa.
Akizungumza
jana na uongozi wa wilaya ya Bunda wakati wa kuhitimisha ziara yake ya
siku moja ya kufuatilia changamoto za uhifadhi wilayani humo, Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani amesema uamuzi huo wa
Serikali utaondoa kilio cha muda mrefu cha wananchi ambao wamepata
madhara mbalimbali ya wanyamapori ikiwemo vifo, majeruhi, kuliwa mazao
na kuharibiwa mashamba yao.
"Serikali
ya awamu ya tano imeshakamilisha takwimu za madai, yale yote
tunayodaiwa huko nyuma, yaliyoifikia Wizara yakafanyiwa uhakiki na
nimesema kwenye uhakiki huo ndani ya kipindi cha miaka kumi, kwa wilaya
zaidi kidogo ya 80 ambazo ndizo zina changamoto hizi kwa kiwango kikuu,
deni jumla ni shilingi 2,081,532,700 (bil. 2.9)", amesema.
Amesema
wilaya ambazo zimeathirika zaidi na vitendo hivyo na ambazo madai yao
ni makubwa zaidi ya Wilaya zingine ni Serengeti na Bunda ambazo ziko
mkoani Mara na zinapakana na Hifadhi ya taifa ya Serengeti, Ziwa
Victoria, Pori la Akiba Grumeti na Ikorongo. "Serengeti ndiyo
inayoongooza kwa madai hayo, shilingi milioni 408,547,600 alafu Bunda
shilingi milioni 265,969,750",.
Pamoja
na Serikali kujiwekea utaratibu huo na wananchi wa kulipa vifuta jasho
na vifuta machozi kwa waathirika, amesema ipo haja ya kutafuta njia
endelevu ya kukabiliana na changamoto hizo na fedha ambayo ingetumika
kulipia fidia hizo ikatumika kuwezesha mpango huo endelevu. Amesema
mpango huo utawezekana kwa kuwashirikisha wananchi.
"Mpango
endelevu wa kukabiliana na changamoto hiyo ni ule wa ushiriki wa pamoja
wa Serikali na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uharibifu
dhidi ya wanyamapori", amesema.
Ili
kufanikisha mpango huo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Bunda na
Serengeti kuratibu ushiriki wa wananchi wao katika zoezi hilo kwa kuunda
vikundi shirikishi katika kila kijiji, kubaini mahitaji yake ikiwemo
vifaa na kuwasilisha taarifa hiyo wizarani kabla ya tarehe 15 januari
mwaka huu, kwa ajili ya hatua zaidi za kufanikisha mpango huo.
Amesema
ushirikiano huo pekee hautoshi kukabiliana na changamoto hizo kama
wananchi nao hawataipunguzia mzigo serikali wa kupambana na vitendo vyao
viovu dhidi ya uhifadhi, ili nguvu hiyo itumike katika kushirikiana nao
kwenye ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu. "Wananchi waache vitendo
viovu dhidi ya uhifadhi, ujangili, kuua wanyamapori",.
Ameeleza
kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa changamoto hizo ni matokeo
ya tabia za wananchi kusogelea maeneo ya hifadhi kwa ajili ya shughuli
za kibinadamu, jambo ambalo lina athari kubwa katika uhifadhi na usalama
wa wananchi wenyewe, hivyo ni lazima liepukwe.
"Njia
ambayo tembo alikua akipita miaka 20, 30, 40 ndo anapita kila siku,
sisi tumeenda kujenga, tumeenda kulima mashamba, sasa tembo wao na
wenyewe wana ownership (umiliki), ile njia wao wanaona ni ya kwao tu,
kwahiyo akikutana na wewe anafanya hayo anayoyafanya, hata kwenda kukaa
kufanya shughuli za kibinaadamu ikiwemo kujenga na kulima jirani kabisa
na kwenye mpaka ya hifadhi na yenyewe ni tatizo".
Naibu
Waziri Makani amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mara jana
ambapo alitembelea vijiji kadhaa wilayani Bunda na Serengeti na kushudia
athari mbalimbali za uharibifu wa wanyamapori pamoja na kupokea
malalamiko mbalimbali ya uharibifu huo kutoka kwa wananchi. Alishuhudia
mashamba kadhaa ya mahindi yaliyokuwa karibu na maeneo ya hifadhi yakiwa
yameharibiwa na tembo.
No comments:
Post a Comment