Wednesday, January 11, 2017

MAJALIWA AZINDUA BARABARA YA MWANAKWEREKWE HADI FUONI- ZANZIBAR


   Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua barabara ya Mwanakwerekwe hadi Fuoni yenye urefu wa kilomita 4.1 iliyopo Zanzibar Januari 11, 2017.  Kushoto ni  Waziri wa  Ujenzi,  Mawasiliano na  Usafirishaji, Ali Karume . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifurahia baada ya kuzindua barabara yenye urefu wa kilomita 4.1  ya kutoka Mwanakwerekwe hadi Fuoni Zanzibar ikiwa ni moja ya shughuli za sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 11, 2017.  Katikati ni Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa rais wa Zanzibar, Mohammed Abood na Kulia ni  Mkuu wa mkoa waMjini Magharibi, Mohammed Mahmoud. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa akiwapungia wananchi wa Zanzibar wakati alipowasili kwenye eneo la  Barabara ya Mwanankwerekwe  hadi Fuoni kufungua barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 4.1 Januari 11, 2017. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi, , Mawasiliano na Usafirishaji, Ali Karume. (Picha na  Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Baadhi ya wananchi wa Zanzibar wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza baada ya kuzindua barabara ya Mwanakwerekwe hadi Fuoni yenye urefu wa Kilomita 4.1 ilyopo Zanzibar Januari 11, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika dua iliyosomwa baada ya kuzindua barabara ya Mwanakwerekwe hadi Fuoni yenye urefu wa Kilomita 4.1 iliyopo Zanzibar Januari 17, 2017.Wengine pichani kutoka kushoto ni Spika wa Baraza la Wawakilishi,   Zubri Ali Maulid, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohammed Mahmoud na kulia ni Waziri wa Ujenzi, Mawsiliano na  Usafirishaji, Ali Karume. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali wahakikishe wanawasimamia vizuri wakandarasi wanaojenga miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya barabara ili viwango vyake vifalingane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Januari 11, 2017) wakati akizundua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kwerekwe/Fuoni yenye urefu wa kilomita 4.01 iliyogharimu sh. bilioni 10.07 zilizotolewa na Mfuko wa Barabara. Ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015.

Waziri Mkuu amezindua barabara hiyo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli ikiwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika miradi ya ujenzi wa barabara hivyo watendaji wake hawana budi kuhakikisha miradi hiyo inalingana na thamani halisi ya kiwango cha fedha kinachotolewa.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watendaji hao kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kulinda na kuhifadhi miundombinu hiyo na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kufanya uharibifu ikiwemo uchomaji wa matairi katikati ya barabara.

Pia amewataka wananchi kutojenga majengo ya kudumu katika hifadhi ya barabara ili kuepusha usumbufu pale Serikali inapotaka kuyatumia maeneo hayo. “Lazima wananchi wazingatie sheria ya hifadhi ya barabara,”

“Serikali imedhamiria kuboresha mawasiliano kwa kujenga barabara zetu kwa kiwango cha lami. Hatatutakubali kuona mtu anaharibu miundombinu hii tunayoijenga kwa gharama kubwa ikiharibiwa. Lazima tuilinde ili iweze kutunufaisha wote,” amesema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka madereva wote kuhakikisha wanakuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ikiwemo kusimama kwenye alama za kuvukia watembea kwa miguu na atakayekaidi achukuliwe hatua.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bw. Mustafa Aboud Jumbe alisema barabara hiyo ni sehemu ya awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Kwerekwe hadi Tunguu.

Alisema awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo wa barabara itakuwa na urefu wa kilomita saba na itaanzia Fuoni hadi Tunguu inatarajiwa kuanza katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha.

Katika hatua nyingine, Bw. Mustafa alitaja changamoto zinazoikabili barabara hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa mitaro ya maji ya mvua jambo linalosababisha maji kutuama barabarani hivyo kutishia uhai wa barabara hiyo.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JANUARI 11, 2017

No comments: