Friday, December 23, 2016

RC SHINYANGA AFANYA ZIARA WILAYANI KISHAPU, AAGIZA MIRADI IKAMILIKE KWA WAKATI ULIOPANGWA

 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) akikagua mojawapo ya nyumba za walimu zinazojengwa katika Shule ya Sekondari Mwamashele wilayani humo.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) akisisitiza jambo wakati akizungumza na watendaji na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya alipotembelea Kata ya Kiloleli. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya  Kishapu, Nyabaganga Taraba.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (mbele) akitembelea mifugo ya mmoja wa wafugaji wilayani humo wakati wa ziara yake.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala alipowasili Kata ya Kiloleli.
 Mhandisi wa Ujenzi Wilaya ya Kishapu, Samson Pamphil (kushoto) akitoa maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa vyoo katika Kata ya Mwamamalasa kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack. Katikati ni Diwani wa kata hiyo, Justine Sheka.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (katikati) akizungumza na watendaji alipofika Kata ya Mwamalasa wakati wa ziara yake. Wengine pichani wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya  Kishapu, Nyabaganga Taraba, Diwani wa kata hiyo, Justine Sheka na  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack amefanya ziara katika Wilaya ya Kishapu na kukagua miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Telack alikagua ujenzi wa mradi wa nyumba za walimu kata ya  Kiloleli na vyoo kata za Mwamalasa, Masanga na Mwakipoya inayoendelea.
Aliagiza miradi hiyo iwe imekamilika kabla ya Desemba 31 mwaka huu huku akionya tabia ya wakandarasi kuchelewesha miradi ya maendeleo wakati tayari wamekwisha lipwa fedha.
“Nataka kuona miradi hii imekamilika na tunajua agizo hili lilishatolewa na Waziri wa TAMISEMI siku nyingi, wahandisi hamieni site kuhakikisha miradi inakamilika,” alisema Telack.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa katika ziara hiyo ya siku moja akiwa ameambatana na wataalamu kutoka halmashauri ya wilaya na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya aliwataka waendelee kusimamia miradi ya maendeleo.
Kwa upande mwingine alikemea utoro mashuleni huku akiagiza wazazi wasiopeleka watoto shule ifikapao Januari wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisema kuwa kwa sasa Serikali inaendelea na utaratibu wa kutoa elimu bure hivyo ni lazima wazazi wapeleke watoto shule kupata elimu na baadaye kulisaidia taifa.
“Nakuagiza mkuu wa shule hakikisha wanafunzi wote wanafika shule, hosteli ipo sasa kwanini wanafunzi hawafiki shule kwa hiyo nakupa kazi hiyo,” alisisitiza.

No comments: