MKUU wa wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa (pichani) ametoa
jukumu kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Yohana Sintoo la kuamua
hatma ya watumishi wake watano wanaotajwa katika tuhuma za ubadhilifu wa fedha
wakati wa zoezi la utengenezaji wa madawati.
Akiwa ndio mamlaka ya nidhamu kwa
watumishi wa halmashauri hiyo,Mkurugenzi Sintoo ndiye mwenye maamuzi ya
kuwasimamisha kazi watumishi hao baada ya tume iliyoundwa na mkuu wa wilaya
hiyo, Byakanwa kumaliza kazi yake ya uchunguzi dhidi ya watumishi hao na
kubaini mapungufu kadhaa.
Akihitimisha taarifa yake wakati wa kikao
na watumishi wa halmashauri hiyo,Byakanwa aliagiza taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watumishi
hao akiwemo aliyekuwa kaimu Mkurugenzi ,Mhandisi Kweka.
“Mamlaka ya nidhamu ya watumishi wa
Halmashauri ni mkurugenzi pamoja na baraza la madiwani ,lakini mwajiri ni
ofisi ya katibu tawala mkoa ,Ofisi hizi mbili ndizo zinazoweza kukaa na
kuchukua hatua za kuzuia matukio au vitendo kama hivyo.”alisema Byakanwa.
“Niishauri ofisi ya Katibu tawala mkoa wa
Kilimanjaro pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai
ambayo ndio mamlaka ya nidhamu kwa watumishi hao kupima kuhusu hatua za
kuchukua dhidi ya watumishi hawa”aliongeza Byakanwa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema tuhuma
zinazowakabili watumishi hao ,majina yao tumeyahifadhi kwa sasa ni pamoja na
kupitisha barua ya malipo bila kujiridhisha kama kuna mkataba wa kutengeneza
madawati na kufanya malipo ya fremu za madawati badala ya madawati.
Tuhuma nyingine inaihusu timu ya ukaguzi
iliyokiri kukamilika kwa kazi bila ya kuonesha kama walipokea madawati au
walienda kukagua kazi ya mzabuni licha ya mzabuni kuomba malipo ya fremu
za madawati badala ya Madawati kamili.
Ofisi ya elimu msingi,ofisi ya
mkurugenzi,ofisi ya Mhasibu wa Halamshauri na kitengo cha manunuzi pia
zinatuhumiwa kushindwa kubaini nyaraka zilizowasilishwa na mzabuni endapo
zilikuwa ni kwa ajili ya fremu za Madawati badala ya Madawati kamili.
Katika kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa
mikutano wa Halmashauri hiyo Byakanwa alisema kampuni iliyopewa zabuni ya
kutengeneza madawati ni ya Ujenzi na haijawahi kufanya kazi ya kutengeneza madawati,
kuwa na karakana wala vifaa vya uselemala.
Byakanwa alisema kwa malipo yaliyofanyika
Halmashauri ilipoteza zaidi ya sh Mil 12 huku akishangazwa na hatua ya mmoja wa
watumishi wanaotuhumiwa kuomba malipo badala ya mzabuni.
Akionyesha namna watumishi hao walivyokiuka
taratibu Byakanwa alisema taarifa ya uchunguzi inaonyesha Halmashauri iliunda
timu ya ukaguzi ambayo katika cheti cha ukaguzi na mapokezi ya bidhaa
kinaonyesha bidhaa au madawati yalipelekwa ,Julai 16, 2016 ,siku 12 tangu siku
ya mkataba na mzabuni.
“Mmoja w wajumbe wa kamati hiyo ya ukaguzi
alikuwa ni mjumbe wa kamati ya kuratibu zoezi la Madawati ,alikuwa na jukumu la
kusambaza mbao kwa wazabuni na alikuwa anajua kuwa hajapeleka mbao za kutosha
kwa mzabuni ,katika maelezo yake mbele ya tume anakiri kuwa mzabuni hajamaliza
kazi kwa sababu Halmashauri haijampa mbao.”alisema Byakanwa.
Alisema mzabuni aliieleza tume kuwa anadaiwa
madawati 246 na halmashauri na kuwa amekamilisha kutegeneza madawati 154 na
ueleza kua alishindwa kukamilisha kutokana na kukosa mbao kutoka halmashauri.
“June 9,2016 malipo ya Sh Mil 19.2 yakalipwa kwa
ajili ya fremu za madawati siyo Madawati.Vocha ya malipo ikasainiwa na DT na
kuandaliwa na mtumishi mwingine (jina tunalo) ikakamilisha
mchezo.”alisema Byakanwa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kufanya hivyo
ilikuwa ni kinyume cha taratibu za malipo kwa kuwa wahusika walipaswa
kujiridhisha na nyaraka walizokuwa wakitumia ,kwa nini mzabuni aliamua
kudanganya Halmashauri.
Byakanwa aliishauri ofisi ya Katibu tawala mkoa
wa Kilimanjaro pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Hai
ambayo ndio mamlaka ya nidhamu kwa watumishi hao kupima kuhusu hatua za
kuchukua dhidi ya watumishi hao.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya
wilaya ya Hai,Yahana Sintoo alisema licha ya kwamba amefika wakati zoezi la
uchunguzi lina kamilika bado atafanyia kazi taarifa hizo kwa umakini mkubwa ili
kujiridhisha na utendajji kazi wa watumishi wa halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment