Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) katika mahafali ya 32 ya Chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Katikati ni Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho na pembeni yake ni Mkuu wa Chuo hicho Prof. Zacharia Mganilwa
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Prof. Blasius Nyichomba (kulia), akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika mahafali ya 32 ya Chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akihutubia kongamano la mahafali ya 32 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahitimu wa fani za Shahada ya Uzamili, Stashahada ya Uzamili, Shahada na Diploma katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akihutubia kongamano la mahafali ya 32 ya Chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwatunuku wahitimu wa fani za Shahada ya Uzamili, Stashahada ya Uzamili, Shahada na Diploma katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
Serikali imekitaka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kuboresha mitaala yake ili kuendana na mageuzi makubwa yanayofanywa katika sekta ya uchukuzi hapa nchini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hayo leo katika mahafali ya 32 ya Chuo hicho na kusisitiza kuwa Serikali itatoa nyenzo zote stahiki kwa chuo hicho ili kukiwezesha kutoa wanafunzi watakaokuwa na soko ndani na nje ya nchi.
“Tumeanza kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Uchukuzi ambapo tayari tumenunua ndege katika mkakati wa kuboresha usafiri wa anga na hivi karibuni tutaanza ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge), itakayowezesha treni ya kisasa naya mwendo kasi kutoa huduma kwa kuanzia Dar es salaam hadi Morogoro”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amesema reli ya kisasa itakuwa inatumia umeme ili kuwa na mwendo kasi wa kilomita 160 kwa saa na hivyo kuwezesha usafiri wa Dar es Salaam-Morogoro kuwa wa chini ya muda wa saa mbili.Amesisitiza awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo utaanza hivi karibuni mara baada ya taratibu za kumpata mzabuni wa ujenzi huo kukamilika.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha ujao, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukarabati ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho ili kukiwezesha kuwa cha kisasa na kitakachotoa elimu bora katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na kuhakikisha wahitimu wa fani ya ‘Logistics na Transport Management’ wanapata bodi ya kitaaluma ili kuratibu fani hiyo .
“Hakikisheni mnaimarisha utawala bora, utafiti, ushauri wa kitaalamu, machapisho na huduma yenu iwe ya viwango vya ubora ili kuwezesha wahitimu wenu kupata soko pindi wanapohitimu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amewataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kwa juhudi, bidii na maarifa ili kuleta manufaa kwao binafsi na Taifa kwa ujumla.Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Blasius Nyichomba amewataka wahitimu kuendela kujifunza wawapo sehemu za kazi ili wawe watendaji bora na kujiepusha na majanga ya utumiaji wa madawa ya kulevya, ulevi na ukimwi ambavyo vina athiri wataalamu wengi hapa nchini.
Ameongeza kuwa Chuo hicho kina mpango wa kuanzisha mfumo wa uatamiaji wanafunzi ili kuwawesha wahitimu kupata ajira mara wamalizapo masomo yao.Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Zacharia Mganilwa amesema idadi ya Wanafunzi katika chuo hicho imeongeza kutoka 3500 mwaka 2014/15 hadi kufikia 5340 mwaka huu na wahadhiri wameongezeka kutoka 63 mwaka 2012 hadi 167 mwaka 2017.
Zaidi ya wanafunzi 1,029 wamehitimu Shahada ya Uzamili, Stashahada ya Uzamili, Shahada na Diploma katika fani mbalimbali za usafirishaji na menejimenti zitolewazo katika Chuo hicho.
No comments:
Post a Comment