Thursday, January 19, 2017

BILIONI 15 KUTUMIKA KUWAJENGEA UWEZO VIJANA

Na Fatma Salum-MAELEZO

Serikali imepanga kutumia bilioni 15 kuwapatia vijana stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam wakati wa kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Teknolojia Dar es saalam (DIT) na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Akizungumzia makubaliano hayo Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ally Msaki amesema kuwa yatasaidia kuiwezesha Taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa vijana hasa ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na ngozi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Vijana 1000 wataanza kupata mafunzo mwezi Februari mwaka huu na yatakayohusu utengenezaji wa bidhaa za ngozi na program hii ipo ndani ya mpango wa miaka mitano.” Alisema Msaki.

Mafunzo hayo ya stadi za kazi kwa vijana yatagharimiwa na Serikali na yatahusisha vijana walio katika mfumo rasmi na wale wasio katika mfumo rasmi wa elimu lengo likiwa ni kuwakwamua vijana ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Akifafanua Msaki alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kuwawezesha vijana baada ya mafunzo hayo kujiajiri na kuwaajiri wenzao hivyo kuondokana na tatizo la ajira na kuongeza nguvukazi ya taifa kwenye uzalishaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba alibainisha kuwa Taasisi hiyo imejipanga vyema kuwawezesha vijana kwa kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko na kuweka msisitizo katika mafunzo kwa vitendo.

Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) ipo imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati.

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba (kushoto) na Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Ally Msaki wakisaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi hiyo utakaowezesha vijana kupata mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya ngozi katika Taasisi hiyo Kampasi ya Mwanza ili kuchochea uchumi wa viwanda nchini.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba (kushoto) akibadilishana hati ya makubaliano ya ushirikiano na Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw.Ally Msaki (kulia), makubaliano hayo ni kati ya Taasisi hiyo na Serikali ili kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya ngozi.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba (kulia) akifafanua kwa waandishi wa Habari kuhusu mikakati ya taasisi hiyo kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na stadi zinazoendana na mahitaji ya soko. Kushoto ni Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa DIT Bw. Sebastian Ndahani.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Taarifa za Soko la Ajira Bw.Ahmed Makbel toka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu akieleza umuhimu wa vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika kuwajengea uwezo ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda. Kushoto ni Mkurugenzi wa Ajira, Bw. Ally Msaki kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. 
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Taarifa za Soko la Ajira Bw.Ahmed Makbel toka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu akieleza umuhimu wa vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali katika kuwajengea uwezo ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda. Kushoto ni Mkurugenzi wa Ajira, Bw. Ally Msaki kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.Picha na Frank Mvungi (MAELEZO) 

No comments: