Friday, January 20, 2017

SACCOS YA POLISI YAJIVUNIA MAFANIKIO YA MIAKA KUMI

 Mwenyekiti wa bodi ya chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD) Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias E.M. Andengenye (aliyesimama) akitoa neno mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa  nane (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mkoani morogoro jana kulia ni Kaimu Mrajis wa vyama vya Ushirika nchini Bwana Tito Haule, anayefuata ni Makamu Mwenyekiti Kamishna Albert M. Nyamhanga na Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, (ACP) Leonce Rwegasila.
 Wajumbe wa mkutano mkuu wa nane wa chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD), wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wa mkutano huo Kaimu Mrajis wa vyama vya ushirika nchini Bwana Tito Haule, (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika jana mkoani Morogoro.
Kaimu Mrajis wa vyama vya ushirika nchini Bwana Tito Haule, pamoja na viongozi wa bodi na wajumbe wa chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa nane uliofanyika jana mkoani morogoro. (Picha zote na Demetrius Njimbwi – Jeshi la Polisi)

Na Demetrius Njimbwi – Jeshi la Polisi Morogoro
Chama cha ushirika cha kuweka akiba na kukopa cha Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD), kimeendelea kujizolea mafanikio makubwa kwa muda wa miaka kumi toka kuanzishwa kwake huku kikijivunia kukopesha wanachama wake jumla ya fedha taslimu bilioni 113.7

Hayo yamethibitishwa na kaimu Mrajis wa vyama vya ushirika nchini Bwana Tito Haule, wakatia akifungua mkutano mkuu wa nane wa Usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD), uliofanyika jana mkoani Morogoro huku ukiwakutanisha wajumbe na wawakilishi 172 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Bwana Haule, alisema kuwa,  mbali na mafanikio makubwa kupatikana pamoja na ongezeko la akiba na amana zenye thamani ya bilioni 23.095  kutokana na ubunifu wa kujenga mtaji wa ndani pia amewaasa viongozi na watendaji kuwa waadilifu na waaminifu ili kufikia malengo makuu yaliyotokana na maadhimio ya vikao vilivyopita.

Aidha, kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usalama wa Raia Saccos Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji (CGF) Thobias E.M. Andengenye, alisema kuwa, usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD),  itaendelea kutoa elimu kwa wanachama wake wote na kuendelea kujenga mtaji wa ndani kwa kununua hisa na kuweka akiba pamoja na kurejesha mkopo kwa wakati alisema.

Kamishna Andengenye, ameongeza kuwa, usalama wa Raia Saccos (URA SACCOS LTD),  itaendelea kuwahudumia wanachama wake wote ili kuwapunguzia makali ya maisha na kuwaepusha na mikopo yenye riba na masharti makubwa ili kukuza ustawi na uchumi wao na kwamba wamejipanga katika kuongeza idadi ya wanachama kupitia fursa walizonazo.

No comments: