Tuesday, December 6, 2016

PAMPU ZILIZOKO NDANI YA MITA 500 KUTOKA KWENYE CHANZO CHA MAJI CHA QANGDED ZIWE ZIMEONDOLEWA IFIKAPO SAA 12.00 JIONI YA LEO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi. Theresia Mahongo kuhakikisha mashine zote za kupampu maji zilizoko ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo cha maji cha Qangded ziwe zimeondolewa ifikapo saa 12.00 jioni ya leo na atakayekaidi atachukuliwe hatua za kisheria.
Amesema kitendo cha kuweka mashine za kupampu maji karibu na chanzo hicho na kuvuta maji kwenda kwenye mashamba yao kinasababisha maji kushindwa kufika katika mashamba ya wakulima wengine hivyo amewataka wafuate utaratibu uliowekwa na waendeshaji wa mradi huo.
Waziri Mkuu ametoa agizo leo (Jumatatu, Desemba 5, 2016)  wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha  Jobaji kata ya Baray wilayani Karatu, ambapo amesema Serikali haitavumilia kuona mtu mmoja akivuruga mradi huo wa umwagiliaji.
Amesema ili kuhakikisha mradi huo wa umwagiliaji unakuwa endelevu lazima chanzo cha maji kilindwe na wananchi wasiruhusiwe kufanya shughuli za kijamii karibu na chanzo na badala yake wasogee umbali wa mita 500.
"Sitaki kuona mashine zikipampu maji ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo na badala yake wakulima wote wafuate taratibu zilizowekwa . Lazima chanzo kilindwe kwa sababu maji yakikauka mazao nayo yatakauka, hivyo tutakosa chakula jambo ambalo hatutaki litokee. Mkuu wa wilaya kesho nenda kafanye ukaguzi katika chanzo ukikuta mashine kamata," amesema.
Awali, Waziri Mkuu  alizindua mradi wa maji safi na salama wa kijiji cha Jobaj unaotekelezwa na shirika la World Vision Tanzania uliogharimu sh. milioni 285. Mradi huo utahudumia vijiji vitatu vya Kata ya Baray ambavyo ni Mbunga Nyekundu, Jobaj na Dumbechand.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Wolrld Vision Tanzania, Bw. Revocutus Kamara amesema mradi huo unatokana na hitaji kubwa la maji katika vijiji hivyo vitatu na uwepo wa kisima kirefu cha maji kilichochimbwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mwaka 2009.
"Mradi huu wa maji unatekelezwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ilianza Machi hadi Novemba 2016, ambapo  wakazi 5,272 ikiwa ni pamoja na taasisi nne za Serikali ambazo ni Zahanati, Magereza, shule ya msingi na sekondari zilizoko katika kijiji cha Jobaj wananufaika kwa kupata maji safi na salama," amesema.
Amesema awamu ya pili na ya tatu ya mradi huo itaanza Disemba 2016 na itagharimu zaidi ya shilingi milioni 200.
Akizungumza kuhusu mradi wa umwagiliaji Mkurugenzi huyo amesema shirika lao limechangia kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga kilomita 1.716  za mfereji katika kijiji cha Jobaj (kilomita moja) na Dumbechand (mita 716) ambapo umegharimu zaidi ya sh. milioni 210 na inalenga kunufaisha zaidi ya wakulima 4,450 wa vijiji hivyo.
Amesema mifereji hiyo itawezesha wakulima katika vijiji hivyo kuwa uhakika wa upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya chakula na biashara hivyo itasaidia kupunguza migogoro ya maji, kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 803 hadi hekta 1,203.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATATU, DESEMBA 5, 2016.

No comments: