Naibu
Waziri ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI)
Seleman Jafo wa kati kati akiwa katika boti maeneo ya nyamisati mto
Rufiji kwa ajili ya kujiandaa na safari ya kwenda kuwatembelea wananchi
wa Wilaya ya Rufiji hususan wale wanaoishi katika maeneo ya Delta ikiwa
ni ziara yake ya kikazi Mkoani Pwani ya kukagua miradi mbali mbali ya
maendeleo(PICHA NA VICTOR MASANGU)
Naibu
Wazari Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI)
Seleman Jafo wa kati kati akiwa kwenye boti katika ziara yake ya kikazi
katika Wilaya ya Kibiti na viongozi wengine wa serikali,na wa kwanza
kulia kwake ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Khatibu
Chaurembo kwa ajili ya safari ya kwenda kuwatembelea wananchi wa maeneo
ya Delta kwa ajili ya kukagua miradi ya mbali mbali maendeleo.(PICHA NA
VICTOR MASANGU)
NA VICTOR MASANGU, KIBITI
LICHA
ya serikali ya awamu ya tano kuongeza juhudi za kuboresha sekta ya afya
katika maeneo mbali mbali hapa nchini bado sehemu nyingine utoaji wa
huduma hali bado ni tete kutokana na kukabiliwa na changamoto mbali
mbali ikiwemo ukosefu wa wauguzi,madaktari, madawa, magari ya kubebea
wagonjwa,vitanda pamoja na vifaa tiba hivyo kusababisha wagonjwa kupata
shida kubwa pindi wanapokwenda kupatiwa matibabu.
Changamoto
hizo ambazo zinadaiwa ni sugu na hazijafanyiwa utekelezaji wowote
zimeweza kubainika baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani
Japo kufanya ziara yake ya kikaz ya siku mbili kwa wananchi wa Wilaya
ya Kibiti Mkoa wa Pwani hususan katika maeneo ya wananchi wanaoishi
katika maeneo ya Delta kwa ajili ya kukagua miradi mbali mbali ya
maendeleo pamoja na kubaini changamoto za muda mrefu zilizokuwa
zinawakabili ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.
Kutokana
na kuwepo kwa hali hiyo Mwandishi wa habari hizi aliweza kuzungumza na
baadhi ya wakinamama ambao ndio wameonekana kuguswa zaidi katika afya
akiwemo Fatma Mbashilu na Hafiswa Hamada wametoa kilio chao kwa Naibu
Waziri huyo na kuweka bayana changamoto zinazowakabili wakati wa
kujifungua kwani wanapandishwa katika kitanda cha kamba ambacho sio
salama na kinawaumiza sambamba na kijifungulia kwa kutumia mwanga wa
kibatali kutokana na eneo hilo la visiwani kutokuwa na nishati ya umeme.
“Sisi
katika kijiji chetu hususan kinamama wajawazito kwa sasa tunakabiliwa
na changamoto nyingi hasa katika upatikanaji wa kupewa huduma, kwani kwa
sasa tunajifungulia katika kitanda cha kamba kwa hiyo tunajikuta wakati
wa kujifungua tunapata maumivu mara mbili, kwa hiyo tunamwomba Waziri
Jafo kwa kuwa ameamua kuja kututembelea huku visiwani atusaidie sisi
wakinamama,”walisema kwa uchungu wakinamama hao.
Aidha
walisema mbali na kukabiliwa na changamoto hiyo ya kitanda pia kero yao
nyingine kubwa ni kutokana na kutumia mwanga wa kibatari katika
kujifungulia na wakati mwingine wanakosa kabisa hela ya kununulia mafua
ya taa, hivyo wanajikuta wanapata shida sana hasa katika nyakati za muda
wa usiku wanakuwa katika hali ya sintofahamu.
Pia
wakinamama hao walimpongeza Jafo kwa kuamua kwenda kuwatembelea katika
maeneo ya delta wanayoishi kwani kwa kipindi kirefu hawajawahi kuona
kiongozi mkubwa wa kitaifa wa serikali ambaye amekwenda kuwajulia hali,
hivyo ujio wa waziri huo utaweza kuleta mabadiliko chanya katika kuleta
maendeleo kwa wakazi wanaoishi maeneo hayo.
Naye
Mganga mfawidhi wa zahanati ya Mchinga Kuluthumu Zuberi amekiri kuwepo
kwa tatizo la kipindi cha muda mrefu kwa wakinamma hao kujifungulia
katika mazingira amabayo sio rafiki kwa upande wao kwa kutumia kitanda
kilichojengwa kwa miti na kamba ambapo amedai kiafya sio nzuri hivyo
serikali inapaswa kuwasaidia ili kuboresha utoaji wa huduma kwa
wagonjwa.
Akijibu
malalamiko ya hayo ya wananchi Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi
Seleman Jafo ambaye alionekana kuchukizwa na kuwepo kwa hali hiyo
aliamua kuchukua maamuzi magumu na kwa kupiga marufuku kabisa tabia ya
kuona wauguzi au madaktari kuwalaza wakinamama wajawazito katika vitanda
vya kamba pindi wanapokwenda kujifungua kwani kufanya hivyo kuna
hatarisha usalama wa uhai wa mama na mtoto anayezaliwa.
Jafo
alisema kuwa serikali ya awamu ya tano lengo lake kubwa ni kihakikisha
kwamba wanaboresha sekta ya afya kuanzia ngazi za vijijini hivyo
wamejipanga vilivyo katika kuzitatua changamoto zinazowakabili wananachi
ili kuweza kuwapatia huduma nzuri, na kuongeza kuwa ameshamwagiza
mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti kupeleka kitanda katika zahanati ya
kijiji cha Mchinga ili wakinamama waondokana na kero hiyo ya
kujifungulia katika kitanda cha kamba.
“Ninaagiza
kuanzia sasa sitaki kuona wakinamama wajawazito wanajifungulia wakiwa
katika kitanda cha miti, hii kwa upande wangu sipapendezwa nayo hata
kidogo kwani inahatarisha maisha ya mama pamoja na mtoto wake kwa hivyo
viongozi wa Wilaya ya Kibaiti kwa hili naomba mlifanyie kazi kwa haraka
kupeleka kitanda kingine,”alisema Jafo.
Aidha
katika hatua nyingine Jafo amewaagiza viongozi wa halmashauri ya Kibiti
kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajikite
zaidi kuwahudumia wananchi wao ikiwa sambamba na kuweka kipaumbele zaidi
katika kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa madawa ya kuwatibu
wagonjwa wakati wote hasa katika zahanati zote zilizopo katika maeneo
yote yaliyozungukwa na maji Delta.
Naibu Wazari huyo kwa sasa yupo anaendelea na ziara yake ya kikazi katika
Mkoani Pwani ikiwa ni moja kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo
pamoja na kuweza kuibaini changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi
hasa wale hasa wale wanaoishi vijijini ambao wamekuwa wakisahaulika na
viongozi wao na kujikuta wanakosa mahitaji na huduma mbali mbali za
msingi ikiwemo, afya, elimu, maji hivyo kuwafanya waishi katika
mazingira magumu na kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment