Tuesday, January 24, 2017

Kijiji cha Mwanzega kupata umeme wa REA

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga
KIJIJI cha Wasanii cha Mwanzega kimechaguliwa kuwemo kwenye orodha ya vijiji saba ambavyo vimepangiwa kupata umeme wa Serikali wa Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA).

Mtendaji wa kijiji cha Mwanzega, Kitwana Kambangwa aliwaomba wanakijiji wasipuuzie fursa hiyo kwa vile serikali imeona umuhimu wa kijiji hicho kupata umeme ili kurahisisha maendeleo.

Akiwasomea wananchi taarifa ya Mratibu wa Vijiji na Kata wa Utawala bora na maboresho wa wilaya ya Mkuranga kuhusu mradi huo, Mtendaji wa kijiji, Kambangwa alisema wananchi wewe tayari kutoa miti yao ya mazao na mimea bila fidia ili kupisha kazi ya kupitisha nguzo za umeme wa REA.

'Ndugu zangu Serikali ya Rais John Magufuli imetusikia kilio chetu sisi watu wa vijijini, tunaletewa umeme ili tuwe na maendeleo kama wenzetu wa mjini, tusiipuzie nafasi hii kubalini kupisha nguzo zipite bila kulalamikia fidia' alisema Mtendaji Kambangwa.

Alisema sambamba na kijiji cha Mwanzega, vijiji vingine vitakavyonufaika na mradi wa REA ni Mbezi, Msorwa, Shungubweni, Boza, Kuruti na Mbonga ambavyo mradi huo utapelekwa moja kwa moja kwenye shule za Msingi, Zahanati, Viwanda na Shule za Sekondari.

Awali wakichangia kuhusu mradi huo Dkt.Frederick Mwakibinga alisema umeme ukishaingia kijijini baada ya muda mfupi kutakuwa na maendeleo ambayo yatawanufaisha wananchi wote na kaongeza ajira kwa vijana.
Mwanakijiji mwingine Ramadhani Mwanehekwa alisema wao wako tayari kuruhusu mazao yao kukatwa bila kudai fidia lakini Serikali nayo iwakumbuke katika kuwaletea wananchi huduma za jamii, kama zahanati, barabara, maji na elimu.

Mkutano huo uliohudhuriwa na wanakijiji wengi waume, wanawake na vijana, Ali Ndambwe aliwashauri wanakijiji wenzake wasifikirie kulipwa  fidia kwa ajili ya mazao zitakapopita nguzo waangalie faida watakayoipata vijana wao na majukuu baada ya kuingia umeme na kujengewa viwanda.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Cassim Taalib aliwapongeza wanakijiji wenzake kukubali kutoa mazao na mimea yao bure kwa wale ambao mradi wa umeme utawapitia.

Katika mkutano huo Mwenyekiti wa kijiji, Abdallah Mwangira aliwataarifu wananchi hao kuwa serikali imewaandalia wananchi wa vijiji hivyo mambo makubwa ya maendeleo ambayo aliahidi kuyasema kikao kijacho.
Kijiji cha Mwanzega ndipo kilipo kijiji cha wasanii ambacho mpaka sasa zimejengwa nyumba 250 za kisasa as wasanii ambazo zitaingia kwenye mradi wa REA.

Mkazi wa Mwanzega Dkt. Frederick Mwakibinga akichangia mada kwa wanakijiji watakaonufaika na mradi huo baada ya kuukubali.



Wanakijiji wa kijiji cha Wasanii Mwanzega Mkuranga wakiwa kwenye mkutano wa kuidhinisha mradi wa Ilene wa REA kupita kijijini hali jana.

No comments: