Monday, January 30, 2017

DC KILOLO ATAKA MKANDARASI WA MRADI WA MAJI IPALAMWA ASILIPWE PESA, MADIWANI WAMPA WIKI MBILI KUKAMILISHA MRADI

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo  Mhe. Asia Abdallah  akifafanua  jambo
Mwenyekiti  wa Halmashauari ya  Kilolo  akifugua  kikao  kushoto  ni mkurugenzi  mtendaji wa Halmashauri ya  Kilolo

Baraza la madiwani  Kilolo

Na MatukiodaimaBlog
BAADA ya  mradi  wa maji Ipalamwa  kujengwa chini ya  kiwango kwa bomba kupasuka ovyo kabla ya mradi  kukabidhiwa ,baraza   la madiwani  la Halmashauri ya  wilaya ya  Kilolo  mkoani  Iringa  limempa muda  wa  wiki  mbili mkandarasi  wa kampuni ya Norcom Ltd kukamilisha mradi  wa maji wa Ipalamwa  kwa  ubora unaotakiwa zinginevyo mkataba  wake  utavunjwa.

Huku  mkuu  wa  wilaya  ya  Kilolo  Mhe. Asia  Abdallah akiagiza Halmashauri hiyo  kutomlipa fedha  yeyote  mkandarasi   huyo hadi  hapo atakapokamilisha mradi  kwa  kiwango  kinachotakiwa  vinginevyo kama  kuna pesa  alilipwa awali basi  pindi  mkataba  wake utakapovunjwa atapaswa  kuzirudisha  fedha  hizo.

Wakitoa  maazimio  hayo katika  kikao  cha  baraza  la  madiwani   kilichofanyika  juzi  katika  ukumbi  wa Halmashauri  ya  Kilolo  na  kuhudhuriwa na mkuu  wa  wilaya  ya  Kilolo , madiwani  hao  walisema  kuwa wamechoshwa na mkandarasi  huyo  kuendelea kuchelewesha  mradi  huo  wa  maji na  kuwa sasa  wanaona  suala   hilo la kero ya  maji kijiji  cha Ipalamwa  lifike  mwisho  kwa  kumpa  muda  wa  mwisho  kwa ajili ya  kukamilisha mradi   huo.

Mhandisi   wa  maji  wa  wilaya ya  Kilolo Enock Basyagile   akijibu  hoja  za  baraza  la madiwani  juu ya  ucheleweshwaji  wa  mradi  huo   alisema  kuwa sababu ya  kuchelewa kwa  kazi hiyo ni  kutokana na  kukosekana  kwa   fedha kati ya Halmashauri na mkandarasi   ila  kwa   sasa  fedha  zimeingia na mchakato  wa  kufanya  kazi   hiyo  kwa  kununua  vifaa  vya mradi  huo  ikiwa ni  pamoja na mchakato  wa malipo kwa mkandarasi   huyo.

Mkuu wa  wilaya  ya  Kilolo Asia  Abdalah  alisema  hakubaliani  na  uamuzi  wa mhandisi    wa maji  wilaya  kutenga   fedha  ama  kufanya mchakato  wa malipo  ya Tsh  milioni 19 kwa  mkandarasi  huyo  aliyejenga  mradi  huo  chini ya  kiwango ila alitegemea  kuona mkandarasi  huyo anachukuliwa hatua kwa kufanya  kazi  chini ya  kiwango.
" Sikubaliani  hata  kidogo  na uamuzi  wa kumlipa fedha  mkandarasi  huyo ama  Halmashauri  kununua mabomba kwa ajili ya kukarabati  mradi ambao haujakabidhiwa  kwa  wananchi .....naagiza mkandarasi  huyo afanye  kazi hiyo  kwa gharama  zake na  asilipwe  pesa  yoyote  hadi mradi  utakapokabidhiwa "
 Mwenyekiti  wa Halmashauri  ya  Kilolo Bw Vellance Kihwaga  alisema  sababu  kubwa ya  mradi   huo  kuendelea  kusumbua kwa mabomba  kupasuka  ni  baada ya  mkandarasi huyo  kwenda  kinyume na mkataba  wa kazi  hiyo kwa kuweza mabomba membamba  zaidi    kuliko  nguvu  ya maji   hivyo pindi  maji  yakifunguliwa mabomba  hayo   hupasuka.
Alisema  kutokana na ubovu   huo  wa mabomba  kamati ya  fedha  ilifanya  ziara ya  ukaguzi  wa  mradi  huo  toka  mwaka jana  na  kumwagiza mkandarasi  huyo kufanya marekebisho  kwa  kutoka mabomba   yote  yasiyo  na ubora na  kufunga mabomba  yenye ubora  na alikubali  kuifanya kazi   hiyo  ndani ya wiki mmoja na kamati  ilimpa  mwezi  mmoja  ila hadi  sasa ni  zaidi ya miezi 4 kazi   hiyo   haijafanyika.
 Mkurugenzi  mtendaji wa  Halmashauri ya  Kilolo Bw Aloyce Kwezi alisema  kuwa mkanadarasi  huyo bado  hajalipwa  fedha   yoyote  na  kuwa Halmashauri  haitamlipa fedha  hadi  hapo mradi  utakapokamilika na anapaswa  kufanya kazi  hiyo  kwa  gharama  zake na iwapo atashindwa  kwa muda  uliotolewa basi  halmashauri  itavunja mkataba  huo. 
Wakati  huo  huo serikali  ya  wilaya ya  Kilolo imepiga  marufuku  wageni  kuingia katika  vijiji ama kata na  kuendesha  miradi  mbali mbali pasipo kushiriisha viongozi wa  ngazi  zote  za vijiji ama Halmashauri 

No comments: