Friday, December 16, 2016

WANANCHI WA WILAYA YA HANDENI WAHAMASISHWA KUJIUNGA NA MFUKO WA AFYA YA JAMII (CHF) KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU

Wananchi Wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wamehamasishwa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF ili kupunguza gharama za matibabu na kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wote pindi huduma ya Afya inapohitajika.

Hayo yalisemwa na Afisa Tawala Wilaya Bi. Upendo Magashi alipokuwa kwenye kampeni  ya uhamasishaji wa wananchi  kujiunga na kuwa wanachama wa mfuko wa afya ya jamii wa hiari  CHF ili kupunguza gharama za matibabu, uliobeba kauli mbiu ya KUKU MMOJA MATIBABU MWAKA MZIMA.

Aliwaeleza wananchi kuwa, kuku mmoja anayegharimu shilingi 10000, anaweza kusaidia kaya moja yenye watu sita kujiunga na mfuko wa  Afya ya jamii CHF, ambao watapata matibabu bure kwenye vituo vya Afya kwa ngazi ya Wilaya mwaka mzima. Aliwataka waratibu wa mfuko wa Afya CHF, Wataalamu wa afya, na viongozi mbalimbali kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi ili kuweza kuwasaidia juu ya umuhimu wa mfuko huo ikiwa ni pamoja na kujibu  hoja zao kwa kuzitafutia ufumbuzi.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya  Wilaya ya Handeni Bw.Credianus Mgimba aliwaeleza wananchi kuwa faida mojawapo kubwa ya kujiunga na mfuko wa CHF ni kusaidia upatikanaji wa dawa za kutosha kwenye vituo  vya huduma za afya. Wanachama wakiwa wengi itasaidia uwepo wa dawa za kutosha kwani fedha itakayokusanywa itakuwa nyingi itakayosaidia upatikanaji wa dawa mbalimbali  na wanachama wakiwa wachache tatizo la upungufu wa dawa halitakwisha.

Aidha  wananchi walielezwa kuwa kuwa kuna thamani kubwa sana wakiwa wanachama wa mfuko wa afya ya jamii  hasa kwa kaya zisizojiweza kwani husaidia katika kipindi kigumu iwapo mgonjwa atakosa fedha za matibabu. kwa kutumia kadi ya  CHF ataweza kupata matibabu tofauti na kutokuwa mwanachama hali ambayo wakati mwingine hupelekekea hata mtu kupoteza uhai kwani wananchi wengi  hawana uwezo wa kujigharamia matibabu. Lengo ni kuhakikisha kila mwananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni  anakuwa na uhakika wa huduma ya afya.

 Wananchi walisisitizwa pia kuwahudumia wazee kwani kumekuwa na changamoto za huduma ya Afya kwa wazee hasa linapokuja suala zima la matibabu. Wameelezwa  kuwa ili wazee waweze kuhudumiwa kila kijiji kinapaswa kuchangia laki mbili (200,000) ili iweze kusaidia dhana ya huduma bure ya afya kwa wazee ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa zinazolenga wazee peke. Mpango huo umepitishwa na baraza la madiwani lililofanyika mwisho mwa mwezi wa kumi na moja hivyo utekelezaji wake unatarajiwa kuanzia januari mwaka 2017.

 Faida za  mfuko huo wa  Afya ya jamii CHF ni pamoja na kupunguza gharama kama za kufungua faili, kumuona daktari na kununua dawa hauta kuwepo hali itakayopelekea uhakika wa afya kwa familia nzima.
  
Mpaka sasa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ina kaya wanachama  22,532 wa mfuko wa afya ya jamii CHF, Malengo ni kufikia kaya wanachama  26,152 ifikapo June 2017. Uhamasishaji huo ulifanywa kwenye kata saba za Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambapo mwananchi aliyejiunga siku ya uhamsishwaji alitengenezewa na kupewa kadi papohapo. Kata hizo ni  Segera, Kiva, Kabuku, Komkonga,Kang’ata, Mkata na Kwamsisi.

Kampeni hii inaongozwa na Mhe. Mkuu wa Wilaya na ni  endelevu lengo likiwa ni kuwafikia wananchi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Awamu ya kwanza imemalizika.

...............................
Alda Sadango
Afisa Habari,Halmashauri ya Wilaya Handeni.


 Afisa Tawala Wilaya Bi. Upendo Magashi akizungumza na wananchi wa Kata ya Kabuku kuhusu faida za CHF
 Bi.Upendo Magashi akitoa mfano kwa kumzawadia mmoja wa wananchi wa kata ya Segera elfu kumi iliyomuwezesha kujiunga na CHF
 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Credianus Mgimba akizungumza na wananchi wakati wa uhamasishaji
 Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Bw. Salumu Masokola akiwaeleza wananchi umuhimu wa mfuko wa afya ya jamii  CHF.
 Mwenyekiti kamati ya Elimu, Afya na Maji Bw. Joel Mabula akiwahamasisha wananchi wakati wa kampeni hiyo
 Mratibu wa mfuko wa Afya ya jamii CHF wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Godfrey Vedasto akiwaeleza wananchi faida za CHF.
baadhi ya wananchi walioshiriki kampeni ya uhamasishaji wa CHF






No comments: