Sunday, January 15, 2017

DOLA ZA MAREKANI BILIONI MOJA ZATENGWA KUIMARISHA ZAO LA MUHOGO NCHINI

KIASI cha Dola za Marekani bilioni moja kimetengwa kwa ajili ya kuimarisha zao la muhogo nchini kupitia mkataba wa kibiashara baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Tanzania Agricultural Export Processing Zone Limited and Epoch Agriculture (TAEPZ) kutoka China.
Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru, alisema huu ni wakati wa wakulima kunufaika na Kilimo cha muhogo baada ya kulima kimazoea.
Alisema, kwa muda mrefu Watanzania wamekua wakilima muhogo kwa ajili ya chakula tu huku wakisafirisha muhogo ghafi hali inayokosesha serikali mapato na kunufaisha mataifa ya nje kupitia zao hilo lenye manufaa mengi.

“Lengo la serikali kuwa na uchumi wa viwanda linaanza kutimia, huu ni uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo cha biashara. Kutakuwa na shamba kubwa la mihogo, kutajengwa viwanda mbalimbali vya kuzalisha unga wa mihogo, makopa, chakula cha mifugo, sukari ya viwandani na mbolea.
“Hii fursa tusiiache, kama mlikua mkilima mihogo kwa kiwango kidogo ongezeni mashamba kwa sababu soko la uhakika lipo, pia tunashauri mnunue hisa katika kampuni hii ili ikiwezekana tuimiliki kwa kiwango kikubwa,” alisema Dk. Meru.
Vilevile alipongeza urafiki wa kibiashara baina ya Tanzania na China na kumshukuru balozi wa China nchini, Balozi Lu Youqing kutokana na juhudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kati kwa kuleta wawekezaji wengi kila mwaka.
Aliongeza kuwa mradi huu utasaidia wakulima wa mihogo kuongeza ufanisi na kuhakikisha wanapata mbegu bora ili kufikia kiwango kinachotakiwa katika kipindi cha miaka mitano ya majaribio, pia kutakuwepo na mafunzo juu ya ulimaji bora wa zao hili pamoja na namna ya kusindika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye amewataka wakulima kugeukia Kilimo cha muhogo kwa sababu wawekezaji hawa wanahitaji tani milioni tano kwa mwaka.

“Takwimu zinaonyesha Tanzania tunazalisha tani milioni tano za mihogo mibichi kwa mwaka, Kampuni ya TAEPZ inahitaji tani milioni 2.5 za muhogo mkavu (makopa), maana yake ikiwa mibichi kutoka shambani inakua na uzito mara mbili.
“Tumeamua kuwaita wawekezaji kwa sababu tuliwahi kupewa fursa ya kusafirisha tumbaku na nyama kwenda China, lakini tulishindwa kutimiza vigezo kutokana na kila mmoja kusafirisha kwa namna yake bila kuzingatia ubora , naamini katika hili tutafanikiwa kutimiza malengo tuliyojiwekea,” alisema Simbeye.
Balozi wa China nchini Dk. Lu Youqing, akizungumza katika mkutano huo alisema, “naamini mkataba huu utaleta tija kwa Watanzania, kwa sababu muhogo ni zao muhimu wa raia wa China na lina faida kubwa. Rais Dk. John Magufuli wakati wa kampeni za urais pia aliwahi kugusia ushurikiano katika mazao ya chakula.
“Hata Waziri wa Mambo ya Nje Jamhuri ya Watu wa China, WANG Yi alipokuja nchini mapema mwezi huu alitilia mkazo kuhusiana na kusafirisha mazao ya biashara China. Kwa hiyo ili kuboresha uhusiano wetu ulioasisiwa na Mwenyekiti Mao Tse Tung na Mwalimu Julius Nyerere, serikali yetu itawekeza zaidi ili kukuza uchumi wa Tanzania.”

Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza Afrika kuwa na uwekezaji mkubwa kutoka China ambapo kiasi cha Dola za Marekani Bil 6.62 kimewekezwa nchini katika miradi mbalimbali. Hivyo, hata katika usafirishaji mihogo China watahakikisha Tanzania inazipita Nigeria na Ghana ambazo ndizo zinazoongoza kwa kusafirisha zao hilo kwa sasa.

Akitoa sababu za kuichagua Tanzania katika mradi huo, mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng alisema ni kutokana na ardhi yenye rutuba na wananchi wengi kujishughulisha na Kilimo cha mihogo lakini hawana soko la uhakika, hivyo wakipewa maelekezo wanaweza kufikia kiwango kinachohitajika.

“Tanzania kuna fursa nyingi za Kilimo, katika awamu ya kwanza ya mradi huu tutaanzisha kiwanda za kusindika mihongo katika mikoa mitatu ambayo ni Lindi, Pwani na Mtwara, ingawa baadaye tutaongeza mikoa mingine mradi utakapoonyesha mafanikio.
“Tuna imani na kasi ya awamu hii na ndiyo maana tumekubali kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa sababu serikali itatusaidia kuhakikisha mradi unafanikiwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Feng.
Kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa na urafiki mzuri na China katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, nishati na uchumi, hivyo hii ni fursa ya kipekee kwa wakulima kunufaika na zao la muhogo.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru (kushoto), akiwa na Mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng wakati wa kutia saini makubaliano ya mradi wa zao la muhogo nchini utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 1. Waliosimama kutoka kushoto ni balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye. Mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru (kushoto), akibadilishana nyaraka na Mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng baada ya kusaini mradi wa zao la muhogo nchini utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 1. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye. Mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru, akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya mradi wa kusindika muhogo nchini utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 1, wengine katika picha ni Mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye. Mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

No comments: