Na Othman Khamis Ame, OMPR,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa linawategemea Vijana wakati wowote katika dhana nzima itakayothibitisha kwamba wanasimamia kwa vitendo Mapinduzi katika kuondoa maovu yote yanayolikabili Taifa.
Alisema Serikali zote mbili ile na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na iIe ya Mapinduzi ya Zanzibar zinataka kuona Vijana wake wanakuwa chem chem ya Maendeleo badala ya kuwa dimbwi la matatizo mitaani.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyafunga Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi { UVCCM } kuunga mkono maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Alisema Vijana ambao ndio warithi wa kulinda Mapinduzi ya Zanzibar dhana iliyoanzishwa na muasisi wa Mapinduzi hayo Mzee Abeid Amani Karume wana wajibu wa kusimamia vita vya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya, udhalilishaji wa wanawake na watoto, uonevu pamoja na ufisadi.
Balozi Seif alikariri maneno ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume yaliyoeleza maana halisi ya Mapinduzi daima ambayo sio kupindua watu bali ni kuondoa matendo mabaya katika jamii na kusimamia haki na mazuri yote.
Akizungumzia changamoto kubwa zinazowakabili Vijana hasa ukosefu wa ajira ambalo limekuwa likizikumba nchi mbali mbali Duniani Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Mipango imara ya kukabiliana na changamoto hiyo .
Mapema akitoa taarifa ya matembezi hayo Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Tanzania Ndugu Shaka Hamdu Shaka alisema Vijana wengi nchini huingia katika majaribu ya kudanganywa historia ya Zanzibar na kupelelekea kukejeli Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Nd. Shaka alisema Mapinduzi ya Zanzibar yametandikwa kwa zulia la Umoja, Upendo na mshikamano chini ya majemadari waliofanya mapinduzi hayo ambao wanastahiki kuendelea kuenziwa na wananchi na Vijana wa kizazi cha sasa.
Akitoa salamu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania anyesimamia Mazingira na Muungano Mh. Januari Yussuf Makamba alisema Mapinduzi ya Zanzibar ni kielelezo tosha cha kujitambua kwa waafrika wa Visiwa vya Zanzibar.
Mh. Januari alisema Wakombozi wa Mapinduzi ya Visiwa vya Zanzibar wameacha urithi mkubwa kwa vijana wa Kizazi kipya unayostahiki kulindwa na kuendelezwa kwa faida na maslahi ya Wananchi wake.
Alisema njia pekee na sahihi ya kuendelea kuimarika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kudumisha Mapinduzi ya Zanzibar kupitia njia ya kuipatia ushindi CCM katika chaguzi zote zinazoendelea kufanyika hapa Nchini.
No comments:
Post a Comment