Sunday, December 4, 2016

Mamia wamuaga Mzee Mzimba, azikwa kijijini kwake Msoga

 Jeneza lililokuwa na mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Yanga Asili, marehemu Yusuf Mzimba nyumbani kwa mtoto wake Magomeni jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwa mazishi katika kijiji cha Msoga, Chalinze mkoani Pwani. (Picha na Francis Dande).
 Mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga na  Taifa Stars,  Abeid Mziba (kushoto), akimfariji Ramadhan Yusuf 'Kampira' ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Yanga Asili, marehemu Yusuf  Mzimba jijini Dar es Salaam jana, kabla ya mwili wake kusafirishwa kwa mazishi Msoga, Chalinze Mkoa wa Pwani. 

Mzee Ibrahim Akilimali (kushoto), akifurahia jambo na wazee wenzake katika msiba wa mzee Yusuf Mzimba. Katikati ni Said Motisha.
 Kisomo kikisomwa.
 Mzee Ibrahim Akilimali akisoma wasifu wa marehemu Yusuf Mzimba.
 Wakiombea Dua mwili wa marehemu.
 Safari ya kuelekea Msoga ikianza.

NA FRANCIS DANDE
 MAMIA ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, jana walijitokeza kwa wingi kuaga mwili aliyekuwa Mwenyekiti wa Kundi la Yanga Asili, marehemu Yusuf Mzimba, uliosafirishwa kutoka nyumbani kwa mtoto wake, Ramadhan Yusuf ‘Kampira’, Magomeni jijini Dar es Salaam leo.
Marehemu alifariki juzi na amezikwa jana katika makaburi ya familia yaliyopo kijijini kwake, Msoga, Chalinze, mkoani Pwani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mtoto wa marehemu mzee Mzimba, Kampira alisema kuwa baba yake  alikuwa anasumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu na kwamba ameacha watoto sita.
Kampira aliongeza kuwa, Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete ataongoza waombolezaji katika maziko hayo, yatakayofanyika katika makaburi ya familia yaliyopo kijijini Msoga.
Akisoma wasifu wa marehemu, Mzee Ibrahim Akilimani alisema kwamba marehemu alikuwa mwanachama wa siku nyingi wa Yanga na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika klabu ya Yanga ikiwemo nafasi ya umeneja.
Alibainisha ya kuwa, Mzee Mzimba aliwahi pia kuwa Katibu Mwenezi wa Yanga na mtu ambaye alikuwa na misimamo katika kuipenda Yanga na hakubadilika katika kuitetea klabu yake ya Yanga. 
Pia alitoa mchango mkubwa ndani ya Yanga na hasa ulipotokea mgawanyiko mkubwa uliodumu kwa miaka 7 na kuibuka makundi ya Yanga Asili na Yanga Kampuni. 
Mzee Akilimali aliongeza kwamba, licha ya kuibuka kwa migogolo ndani ya klabu hiyo, lakini Mzee Mzimba alibaki na msimamo wake mpaka leo na kuwa Yanga kitu kimoja.
“Mtu kama Yusuf Mzimba alivyokuwa maarufu kwa Yanga leo hebu nitazamieni hao viongozi wa Yanga wako wapi, tumeondokewa na wapenzi wa Yanga kama Ismail Idrissa, Bilal Hemed Chakupewa hakuonekana hata kiongozi hata mmoja, naamini hata Ibrahim Akilimali akifa, hatoonekana kiongozi yeyote wa Yanga,” alisema.
Mzee akilimali alisema kuwa Yanga ilianzishwa na wazee mwaka 1935 ikiwa na lengo la kujuana, kuzikana, kusaidiana kufurahi pamoja, lakini leo imekuwa hawajuani. 
Aidha amewasihi wana Yanga kutopoteza adhima ya kuanzishwa kwa klabu hiyo.
Naye mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Abeid Mziba alisema kuwa: “Katika miaka ya 80 wakati najiunga na Yanga, Mzee Mzimba ni miongoni mwa wazee walionipokea, kwa kweli tumepoteza nguzo muhimu sana ndani ya Yanga na katika familia ya mpira kwa ujumla.”
Naye Mzee wa Yanga, Hashim Mhika alisema kuwa alimfahamu siku nyingi mzee Mzimba kutokana na misimamo yake pia alisema kuwa katika serikali ya Kikoloni, Mzee Mzimba aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya (DC), lakini, ameshangazwa kuona hata viongozi wa serikali hawakuonekana katika msiba huo.

No comments: