Wednesday, December 7, 2016

Waziri Mahiga akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea jijini Addis Ababa.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se ametangaza kuwa Tanzania itapokea msaada mkubwa zaidi wa maendeleo kuliko nchi yeyote barani Afrika inayotolewa na Serikali ya Korea kwa ajili ya bara hilo.

Hayo aliyabainisha leo alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Korea ulioanza jana jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mahiga aliipongeza Korea kwa hatua ya maendeleo iliyofikia ambapo katika kipindi kifupi imeweza kuendelea kiviwanda na teknolojia ili hali wakati nchi za Afrika zinapata uhuru katika miaka ya 60 Korea ilikuwa ni moja ya nchi masikini duniani.
Waziri Mahiga aliishukuru Jamhuri ya Korea kwa misaada inayoipatia Tanzania. Alisema misaada hiyo ni kwa ajili ya watu masikini kwa kuwa inaelekezwa maeneo yanayogusa watu wa chini kama vile afya, maji, elimu na miundombinu ya mawasiliano.
Waziri Mahiga aliweka wazi kuwa Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Korea kwa dhamira ya kujifunza namna nchi hiyo ilivyopiga hatua ya maendeleo ya viwanda na teknolojia ili nayo iweze kufikia azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
"Tunahitaji kushirikiana na Korea katika maeneo ya viwanda, nishati jadilifu, miundombinu, madini, tehama na gesi na mafuta. Kutokana na hatua ya maendeleo iliyofikiwa na Korea, Tanzania ina matumaini makubwa kuwa nchi hiyo itatoa msukumo mkubwa katika kuendeleza maeneo hayo".
Aliongeza kuwa Tanzania inahitaji sio ilimradi viwanda bali viwanda vitakavyotumia malighafi za kilimo na madini ambavyo licha ya kutoa soko kwa wakulima bali pia vitaongeza ajira kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Mahiga aliishauri Korea kuangalia namna itakavyoshirikiana na bara zima la Afrika, hususan kusaidia miradi ambayo itakuwa alama ya kudumu ya ushirikiano kati ya nchi hiyo na bara la Afrika. Alitolea mfano wa mradi wenye sifa hiyo ni Korea kufadhili ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao yake jijini Arusha, Tanzania. Mahakama hiyo ni muhimu katika uimarishaji wa utawala wa sheria na demokrasia barani Afrika.
Halikadhalika, Waziri Mahiga alipendekeza Chuo cha Diplomasia cha Tanzania na kile cha Korea vianzishe ushirikiano wa kindugu ili vibadilishane uzoefu na kutatua changamoto zinazovikabili vyuo hivyo kwa pamoja.
Vile vile. Mhe. Waziri alimfahamisha Waziri mwenzake kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alishateua Balozi kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania nchini Korea kwenye Ofisi ya Ubalozi itakayofunguliwa hapo baadaye katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Kwa upande wake, Mhe. Yun alieleza kuwa Tanzania ni mshirika mkubwa wa Korea na kusisitiza umuhimu wa Serikali kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji ili makampuni ya Korea yaje kwa wingi kuwekeza Tanzania. Alisisitiza umuhimu wa kukamilisha Mkataba wa Kulinda Vitega Uchumi na ule wa Kuepuka Tozo ya Kodi mara mbili kama moja ya njia ya kuvutia wawekezaji kutoka Korea.
Aidha, alikumbusha kuwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea yanatimiza miaka 25 mwaka 2017 tokea yalipoanzishwa mwaka 1992, hivyo alihimiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuangalia namna zitakavyoadhimisha miaka 25 ya ushirikiano huo.

Imetolewa na: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
08 DESEMBA, 2016
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Yun Byung-se. . Mazungumzo hayo yalifanyika jijini Addis Ababa kando ya Mkutano wa Ushirikiano wa nchi za Afrika na Korea.

No comments: