Saturday, December 31, 2016

MBUNGE WA MKURANGA AOMBA RAIS MAGUFULI KUFUTA HATIMILIKI YA SHAMBA LENYE HEKARI 2472 LINALODAIWA KUMILIKIWA NA WAWEKEZAJI

MBUNGE wa Jimbo la Mkuranga Mkoani Pwani, Abdallah Ulega amemuomba Rais Dkt. John Magufuli kufuta hatimiliki ya shamba lenye hekari 2472 linalodaiwa kumilikiwa na wawekezaji wenye asili ya Kiasia baada ya wawekezaji hao kushindwa kuliendeleza kwa muda mrefu na badala yake wapewe wananchi.
Hayo ameyasema leo jimboni humo wakati wa mkutano kati ya wananchi na kamati ya usalama ya wilaya hiyo uliokuwa na lengo la kujadili shamba hilo linaloonekana kutishia usalama wa raia pamoja na mali zao.
Alisema shamba hilo lilitelekezwa kwa kipindi kirefu na wawekezaji hao, hali iliyopelekea wakazi wa kata ya Tambani pamoja na Mipeko kuyaendeleza kwa kufanya ujenzi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Ulega alisema Wakazi wa maeneo hayo waliweza kutafuta hati miliki ya maeneo waliyokuwa wanamiliki kwa kipindi chote na kushangazwa na kitendo cha wamiliki hao kuwataka kutoka katika maeneo yao kwa madai kuwa wakazi takribani 45,000 wamevamia eneo hilo.
Alidai wananchi wa vijiji vya Mlamleni, Luzando, Mwanambaya pamoja na Mipeko wamekuwa katika hali ya taharuki toka walipopewa notisi ya siku 21 ya kuwataka waondoke katika maeneo hayo ambayo wameyaendeleza kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

"Mi najua Rais wetu ni msikivu na anaweza kuzifanyia kazi kero za wananchi kwa wakati, na kero hii ya kwenye hivi vijiji vyetu anapaswa kutilia mkazo kwa sababu wananchi wa vijiji hivi wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi na hata kujadili shughuli za maendeleo kwa sasa hakuna kabisa kwa kuogopa hawa watu wawili wanaotaka kutudhurumu haki zet," alisema Ulega.

Aliongeza anaamini kuwa Rais sio kabaila na kamwe hatoweza kukaa upande wa makabaila ambao wanategemea kuwalalia wananchi na kujiingizia pesa kupitia wao.

Hata hivyo Ulega alimueleza Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga kumuagiza Ofisa Ardhi wa wilaya hiyo kumuandikia notisi ya siku 90 ili kueleza wapi hilo shamba lililo na ni kwa nini hawakuliendeleza kwa muda wote huo.

Pia alimueleza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutoruhusu kampuni ya 'Ardhi Plan' kupima maeneo ya wilaya hiyo kwani kama ataruhusu kampuni hiyo kufanya upimaji watapelekea kutokea kwa vurugu ambazo zinaweza kusababisha hali ya amani na utulivu kutokuwepo katika wilaya hiyo.

Kwa Upande wake Mkuu wa wilaya hiyo ya Mkuranga, Philberto Sanga aliwataka wakazi wa vijiji hivyo kukaa vikao vya kutayarisha mihutasari ya kuipeleka katika ngazi za juu ili Rais kufuta hati ya maeneo hayo ambayo yamekuwa msaada kwa wananchi hao kwa muda mrefu.

Alisema Viongozi wa vijiji hivyo wanapaswa kuhakikisha shughuli zote za upimaji ardhi katika vijiji hivyo vilivyodaiwa kumilikiwa na wamiliki hao wa kiasia zinasitishwa mpaka pale taratibu mbalimbali zitakapokamilishwa.

Aliongeza kuwa hatokubali kuona ardhi hiyo ikimilikiwa na watu wawili wenye kutumia fedha na badala yake atahakikisha haki inapatikana kwa wananchi hao kwa kupata ardhi yao.

Sanga alisema viongozi wa vijiji hivyo wanapaswa kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayeweza kufanya maamuzi ya aina yoyote katika vijiji hivyo pasipo kupata ruhusa na kibali kutoka katika ofisi za Serikali.
Mbunge Jimbo la Mkuranga,Abdallah Ulega akizungumza na wananchi wa Mwanambaya, Luzando, Mipeko na Mlamleni juu ya kumuomba Rais Dkt. John Magufuli kufuta hatimiliki ya shamba lenye hekari 2472 linalodaiwa kumilikiwa na wawekezaji wenye asili ya Kiasia baada ya wawekezaji hao kushindwa kuliendeleza kwa muda mrefu na badala yake wapewe wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Filberto Hassan Sanga wapili kutoka kushoto akiwasili katika mkutano uliofanyika leo mkoani Pwani.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga, Msham Munde akizungumza na wananchi wa Mwanambaya, Luzando, Mipeko na Mlamleni katika mkutano uliofanyika leo mkoani Pwani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Juma Abeid akizungumza na wananchi wa Mwanambaya, Luzando, Mipeko na Mlamleni katika mkutano uliofanyika leo mkoani Pwani.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Salum Ally Papen akifafanua jambo kwenye mkutano uliofanyika leo mkoani Pwani. 
Baadhi ya wananchi wa Mwanambaya,Luzando,Mipeko na Mlamleni wakimsikiliza Mbunge Jimbo la Mkuranga,Abdallah Ulega, Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii.

Mamia ya wananchi  katika mkutano huo uliofanyika leo mkoani Pwani. 
Picha zote na Emmanuel Massaka, Globu ya Jamii.

No comments: