Tuesday, January 17, 2017

Mkuranga, Rufiji na Kibiti kuunganishwa katika Gridi ya Taifa

Mbunge wa jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega,( kulia)akimueleza jambo Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani( kushoto) wakati wa ziara ya kukagua miradi ya umeme vijijini wilayani Mkuranga katika kijiji cha Njopeka.

Na Zuena Msuya, Pwani

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema Wilaya za Mkuranga, Rufiji pamoja na Kibiti mkoani Pwani zitaunganishwa katika Gridi ya Taifa wakati wa kuanza kwa Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mradi Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO).

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kukagua maendeleo na utekelezaji Mradi wa Umeme Vijiji katika  Wilaya hizo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Alifafanua kuwa ni lazima Wilaya hizo zikaungwanishwa katika Gridi ya Taifa ili waweze kupata umeme mwingi, wa kutosha na wa uhakika ili kuongeza kasi na ufanisi katika shughuli za wananchi za kujipatia maendeleo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani, (aliyesimama), akizungumza na Wakazi wa Rufiji wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijiji (REA) katika wilaya hiyo.

dkt. kalemani aliweka wazi kuwa wakati wa kutekeleza awamu ya tatu ya mradi wa rea, tanesco itajenga kituo kikubwa cha kupokea na kupoza  umeme katika Wilaya ya Mkuranga ili kusambaza katika Wilaya hizo. 

" Umeme unaopatikana hapa Mkuranga , Kibiti na Rufiji kwa sasa hautoshelezi mahitaji ya watumiaji,ni mdogo sana na unakatika mara kwa mara,kwa kuwa shughuli za kiuchumi zimeongezeka, sasa suluhu ya tatizo hili ni kuunganisha Wilaya hizi katika Gridi ya Taifa mara tu baada ya REA, Awamu ya Tatu kuanza", alisema Dkt. Kalemani. 

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa huduma ya umeme kwa sasa ni jambo la lazima kwa kila mtanzania ili kurahisisha maendeleo, hivyo ni vyema kila mmoja ajiunganishe na huduma hiyo kupitia  Mradi wa REA ambao huduma hiyo hupatikana kwa bei nafuu na Serikali imeugharamia kwa asilimia mia moja kwa ajili wananchi wa vijijini.
Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa, akizungumza na wakazi wa rufiji (hawapo pichani)wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani ya kukagua miradi ya umeme vijijini wilayani Rufiji.

Katika hatua nyingine, aliwagiza wakandarasi wote wanaotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili, katika Mkoa wa Pwani,kuwasha umeme katika vijiji vyote ambavyo vimepitiwa na kuunganishwa na mradi wa huo ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Januari kabla ya kuaza kwa Awamu ya Tatu ya Mradi huo.

Pia alimuagiza Meneja Tanesco wa Mkoa huo kusimamia wakandarasi hao ili kutekeleza agizo hilo, na endapo halitatekelezwa kama alivyoagiza hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

"Mwishoni mwa mwezi huu nataka kuona vijiji vyote vilivyounganishwa na REA vinawashwa umeme, nawaagiza wakandarasi wote kutekeleza agizo hilo, Meneja Tanesco fuatiliwa na hakikisha  jambo hili linatekelezwa kwa wakati, bila kufanya hivyo mtakuwa mmejifukuza kazi mwenyewe, kwa kuwa hakuna sababu ya kutotekeleza hili agizo", alisisitiza Dkt. Kalemani.

Sambamba na hilo aliiagiza Tanesco,kusogeza huduma zao karibu na wateja kwa kuweka madawati ama kujenga vituo vidogo vya huduma kwa wateja katika kila kijiji kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa urahisi badala ya wananchi kuwafuata Tanesco maofisini.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani, (aliyesimama kushoto), akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijiji (REA) katika wilaya hiyo.

Pia alitumia ziara hiyo kuwaeleza wananchi kuwa Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 68.5 kwa ajili ya kuwalipa fidia, jumla ya wananchi 2913 waliopisha Mradi wa msongo mkubwa wa umeme kutoka Somanga hadi  Kinyerezi katika vijiji  vilivyopitiwa na mradi huo.

Vilevile alibainisha kuwa fidia hiyo italipwa kwa ratiba maaalum ili kuondoa usumbufu kwa wananchi, ambapo mpaka sasa zaidi ya shilingi Bilioni 42, zimelipwa kwa wananchi 923, huku zoezi la ulipaji likiendelea kwa mujibu wa ratiba na linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na REA kwa kushirikiana na TANESCO unatarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu( Januari)mwaka huu, na utatekelezwa kwa takribani kipindi cha miaka minne.

Wakazi wa Rufiji wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani (hayupopichani) alipokuwa akizungumza wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijiji (REA) katika wilaya hiyo.Wakazi wa Kijiji cha Ikwiriri wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani( aliyenyoosha mkono katikati) wakati wa ziara ya kukagua miradi ya umeme vijijini wilayani Rufiji.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani, (jukwaani kushoto) na mbunge wa Kibiti, Ally Ungando( kulia) akizungumza na Wakazi wa Kijiji cha Jaribu Mpakani wilayani Kibiti, mkoani Pwani wakati wa ziara yake ya kukagua Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijiji (REA) katika wilaya hiyo. Wananchi hao wanadai fidia baada ya kupisha mradi wa kupitisha msongo mkubwa wa umeme kutoka Somanga hadi Kinyerezi jijini Dar es salaam.

No comments: