Friday, December 16, 2016

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MWEKAHAZINA WA WILAYA YA BAH

*Aagiza arudishwe Longido kujibu tuhuma zinazomkabili


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na kuagiza arudishwe haraka na kuja kujibu tuhuma za ubadhilifu sh. milioni 642.4 za miradi zinazomkabili.


“Tunaendelea kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido usitegemee kuhamishiwa wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina huyu arudishwe haraka Longido,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Desemba 16, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Pia amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega kumuandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akimuomba amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo chake cha kazi cha zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.

Amesema Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo halafu kuhamishwa sehemu nyingine, “hivyo naagiza kuanzia sasa nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa kujibu kwanini ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo kwenu,” amesema.

Amesema miradi mingi ya maendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi kuweka mbele maslahi binafsi badala ya kuzingatia maadili ya utumishi, hivyo amewaagiza Wakuu wa Idara wafuatilie kwa makini miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kama inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.

Akizungumzia kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani Longido, Waziri Mkuu amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kufanya kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote watakaokutwa wanafanya biashara hiyo.

“Wilaya hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya zikiwemo bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,”.

“Ukivuta bangi unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala jambo ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua mirungi na bangi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kutaifisha magari yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.

Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo akisoma Taarifa ya Wilaya amesema Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumika kama njia kuu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi kwenda nchi jirani ya Kenya ambako biashara hiyo imehalalishwa.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa hospitali ya wilaya hali inayofanya wananchi kwenda kutibiwa Kenya, ambapo Waziri Mkuu alisema haiwezekani wakakosa hospitali ya wilaya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikiusha anatenga fedha za ujenzi huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya magadi soda ili yawe na ubora na thamani kubwa. Ametoa kauli hiyo aliposimamishwa na wananchi katika kijiji cha Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai Merugoi Wilayani Longido akitokea wilayani Ngorongoro.

Amesema lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo hasa akinamama wanaoishi karibu na Ziwa Natron linalotoa magadi hayo waweze kunufaika na uwepo wa ziwa hilo.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha vijana na akinamama hao wanaouza magadi maeneo ya pembezoni mwa barabara katika ziwa Natron kupata ajira kwa kuwa kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo mbili za Longido na Ngorongoro.

Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kushirikiana na wataalam wake kufanya tathimini ya uhaba wa chakula katika wilaya za Longido na Ngorongoro ili Serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa chakula kwa kiasi gani.

"Gambo fanya tathimini ya hali ya njaa katika wilaya hizi mbili ili tuweze kuwasaidia wananchi hawa. Hata hivyo nawaomba wananchi mtunze kiasi cha chakula mlichonacho na marufuku tumia nafaka kwa ajili ya kupika pombe,” amesema.

Awali, wananchi hao waliokuwa na mabango mbalimbali walilalamikia kero ya mipaka ya ardhi kati ya vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Afisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Bw. Hamdoun Mansour kwenda katika vijiji hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.  

No comments: