Sunday, January 29, 2017

Meya wa jiji la Dar ahimiza upendo kwenye huduma za afya

NA CHRISTINA MWAGALA,Dar es Salaam

MEYA wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amewataka Madaktari ,wauguzi pamoja na watoa huduma za afya katika Hospitali Vijibweni kutumia taaluma yao vizuri  ili kuwawezesha wananchi wa eneo hilo kupata huduma nzuri.

Meya Isaya ametoa ushauri huo jijini Dar es Salaam jana katika hafla iliyoandaliwa na wauguzi wa Hospitali hiyo iliyopo Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati walipokuwa wakiuwaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017.

Katika hafla hiyo pamoja na mambo mengine Meya Isaya alisisitiza kwamba kila mmoja anapaswa kufanya kazi kwa upendo kwani kazi yao ni yawito kuliko sekta nyingine.

Alisema wananchi wanapopata huduma nzuri hupata faraja lakini wanapokumbwa na misukosuko kwa watoa huduma sio jambo zuri kwani unaweza kumuongezea mgonjwa maradhi mengine na hivyo akawasihi wafanye kazi zao kwa upendo.

“ Niko pamoja na nyinyi, najua kazi yenu hii ni yawito, lakini mnaposhindwa kufanya kama ambavyo imekusudiwa hili ni tatizo, kwanini mpate sifa mbaya katika huduma yenu?” aliuliza Meya Isaya.

Awali akisoma risala Dokta wa hospitali hiyo, alisema kwamba Hospitali hiyo inatoa huduma za rufaa kwa Kata za vijibweni ,Mjimwema, Kigamboni, Tungi, Somangila, Kibada na maeneo yote ya manispaa ya Kigamboni ambapo kwa sasa hospitali hiyo ndio inayofanya kazi za hospitali ya Wilaya katika manispaa ya Kigamboni.

Alieleza kwamba Hospitali hiyo inatoa huduma za wagonjwa wa nje (OPD) na ndani (IPD) pamoja na vipimo mbalimbali vya maabara na Ultrasound, Huduma za meno, Macho, Kisukari, huduma za maabara, baba na mtoto, magonjwa ya akili ,wagonjwa walio na maambukizi ya Ukimwi pamoja na mazoezi ya viungo.

Alieleza kwamba hospitali hiyo kwa sasa imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kununua mashine ya kisasa ya Ultrasound kwa mkopo wa bima ya afya, kufungua chumba cha matibabu kwa ajili ya wagonjwa wabima.

Aidha alisema kwamba kununua mashine ya kufulia kwa ajili ya kuendesha shuguli za ufuaji wa mashuka ya wagonjwa na nguo nyingine kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa.

Mafanikio mengine waliyataja kuwa ni kuendesha malipo ya huduma za afya kwa njia ya Kielekronikia, kuongezeka kwa mapato kutoka milioni 10 kwa mwezi hadi kufikia milioni 18, nazaidi kwa mwezi sambamba na mapato yatokanayo na bima toka milioni 6 hadi milioni 10.Akizungumzia changamoto alisema kwamba wanaupungufu wa wafanyakazi 117 wa kanda mbalimbali ,kujaa mara kwa mara kwa matanki ya kuhifadhia maji taka na hivyo kusababisha gharama kubwa ya unyonyaji wa maji taka.

No comments: