Tuesday, January 24, 2017

MOUNT MERU RICKERNEST MUSIC BAND YAJA KWA KASI JIJINI ARUSHA, YAAHIDI KUFANYA MAPINDUZI YA MUZIKI WA DANSI NCHINI

Habari picha na Woinde Shizza,Arusha 
Bendi mpya ya mziki wa dance ijulikanayo kwa jina la Mount Meru Ricknest music bandi imezinduliwa rasmi mkoani Arusha ikiwaahidi wapenda mziki wa dance burudani isiokuwa na mpinzani. 

Akiongea na waandishi wa habari jana mmoja wa wakurugenzi wa bendi hiyo Ernest mlolere alisema kuwa kwa sasa wameitambulisha bendi hiyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha tu na wanatarajia kuzindua bendi hiyo rasmi katika siku ya wapendanao (valentine day ) hapa hapa jijini Arusha. 

Alibainisha kuwa bendi hiyo ipo chini ya wakurugenzi watatu akiwemo yeye mwenyewe Ernest Mlolere, Denis Kaiza pamoja na Prisca Aloyce ambapo wamekaa chini na wakaamua kuanzisha bendi hiyo ili kuweza kuwapa burudani wakazi wa mkoa wa Arusha ambao wamekuwa wakikosa burudani ya bendi ya uhakika kwa muda mrefu. 

Alisema kuwa kumekuwa na bendi jijini hapa lakini zimekuwa hazikoshi nyoyo za wapenzi wao wa musiki wa dance hivyo wameona wawaletee wanamusiki wenye uzoefu, wenye vipaji vya kutosha ili wananchi wa mkoa wa Arusha pamoja na jirani kuweza kupata burudani. 

Aidha aliongeza kuwa bendi hii haitakaa Arusha tu bali itakuwa inatembea mikoa mbalimbali ili kuwapa burudani wapenzi wa music wa dance wa nchi nzima. 
“Tumejipanga vyema. Tunaweza na tuna uhakika ujio wa bendi hii utawafurahisha na kuwashika wapenzi wengi wa music wa dance kwani wanamuziki ambao wapo katika bendi hii ni wazuri na wana vipaji vya kutosha. Nadhani unajua kabisa ukiwa na kitu kizuri lazima watu wakipendi naamini kabisa wetu wapenzi wa bendi watawapenda. 

 Alibainisha kuwa katika bendi hii pia kuna wana music kutoka katika bendi maarufu za nje ambapo alitaja baadhi ya wanamusic waliotoka katika bendi za nje kuwa ni pamoja na rais wa bendi Fabrice Kinyenya (kulialia) ambapo yeye ametoka katika bendi ya Ferre Gola pamoja na Katoto (Tanesco) ambaye yeye ametoka katika bendi ya Fally Ipupa nchini DRC. 

Aliongeza kuwa wanajua kabisa kuna bendi zilizotangulia hapa nchini na zinaaminika ila kwa jinsi walivyojipanga yeye na wanamuziki wake ana imani kabisa watazipita bendi zote zilizopo hapa nchini na hata zile zilizoanzishwa hivi karibuni zilizopo jijini hapa. 

 “Sasa hivi tupo katika harakati za kupanga siku ya uzinduzi rasmi wa bendi hii ila hii leo tumekuja kuwaonjesha wakazi wa mkoa wa Arusha kuwa kuna bendi inayopiga vizuri sana iliopo hapa mkoani kwao. Na kwa kuwa ni nyumbani tumejipanga kila siku ya Jumamosi kuwapa burudani ambapo tutakuwa tunapiga katika ukumbi wa Triple A”, alisema Mlolere. 

Kwa upande wake Rais wa bendi hiyo Fabrice Kinyenya (Kulialia) alisema kuwa wamejipanga vilivyo kuwapa wapenzi wa musiki wa dance burudani ya uhakika ambayo itamkosha kila mtu nyoyo. 

 “Mimi sipendi kuongea sana. Napenda kufanya vitendo zaidi. Wasanii wangu wapo vizuri na nachosema tu ni kuwa wapenzi wa musiki wa dance wasubiri kupata burudani ya nguvu yenye viwango vya kimataifa. Hapa ni kazi tu hakuna maneno mengi “alisema Fabrice. 

Alisema kuwa hadi sasa wameshatunga nyimbo za bendi na watazitambulisha siku ambayo bendi itazinduliwa rasmi, akibainisha kuwa bendi hiyo ina nyimbo nzuri ambazo zitamfurahisha kila mtu. 

Hii ni bendi ya tatu kuzinduliwa ndani ya jiji la Arusha kwani kabla ya hii kipindi cha mwaka uliopita 2016 bendi mbili zilianzishwa jijini hapa ambapo bendi ya kwanza ya ikiwa mjengoni music band, na pia kuna bendi ya East Afrika music bandi zote zikiwa ni bendi za musiki wa dance. 

Hivyo wakazi wa jiji hili wamenufaika kwa kuletewa muziki wa ladh tofauti na kipindi cha nyuma ambapo wakazi wa jiji hili walikuwa wakipata taabu sana kupata burudani ya muziki wa live band.

 Rais wa bendi ya  Mounti Meru Rickernest Music Band Fabrice Kinyenya (kulialia) Akiwa anaimba katika usiku wa kuwatambulisha bendi hiyo wakazi wa jiji la Arusha
 wanamusiki wa bendi ya Mounti Meru Rickernest Music Band wakiwa wanaonyesha kiwango chao ndani ya ukumbi wa Triple A jijini Arusha
 waimbaji wa bendi ya  Mounti Meru Rickernest Music Band wakiwa fanya yao

 Wanenguaji wa bendi ya Mount meru Rickernest Music Band wakifanya yao

 Rais wa bendi akifanya mambo ndani ya ukumbi wa Triple A
 Wa kwanza kulia ni mmoja wa wakurugenzi wa bendi ya  Mount meru Rickernest Music Band Akifatilia onyesho, wa pili kushoto ni mkurugenzi mwingine wa bendi hiyo Prisca Aloyce wote wakiwa wanafatilia kwa makini onyesho.
No comments: