Sunday, December 18, 2016

PROF. MBARAWA AAGIZA BARABARA YA MAKUTANO-NATA YA KM50 IKAMILISHWE

 Mhandisi Mshauri Eng. Domicus Mapunda wa Kampuni ya Ujenzi ya Mbutu Bridge JV akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Makutano-Nata KM 50 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Mara wakati alipokagua mradi huo.
Muonekano wa barabara ya changarawe ya kuruka na kutua ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Musoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewapa miezi minne Wakandarasi Wazawa wa Kampuni ya Ujenzi ya Mbutu Bridge JV inayojenga barabara ya Makutano-Nata kukamilisha km 18 kati ya 50 za barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Agizo hilo limetolewa na Waziri huyo, alipokuwa akikagua mradi huo wa barabara inayoanzia makutano kupitia Butiama, Nyamuswa hadi Sanzate ambao upo katika mkoa wa Mara, na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambayo imesuasua kwa takriban miaka 3 sasa.
"Nataka mwezi Aprili mwakani sehemu ya barabara hii iwe imeshakamilika kwa kiwango cha lami na wananchi waanze kufurahia matunda yake, hatuwezi kusubiri kwa muda wote huo kuwavumilia kukamilisha mradi huu”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza kuwa nia ya Serikali ya kuboresha barabara hiyo ni kupunguza gharama za usafirishaji, kuboresha makazi, kukuza uchumi kwa maeneo yaliyo kando ya Barabara hiyo na kuhamasisha utalii kwenye mbuga za Wanyama za Serengeti na Ngorongoro.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Mara Eng. Japherson Nnko amesema kuwa barabara hiyo itakapomalizika itakuwa na njia ya magari yenye upana wa mita6.5, mabega ya barabara ya mita 1.5 kila upande na Daraja kubwa la Kyarano lenye urefu wa mita 37.5.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema itawapa kipaumbele makandarasi wazawa kuweza kushiriki katika mradi wa ujenzi wa reli mpya ya kisasa (Standard Gauge), inayotarajiwa kuanza hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali imewataka Makandarasi hao kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa  kwa kuomba zabuni za ujenzi huo na kuziimarisha kampuni zao ikiwemo kuwa na vifaa vilivyo bora ili kupambana na soko la kibiashara na makandarasi wa nje.
Sambamba na hayo, Waziri Prof. Mbarawa amekagua Uwanja wa Ndege wa Musoma na kusema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inapanua na kujenga kwa kiwango cha lami uwanja huo hususani njia ya kuruka na kutua ndege  kutoka KM 1.6 ya sasa  hadi KM 1.8 ili kuruhusu ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba abiria 70  kutua katika uwanja huo.
Waziri Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku mbili mkoani Mara ambapo amekukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake katika Wilaya ya Bunda, Butiama, Musoma Mjini na Serengeti.

Imetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na 
Mawasiliano, kitengo cha Mawasiliano Serikalini

No comments: