Wednesday, December 14, 2016

PROF. MBARAWA ASHUSHA NEEMA VIWAJA VYA NDEGE

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG), anayejenga jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Yuzhang Xiong, wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa ujenzi huo.
 Meneja Mipago, Ubunifu na Tathimini wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Eng. Mbila Mdemu akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, kuhusu mradi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza.
 Muonekano wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kinachojengwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG), ambapo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwakani.
 Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Salum Msangi akieleza mikakati ya utekelezaji wa upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini. Pembeni yake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
 Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), mkoa wa Mwanza, Eng. Marwa Rubirya akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa upanuzi wa sehemu ya barabara ya Mwaloni-Furahisha yenye urefu wa Mita 725, wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja la Furahisha na upanuzi wa Barabara ya Makongoro-Uwanja wa Ndege,  mkoani Mwanza.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiongea na wakazi wa Pasiansi wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja la Furahisha na upanuzi wa Barabara ya Makongoro-Uwanja wa Ndege, mkoani Mwanza.
Muonekano wa Daraja la Furahisha mkoani Mwanza, ambalo linatarajiwa kukamilika mwazoni mwa mwezi Januari mwakani. Ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80.


Serikali imeanza ujenzi na upanuzi wa viwanja 11 ikiwa ni hatua ya kuendelea kuboresha na kukuza usafiri wa anga hapa nchini.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege cha Mwanza, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 150 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya upanuzi wa viwanja hivyo.Ameongezeza kuwa miradi itakayotekelezwa katika viwanja hivyo ni pamoja na ujenzi wa majengo ya abiria na upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege.

"Maboresho ya miundombinu ya viwanja vya ndege yatachochea ongezeko la pato la Taifa, hivyo basi Serikali imeonesha nia ya dhati katika kuhakikisha usafiri huu utakuwa ni wa uhakika na nafuu kwa wananchi”, amesema Profesa Mbarawa.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amevitaja baadhi ya viwanja hivyo kuwa ni kiwanja cha ndege cha Shinyanga, Tabora, Sumbawanga, Kigoma, Mtwara, Songea na Iringa.

Kuhusu ujenzi wa Jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha  Mwanza, Profesa Mbarawa amesema kuwa Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 7.6 kwa ajili ya kumlipa mkandarasi na msimamiz wa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwakani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Salum Msangi amesema Mamlaka itaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watanzania wanapata huduma zilizo bora na kukuza pato la Taifa.

Ameahidi kuendelea kutatua changamoto ya ndege hai wanaohatarisha uharibufu wa miundombinu za injini za ndege katika uwanja huo ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha usalama wa anga na watumiaji wake.

Naye, Mkandarasi wa Kampuni ya Japan Engineering Construction Group (JECP), anayejenga jengo hilo, Yuzhang Xiong, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kwani kwa sasa jengo limefika  katika hatua nzuri.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ametembelea Daraja la Furahisha na barabara ya makongoro  hadi uwanja wa ndege yenye urefu wa kilomita tano na kusema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kupunguza foleni kwa watumiaji wa vyombo vya moto na  ajali kwa watembea kwa miguu.

Aidha, amefafanua mradi huo kuwa umegawanyika katika sehemu tatu ambapo kwa sasa sehemu ya tatu ya mradi huo iliyoanza inahusisha upanuzi wa barabara ya Mwaloni hadi Furahisha Mita725 na ujenzi wa barabara ya Pasiansi hadi Uwanja wa Ndege (km 5) kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Prof. Mbarawa amewataka wananchi kutunza na kulinda miundombinu hiyo ambapo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharamia utekelezaji wa miradi hiyo.

Amewaagiza uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Mwanza kumsimamia mkandarasi wa kampuni ya Nyanza Roads anayejenga barabara hiyo kujenga kwa kiwango kilicho bora ili  kuweza kushawishi Serikali kuwapatia tenda za miradi mengine.

Meneja wa TANROADS, mkoa wa Mwanza, Eng. Marwa Rubirya amesema kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi wa Daraja la Furahisha umefikia asilimia 80 ambapo ujenzi wa daraja na ufungaji wa vyuma umekamilika na unatarajiwa kukamilika mwanzoni  mwa mwezi Januari.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments: