Dkt, Mohammed Seif Khatibu |
Na Judith Mhina - MAELEZO
Waziri
katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Pili na ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, Dkt, Mohammed Seif Khatibu amesema
Mapinduzi ya Zanzubar ya mwaka 1964 yalimaliza mateso ya muda mrefu
waliyoyapata Waafrika wa Tanzania Bara na Visiwani.
Dkt,
Mohammed Seif Khatibu amesema hayo alipohojiwa na Idara ya Habari - MAELEZO leo
kuhusiana na mafanikio yaliyopatikana tangu mapinduzi ya Zanzibar yalipofanyika
miaka 53 iliyopita. Amesema, Mapinduzi yameondoa madhila ya utumwa, masuria, kubaguliwa,
kufanyishwa kazi, kudhalilishwa, kunyanyaswa, kudharauliwa na kuuzwa kama
samaki:
“Inashangaza
kuona Watanzania hawasheherekei ipasavyo Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa kama si
Mapinduzi hayo mateso na madhila kwa Waafrika wa Bara na Visiwani yangeendelea”.
“Madhila ya Zanzibar hayawagusi Waafrika wa Zanzibar peke yake, bali pia
Waafrika wa Tanzania Bara”.
Aliongeza kwa kusema “Mapinduzi Daima” maana
yake ni endelea kutekeleza yale yaliyokusudiwa na “Mapinduzi” usawa, umoja na
mshikamano ambao utapatikana pale tu kila mtu akipata huduma bora za afya,
elimu, maji, umeme na makazi bora ambayo kwa asilimia kubwa Rais wa Zanzibar Shekh
Abeid Amani Karume alitekeleza.
Akizungumizia
maadhimisho ya miaka 53 ya Maapinduzi ya Zanzibar Waziri huyo wa zamani amesema,
Mapinduzi yaliyofanywa mwaka 1964 yanahitaji kuendelezwa kwa sababu yameleta
ukombozi wa Waafrika, yameondoa utawala wa Uingereza na Waarabu. Kujitawala
maana yake Wanzanzibar wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kujituma
ili kujiletea maendeleo.
Alifafanua
suala linalotiliwa mkazo na Rais Dkt Ali Mohammed Shein la nidhamu kazini alisema “Hili ni tatizo kubwa sana kwa Zanzibar,
Wazanzibar wengi hawajali kazi hawaoni kama maisha yao yanategemea kazi mpaka
imekuwa sehemu ya utamaduni wao kutothamini kazi. Hivyo, ni lazima mfumo mzima
ubadilike na kuona watu wana wajibu wa kazi. Rais anahitaji kuungwa mkono
katika hili maana akiachiwa mwenyewe hataliweza ni lazima tulichukulie kwa
mtazamo wa pamoja.
Akijibu
maswali mawili mosi, kuhusiana na lipi la kujivunia kutokana na Mapinduzi ya
mwaka 1964 alisema: “Mpaka leo Mapinduzi yanakumbukwa naona fahari sana kwa hilo”. Kama sio
Mapinduzi mpaka kesho Sultani angeendelea kutawala, kama sio yeye mwanae au
mjukuu wake. Pia,
dhamira ya kuzindua mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo wakati wa
maadhimisho hayo kunaendeleza dhamira ileile ya Mapinduzi iliyokusudiwa mwaka
1964.
Pili, kwa nini vyama vya siasa vya Upinzani vinalalamika kuwa
Demokrasia inakandamizwa Zanzibar, alisema: “Nadhani hii ni tabia au hulka ya
nchi za Afrika za kupinga kila kitu wakati wa uchaguzi ili mradi upande wa
anayelalamika umeshindwa, lazima atasema uchaguzi sio huru na wa haki, hali
kadhalika kwa upande mwingine. Lakini kwa yoyote anayeshinda uchaguzi ulikuwa
huru na wa haki”.
Akitoa ushauri Dkt Khatib alisema “Mimi nadhani mambo ambayo
Zanzibar wanaweza kufanyia kazi ni mambo
matatu. Kwanza viwanda vya samaki, pili utalii wa ndani katika utamaduni na
kutembelea maeneo ya kihistoria, mwisho Utalii
wa matibabu kujenga hospitali nzuri yenye huduma zote, ili wakati watalii
wanakuja Zanzibar anapata nafasi ya kupewa matibabu. Utalii huu ni maarufu sana
nchi za Urusi na China.
Pia, kwa vijana wa Zanzibar wapewe maeneo ya ardhi Tanzania
Bara waweze kulima na kuzalisha chakula ambacho kitapelekwa Zanzibar. Zoezi
hili litatoa nafasi ya vijana kujifunza, kujiajiri na kuwa na tabia ya kupenda kazi.
Mwisho
alimalizia kwa kutoa wito kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kujenga makumbusho ya kisasa ili kizazi cha sasa na kijacho, waone,
wajue na kujifunza nini kilitokea kabla ya Mapinduzi, kwa nini tunasheherekea
Mapinduzi na kwa nini tunasema tuko huru.
Huku akionesha msisitizo: “Ni vema kuonyesha katika picha na
sura halisi historia ya Zanzibar kabla ya Waajemi, Wareno, Waarabu, Waingereza
na sasa Mapinduzi”.
“Vijana wengi ukiwaambia nchi hii kulikuwa na unyanyasaji wa Waafrika
hawakubali, maana kuna wasioitakia mema Zanzibar wanapotosha historia hiyo”.
No comments:
Post a Comment