Na Benny Mwaipaja,
WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na
Mipango, Dokta Philip Mpango, amewataka wataalamu wa Mipango na Maendeleo
Vijijini kufanyakazi zao kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na
ufisadi ili kuwawezesha wananchi hususan waishio vijijini kunufaika na huduma
yao ili kujikwamua kiuchumi na kuodokana na umasikini
Dokta Mpango
ametoa rai hiyo wakati wa mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo
Vijijini kilichoko eneo la MIYUJI mkoani Dodoma, ambapo wahitimu 1,641 wakiwemo
wanaume 796 na wanawake 845 wametunukiwa tuzo zao katika kozi 11 zinazohusu
Mipango, Maendeleo, Fedha na uwekezaji.
Amesema kuwa
ubunifu na upangaji mzuri wa mipango ya maendeleo vijijini utaharakisha nia ya
serikali ya kuwaondolea wananchi wake umasikini hivyo kuboresha maisha yao
Waziri huyo wa
Fedha na Mipango, amewahimiza wahitimu hao kuja na mawazo mapya au njia mbadala
za kukabiliana na changamoto za kukuza
shughuli za biashara vijijini, hasa ukosefu wa mikopo na mitaji, bima, mfumo
dume pamoja na mfumo duni wa uzalishaji na ukosefu wa masoko.
“Ninawaasa
wahitimu wetu muwe wazalendo na mfanyekazi kwa bidii kokote mtakako kwenda ili
muwe kioo cha chuo hiki kwasababu Tanzania yetu inawataka muwe wabunifu na
kukataa kujihusisha na mambo yanayohatarisha amani, usalama na umoja wetu kama
watanzania” aliongeza Dkt. Mpango
Aidha, amevishauri
vyombo vya habari nchini kuandika habari za changamoto na fursa zinazowakabili
wananchi vijijini badala ya kuandika na kutangaza mambo yanayodhalilisha nchi
yao kwa kukosekana uzalendo
“Tumeshuhudia mafanikio makubwa waliyoyapata
wakulima kutoka Wilayani Mbulu mkoani Manyara, na Njombe mkoani Iringa ambao
wameongeza uzalishaji wa mazao yao ya vitunguu saumu, mahindi na maharagwe pamoja
na kuongeza thamani ya mazao hayo, hizo ni habari nzuri za kuandika”
alisisitiza
Kwa Upande wake,
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini, Dkt. Frank Hawassi, amesema
kuwa wahitimu wa chuo hicho wameandaliwa katika mfumo unaolenga weledi na
umahiri utakao wawezesha kutekeleza majukumu yao kwa tija zaidi katika maeneo
yao ya kazi.
Amesema kuwa
wahitimu hao wameiva na wako tayari kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa
kimaendeleo katika kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda.
Naye Mwenyekiti wa
Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Razack Lokina, ameiomba serikali
kukisaidia chuo hicho kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa jengo la utawala,
hosteli na upungufu wa wahadhiri ili kukiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa
elimu bora kwa wahitimu wake.
Akizungumza katika
mahafali hayo, Mwanafunzi bora wa shahada ya uzamili, Bi. Gemma Mafwolo,
amesema kuwa wahitimu wa chuo hicho wameiva na wako tayari kutumika mahali
popote hapa nchini kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi
vijijini.
“Tunapenda kukuahidi kuwa tutatumia elimu
tuliyoipata kwa manufaa mapana ya taifa letu kwa kuibua, kupanga, kutekeleza,
kusimamia, kufuatilia na kufanya tathimini ya mipango na maendeleo katika
nyanja zote za maendeleo” alisisitiza Mafwolo
Vilevile
ameishukuru serikali kwa kuahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo
hicho ikiwemo ukosefu wa sehemu za malazi ya wanafunzi, maeneo ya michezo
pamoja na upungufu wa wahadhiri.
Zaidi ya wataalamu
wa mipango ya maendeleo vijijini 14,583, wamehitimu mafunzo yao tangu chuo
hicho cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kianzishwe mwaka 1980 kikisimamiwa na
Wizara ya Fedha na Mkipango.
Katika tukio
jingine, waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amezindua jengo la pili
la taaluma la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini lililojengwa kwa gharama
ya shilingi Bilioni 10.3 lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,250
wanaofundishwa kwa wakati mmoja.
Jingo hilo la
ghorofa 7 lina kumbi 4 za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua watu 320 kila
mmoja, madarasa 6 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kila moja, chumba
kimoja cha maabara ya kompyuta chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kwa
wakati mmoja, ukumbi 1 wa mikuta (80), Stoo 2, kantini 1 na vyumba vya ofisi
32.
Mwisho
Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (Wa pili kulia), akipata maelezo ya Chuo
Cha Maendeleo ya Mipango Vijijini Kampasi Kuu ya Dodoma, kutoka kwa Mkuu wa
Chuo hicho, Dkt. Frank Hawassi (Wa pili kushoto) kabla ya kuanza kwa sherehe ya
Mahafali ya 30 ya Chuo hicho kilichoko eneo la Miyuji, mkoani Dodoma.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (wa pili kulia) akingalia moja ya
machapisho yanayotolewa na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini wakati wa
maonesho ya bidhaa na huduma zinazotolewa na chuo hicho wakati wa Mahafali ya
30 ya kampasi Kuu ya Dodoma. Anayetoa maelezo Kushoto ni Mkuu wa mradi wa Agra
Dkt. Mark Msaki ambaye ni mhadhiri wa chuo hicho.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akiangalia viatu vya ngozi vilivyotengenezwa
na mjasiliamali mdogo Bw. Stephano Chifwaguzi (nayeonesha bidhaa ya ngozi
kiunoni) baada ya kuwezeshwa kiutaalamu na Chuo cha Mipango na Maendeleo
Vijijini, kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya, wakati wa mahafali ya 30 ya Chuo
hicho Kampasi Kuu ya Dodoma.
Mhadhiri wa Chuo
cha Mipango na Maendeleo Vijijini, Ezekiel Kanile (kushoto) akimweleza waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kulia) namna chuo hicho
kinavyosaidia wakulima wa Vitunguu Saumu wilayani Mbulu Mkoani Manyara, wakati
wa maonesho ya Bidhaa na huduma katika Mahafali ya 30 ya Chuo hicho kampasi Kuu
ya Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Mpango (Mb), akiongea na mkulima wa vitunguu saumu Bw. Boniface John, kutoka
Wilayani Mbulu mkoani Manyara (aliyeshika kipaza sauti) wakati akielezea namna
alivyofanikiwa kuongeza thamani ya zao hilo kwa msaada wa Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini, Dodoma wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo hicho yaliyofanyika
katika eneo la Miyuji, mkoani Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Mpango (Mb) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la pili la Taaluma lenye
ghorofa 7 la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampasi Kuu ya Dodoma,
lililogharimu shilingi Bilioni 10.3.
Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Razack
Lokina na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Dkt.
Frank Hawassi wakifurahi kwa pamoja mara baada ya uzinduzi huo.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akimpongeza Mkuu wa Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini, Dkt. Frank Hawassi, kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Jengo la
Taaluma la Chuo hicho lenye urefu wa ghorofa 7, lilojengwa kwa gharama ya
shilingi Bilioni 10.3 zilizotolewa na Serikali, baada ya waziri huyo kulizindua
rasmi jengo hilo.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akiwa na Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Razack Lokina
(Kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Frank Hawassi akiwa wameketi kwe moja ya
kumbi za mihadhara iliyoko katika Jengo la Pili JIpya la Taaluma
lililozinduliwa wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo hicho Kampasi Kuu ya Dodoma.
Mgeni Rasmi katika
Mahafali ya 30 ya Chuo cha MIpango ya Maendeleo Vijijini, Kampasi Kuu ya
Dodoma, Mhe. Dkt Philip Mpango (Mb) pamoja na wahitimu wakiingia kwenye ukumbi
wa J.K Nyerere uliopo Chuoni hapo kwaajili ya Mahafali ya 30 ya Chuo hicho
ambapo wahitimu 1,641, wametunukiwa tuzo mbalimbali ngazi ya Astashada, Stashahada
na Shahada.
Meza Kuu
ikiongozwa na Mgeni Rasmi, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango
(Mb) akifurahia mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini,
yaliyofanyika Kampasi Kuu ya Dodoma katika eneo la Miyuji-mkoani humo.
Wajumbe wa Baraza la kumi na la tisa
la uongozi wa Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo cha
Mipango na Maendeleo Vijijini Kampasi ya Dodoma, iliyoko katika eneo la Miyuji,
mkoani humo.
Wahitimu wa Chuo
cha Mipango ya Maendeleo Vijijini pamoja na wageni waalikwa, wakiimba wimbo wa
Taifa wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika eneo la
Miyuji, mkoani Dodoma
Wahitimu wa Chuo
cha Mipango ya Maendeleo Vijijini pamoja na wageni waalikwa, wawakiwa wamekaa
kwenye ukumbi wa J.K Nyerere uliopo katika Chuo hicho Kampasi Kuu ya Dodoma
wakisubiri kutunukiwa tuzo ama vyeti vyao wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo
hicho yaliyofanyika katika eneo la Miyuji, mkoani Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Mpango (Mb) (katikati) akiwatunuku wanafunzi wa Astashahada na Stashahada
(hawamo pichani) tuzo zao katika kozi kumi na moja katika mahafali ya 30 ya
Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini- Dodoma yaliyofanyika katika ukumbi wa
Mwalimu J.K. Nyerere – Miyungi Dodoma.
Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof.
Razack Lokina na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Frank Hawassi.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akimtunuku shahada mmoja wa wanafunzi
Meza Kuu
ikiongozwa na waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akiwa katika
picha ya pamoja na Baadhi ya wahitimu wa Shahada baada ya kukamilika kwa zoezi
la kuwatunuku tuzo mbalimbali wahitimu wa Mahafali ya 20 ya Chuo cha Mipango ya
Maendeleo Vijijini yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya Dodoma katika eneo la
Miyuji mkoani humo
Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akishukuru kwa Tuzo aliyopewa na
uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa kutambua mchango wake wa
kumsaidia Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwaletea
wananchi Maendeleo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipokea
tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Razack
Lokina, ikiwa ni alama ya kutambua mchango wake katika kuwatumikia wananchi na
kumsaidia Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutekeleza ahadi zake za
kuwatumikia watanzania.
(Picha zote na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment